Said Mwishehe
KABLA ya kwenda mbali naona namna ambavyo tutaingia kwenye utamaduni wa baadhi ya wazazi au familia kukaa kikao cha siri kwa ajili ya kutafuta daktari ili awe na kazi moja tu ya kutoa mimba ya binti wa darasa la sita, saba au hata wa kidato cha kwanza na cha pili.
Unashangaa nini? Shauri yako kwani hujamsikia Mkuu wa Kaya alivyotoa maagizo yake? Wee unakaa nchi gani hadi mambo muhimu yanakupita? Usikilizi redio? Husikilizi wenzako wanazungumzia nini vijiweni? Shauri yako kaa vivyo hivyo.
Rais John Magufuli amesisitiza hakuna mwanafunzi atakayepata ujauzito na kuruhusiwa kuwa shuleni ndani ya uongozi wake.
Isiwe tabu acha nikukumbushe ambacho kinaendelea kwenye nchi yetu kwa sasa.Achilia mbali habari ya mchanga wa madini. Habari iliyopo ni kwamba mwanafunzi wa kike ambaye atapata mimba akiwa shule ya msingi au sekondari ni marufuku kuendelea na masomo.Unashtuka nini? Ndio tayari maagizo yameshatoka tena kilichobaki ni utekelezaji.
Baada ya kauli hiyo ya Mkuu wa Kaya kuwa kwenye utawala wake ni marufu mwanafunzi mwenye mimba kuendelea na masomo, Kwa Ujinga Wangu moja kwa moja nikawaza wale wanafunzi ambao walibakwa na wanaume wenye uchu na kisha wakapata ujauzito nafasi yao iko wapi?
Wafanye nini maana wamebeba mimba si kwa hiyari yao bali kuna mijitu imefanya ukatili kwa kubaka binti ambaye alikuwa na malengo yake kwenye elimu.
Kwa Ujinga Wangu nikaanza kuwaza namna ambavyo wapo wanafunzi wanapata mimba si kwasababu ya kupenda bali hali ngumu ya maisha inamfanya ajikute akijiingiza kwenye vitendo vya ngono na matokeo yake mimba.Jamani, jamani, jamani sijui itakuaje huko mtaani.
Binafsi naiona nia njema ya Mkuu wa Kaya ya kuhakikisha waliopata fursa ya kwenda shuleni wanaitumia nafasi hiyo kwa ajili ya kujikita kwenye masuala yanayohusu elimu tu. Hataki kuona mwanafunzi badala ya kufikia somo la kesho anafikiria namna ya kwenda kliniki au kulea mtoto.
Kwa Ujinga Wangu naiona changamoto ya utekelezaji wa maagizo hayo. Lakini kabla ya kuendelea pia nafahamu utaratibu uliopo hivi sasa wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shuleni baada ya kujifungua walikuwa wanaendelea na masomo.
Lengo la kufanya hivyo ilikuwa ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kusoma.Kila jambo na wakati wake na hivi sasa naona utaratibu huo wakati wake umefika mwisho.Atayakayepata mimba ajue kwenye elimu ya msingi na sekondari amejiondoa. Duh!
Pata picha familia imejinya kwa ajili ya kuhakikisha binti yao anapa elimu ya sekondari na kabla ya kumaliza kidato cha nne anapata mimba. Ujue nini kitatokea. Kwa Ujinga Wangu naona kabisa ambavyo wazazi au walezi ambavyo wataungana kwa ajili ya kumuita daktari ili atoe mimba ili binti yao aendelee na masomo.
Unakunja uso sawa ila huo ndio ukweli na ndicho ambacho kitatokea.Najua si wazazi wote wanaweza kufanya hivyo lakini kwa sehemu kubwa hawatasita kuchukua hatua hiyo.
Fanya utafiti mdogo tu utabaini licha ya kwamba wanafunzi waliokuwa wanapata mimba kuendelea na masomo bado baadhi ya familia hazikuwa zinataka jamii ijue. Sasa ndio maagizo yametoka unatarajia nini?
Watanzania wanafahamu umuhimu wa elimu na wanatamani kuona wanairithisha kwa watoto wao iwe wa kike au wa kiume. Kuna mambo yatatokea tu na usishangae suala la utoaji mimba nchini litaongezeka.
Sitaki kuudhi wengine lakini naaomba nieleze hivi kwa lugha rahisi ni hivi zipo roho za Watanzania ambazo zitaondolewa zikiwa tumboni ili kufanikisha ndoto za Watanzania wengine walioko mashuleni.
Nishauri tu kwa wazazi na walezi kuwa kinachotakiwa ni kuwa karibu na wanafunzi hasa wa kike kuhakikisha wanakuwa salama na hawajiingizi kwenye matendo yanayohusu ngono ambazo madhara yake itakuwa pamoja na kukosa elimu ya msingi au sekondari.
Wazazi lazima wakae na watoto wao bila kuona aibu kueleza ukweli kuhusu kukaa mbali ya wanaume si tu wa mtaani hata wale wa shuleni. Pia kutocheka na walimu wa kiume kwani baadhi yao wamekuwa wakiwapa wanafunzi mimba.
Zipo kesi nyingi tu za baadhi ya walimu wa kiume kuwapa mimba wanafunzi wa kike. Kwa Ujinga Wangu natamani kuwe na sheria kali ambayo itachukuliwa dhidi ya mwanaume ambaye atabainika kumpa mimba mwanafunzi. Hii itasaidia kukomesha mimba kwa wanafunzi.
Kwa sasa naona kama adhabu imewekwa kwa mwanafunzi wa kike tu.Kwa Ujinga Wangu natamani Mkuu wa Kaya atoe kauli hata kwa watakaobainika kuwapa mimba wanafunzi hatua gani zichukuliwe.
Tuanze na kaulimbiu mimba kwa wanafunzi mashuleni sasa basi.Hakuna njia ya mkato maana maagizo wote tumeyasikia. Jamaa yangu mbona umenuna vipi? Nimekukera? Basi samahani maana huu ni Ujinga Wangu acha hasira na hakikisha mwanafunzi wa kike hapati mimba akiwa shuleni.
Kwa maoni 0713 833822
SHARE
No comments:
Post a Comment