Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi akiupokea mwenge wa uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma Jordan Rugimbana mapema katika kijiji cha Sanza Wilayani
Manyoni.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa
uhuru kitaifa Amour Hamad Amour na mkimbizi mwenge kitaifa Fredrick
Ndahani (ambaye ni mwana Singida) wakiendesha pikipiki zitakazotumiwa na
waratibu wa sekta binafsi mkoani singida wakati wa uzinduzi wa Mkakakti
huo.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa
uhuru kitaifa Amour Hamad Amour akishona nguo mara baada ya kuzindua
kikundi cha ushonaji katika kijiji cha Nkonko Wilayani Manyoni.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt
Angelina Lutambi akiwa ameubeba mwenge wa uhuru mara baada ya
kukabidhiwa Mkoani Singida Mapema leo katika kijiji cha Sanza Wilayani
Manyoni.
Mkimbizi Mwenge kitaifa Fredrick
Ndahani (ambaye ni mwana Singida) akiendesha pikipiki zitakazotumiwa na
waratibu wa sekta binafsi mkoani singida wakati wa uzinduzi wa Mkakakti
huo.
…………………………………………………………………………….
Mwenge wa uhuru umezindua
rasmi mkakati wa kuboresha sekta binafsi mkoani Singida kwa kuwa na
madawati ya kuratibu sekta hizo ili kufikia uchumi wa kati wenye
viwanda.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa
uhuru kitaifa Amour Hamad Amour na mkimbizi mwenge kitaifa Fredrick
Ndahani (ambaye ni mwana Singida) wamezindua mkakati huo kwa kukabidhi
pikipiki mbili kati ya saba kwa maafisa maendeleo ya jamii ambao ndio
waratibu wa madawati hayo.
Akitoa maelezo ya Mkakati huo
mara baada ya kuupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoani Dodoma, Mkuu wa
Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema ushirikiano baina ya
serikali na sekta binafsi utaufikisha Mkoa wa Singida katika azma ya
kuwa na uchumi wa kati pamoja na viwanda.
Dkt Nchimbi amesema usafiri huo
wa pikipiki unalenga kuwawezesha waratibu wa sekta binafsi kila
halmashauri Mkoani Singida kutembelea na kutambua changamoto, fursa na
mafanikio ya sekta binafsi na sio kusubiria ofisini waletewe taarifa au
malalamiko.
“Dawati litatambua kwa takwimu,
mahali, aina ya shughuli na hali ya uzalishaji ili kuhakikisha ushiriki
mtambuka unaowajibika ipasavyo ikiwemo kutoa taarifa ya soko la mazao
mbalimbali. Lengo ni kurahisisha uwekezaji mkoani kwetu”, amesema Dkt.
Nchimbi.
Amesema Mkoa wa Singida unazo
fursa za uwekezaji katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa hasa
vitakavyolenga kuongeza thamani ya mazao kutokana na uzalishaji mzuri wa
mazao kama ya vitunguu, alizeti na asali mkoani hapa.
Dkt Nchimbi amesema sambamba na
mkakati huo mwenge wa uhuru umezindua mkakati wa kutunza mazingira wenye
kauli mbiu ya ‘achia shoka kamata mzinga’ ambapo mkoa umetoa mizinga ya
nyuki kwa wachoma mikaa.
Amesema mkakati huo umewalenga
hasa wachoma mikaa ambao wamekiri kuwa waharibifu wa mazingira kwa
kukata miti hovyo hivyo wamekubali kufuga nyuki kwa ajili ya
kujitengenezea kipato cha uhakika huku wakitunza mazingira.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio
za mwenge wa uhuru kitaifa Amour Hamad Amour ameupongeza uongozi wa Mkoa
wa Singida kwa ubunifu huo unaolenga kuboresha mazingira ya kufanikisha
lengo la kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.
Amesema jitihada hizo za vitendo
zinaonyesha wazi ushirikiano mzuri na kudhihirisha namna wanavyomuunga
mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano katika kufanikisha kuinua uchumi wa
taifa.
Aidha amewapongeza wananchi wa
Singida kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha mazao ya kutosha,
amewasisitiza kuendelea kumuunga mkono Rais pamoja na kutunza umoja na
amani ya Taifa.
Aidha kiongozi wa mbio za mwenge
wa uhuru Amour Hamad Amour, amefurahishwa na namna wilaya ya Manyoni
ilivyokuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha dhana ya Tanzania ya
viwanda inatekelezwa kwa vitendo.
Amour ametoa pongezi hizo wakati
mwenge ukipita katika miradi mbalimbali wilayani Manyoni huku akiusemea
mradi wa ushonaji nguo na wa ufugaji nyuki kibiashara kuwa ni ishara ya
uwepo wa viwanda vidogo, vya kati na hata vikubwa siku za baadaye
wilayani humo.
“Nitumie fursa hii kuwaomba
maafisa wa maendeleo ya jamii, wahakikishe vikundi vya wanawake na
vijana wanapatiwa mikopo kutoka asilimia tano ya mapato ya ndani ya
halmashauiri ili viweze kupata nguvu ya kuanzisha viwanda vidogo.
Msiishie hapo, wapeni na mafunzo mbalimbali ya ufugaji nyuki, kuku na
mifugo kibiashara”, amesema Amour na kuongeza;
“Na hawa akina mama waliojiunga kwenye kikundi cha ushonaji, wapewe mafunzo ya kuboresha shughuli zao ziweze kwenda na wakati”.
Mwenge wa uhuru leo umepokelewa
mkoani Singida ukitokea Mkoani Dodoma kupitia kijiji cha Sanza wilayani
Manyoni, mwenge wa uhuru unakimbizwa mkoani Singida katika halmashauri
saba, unakimbizwa kilomita 1064, unatembelea, kuzindua na kufungua jumla
ya miradi 45 yenye thamani ya shilingi bilioni 21.9.
SHARE
No comments:
Post a Comment