Na: Mwandishi Wetu-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, anatarajiwa kufungua Maonesho ya
41 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sababsaba
Julai Mosi mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa kwa Vyombo
vya Habari iliyotolewa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Charles Mwijage, Rais atafanya ufunguzi huo katika Uwanja wa Maonesho wa
Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa Jijini Dar es Slaam.
Waziri Mwijage ameeleza katika
taarifa hiyo kuwa lengo la maonesho ni kutoa fursa kwa wafanyabiashara
wa ndani na nje ya nchi, pamoja na taasisi mbalimbali kutangaza biashara
na huduma, kutoa fursa kwa wafanyabisashara wa ndani kujifunza mambo ya
biashara na uzalishaji bora wa bidhaa kulingana na soko la kimataifa,
kutengeneza mitandao ya mawasiliano baina yao ambayo itasaidia kukuza
biashara na kufikia malengo waliyojiwekeka na pia kutoa fursa ya kuuza
bidhaa.
“Maonesho haya yanabeba kauli mbiu isemayo Ukuzaji wa Biasha kwa Maendeleo ya Viwanda,
inanalenga kutumia Maonesho haya kama jukwaa la kutangaza biashara na
huduma mbalimbali kwa ajili ya ukuzaji wa sekta ya viwanda, ikizingatiwa
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaweka mkazo mkubwa katika kuendeleza
uchumi wa viwada hapa nchini”, anaeleza taarifa ya Waziri.
Aidha Maonesho ya mwaka huu
yatatoa fursa kwa wenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kukutana na
wanunuzi wa bidhaa zao na kutakuwa na kampeni maalum ya kuhamasisha
wananchi kupenda na kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
“Napenda kuwafahamisha kuwa Tan
Trade kwa kushirikiana na washirika wake kwa mara ya kwanza imeandaa
Siku ya ‘Afrika Mashariki’ ambayo itaadhimishwa tarehe 6 Julai, 2017.
Lengo la siku hii ni kuimarisha biashara katika nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Kama inavyojulikana nchi hizi zimejaliwa kuwa na
rasilimali nyingi hali ambayo itatoa fursa nzuri katika maendeleo ya
kiuchumi katika nchi hizo ili kuwe na uchumi endelevu”, ilieleza taarifa
hiyo.
Katika maonesho hayo, Waziri
anaeleza kuwa Tan Trade imeandaa eneo maalum litakalojulikana kwa jina
la ‘Banda la Tanzania’ kwa ajili ya wazalishaji wa bidhaa mbalimbali
zinazotengenzezwa ndani ya nchi na ‘Banda la Asali’ kwa ajili ya kukuza
bidhaa za nyuki na pia kutakuwa na eneo maalum la wazalishaji wa bidhaa
za ngozi ambalo washiriki wake watapata fursa ya kuonesha bidhaa bora za
ngozi kwa ajili ya kuvutia wananchi wengi kupenda bidhaa zinazozalishwa
hapa nchini.
Katika kuimarisha huhusiano wa
kibishara na kuwakutanisha wafanyabiashara wa Kitanzania na wenzao
kutoka nje ya nchi, kutakuwa na banda maalum kwa ajili ya mikutano ya
kibiashara yaani Business to Business (B2B) na pia banda maalum
litakalotumika kwa utoaji wa mafunzo ya kibiashara.
Hadi sasa washiriki zaidi ya 2500
kutoka ndani na nje ya Afrika wamethibitisha kushiriki Maonesho ya
mwaka huu. Nchi zitakazoshiriki ni Burundi, China, Comoro, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Misri, Ujerumani, Ghana, India, Indonesia,
Iran, Italia, Japan, Kenya, Malawi na Mauritius.
Nchi zingine ni pamoja na
Morocco, Msumbiji, Namibia, Pakistani, Rwanda, Singapore, Afrika Kusini,
Sudani Kusini, Syria, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Uganda,
Marekani, Uingereza na Vietnam.
SHARE
No comments:
Post a Comment