
Mratibu wa Uanzishwaji wa Mfuko wa
Ubunifu Vijijini, Bw. Albert Ngusaru akizungumza kabla ya ufunguzi wa
mkutano wa siku moja wa kujadili namna bora ya kuendeleza Mfuko huo.

Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa TADB, Bw. Adam Kamanda (kushoto) akifungua mkutano wa siku
moja wa kujadili namna bora ya kuendeleza Mfuko wa Ubunifu Vijijini huo.

Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Adam Kamanda akieleza lengo la uanzishwaji wa Mfuko wa Ubunifu Vijijini.

Mshauri wa Kiufundi wa MIVARF, Bw. Ravi Malik akiwasilisha dhana ya uanzishwaji wa Mfuko wa Ubunifu Vijijini.

Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa TADB, Bw. Adam Kamanda (kushoto) akizungumza na Mratibu wa
Uanzishwaji wa Mfuko wa Ubunifu Vijijini, Bw. Albert Ngusaru (kulia).

Mwezeshaji wa Majadiliano ya
Uanzishwaji wa Mfuko wa Ubunifu Vijijini, Bw. Severin Ndaskoi (kushoto)
akihimiza jambo wakati wa majadiliano hayo. Kulia ni Meneja wa Hazina na
Ukwasi wa TADB, Bibi Beatrice Mrema.

Washiriki wa Mkutano wa Majadiliano ya Uanzishwaji wa Mfuko wa Ubunifu Vijijini wakifuatilia kwa umakini mkutano huo.
……………………………..
Na Mwandishi wetu,
Wadau kutoka sekta za kilimo na
uchumi wamekutana kujadiliana namna bora ya uanzishwaji wa Mfuko wa
Ubunifu Vijijini (rural innovation fund) wenye lengo la kuchochea,
kuhamasisha na kusaidia uvumbuvi katika maeneo ya maendeleo vijijini,
ukopeshaji wa shughuli za kilimo na huduma za taasisi ndogo za kifedha.
Mkutano huo wa siku moja
umeandaliwa kwa ushirikiano wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania
(TADB) na Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na
Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa
mkutano huo, Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Adam
Kamanda amesema wadau wana mchango mkubwa wa kutoa maoni yatakayosaidia
kuboresha usimamizi wa Mfuko huo ambao utakuwa chini ya TADB.
“Nawaomba tujadili namna bora
itakayosaidia ndoto ya Serikali ya kuchagiza upatikanaji wa fedha za
gharama nafuu kwa ajili ya kuwasaidia wakulima hasa katika maeneo ya
maendeleo vijijini, ukopeshaji wa shughuli za kilimo na huduma za
taasisi ndogo za kifedha,” alisema.
Bw. Kamanda ameongeza kuwa
uanzishwaji wa mfuko huu unalenga kutekeleza kwa vitendo dhamira ya
Serikali ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo ambayo ni
shughuli kuu kwa Watanzania wengi wanaoishi maeneo ya vijijini.
“Uanzishwaji wa Mfuko huu
utasaidia bado ukuaji wa sekta ya maendeleo vijijini ambayo imekuwa
ukikabiliwa na changamoto mbali mbali kama vile kiwango kidogo cha
uzalishaji; ukosefu wa mbinu na teknolojia za kisasa; matumizi madogo
ya umwagiliaji; ukosefu wa mtaji na upatikanaji wa mikopo kwa wakulima,”
aliongeza.
Kwa upande wake Mshauri wa
Kiufundi wa MIVARF, Bw. Ravi Malik alisema kuanza kazi kwa Mfuko huu
kutasaidia changamoto za ukosefu wa masoko ya mazao, miundo mbinu mibovu
ya usafirishaji, nishati ya umeme na miundombinu hafifu vijijini hali
itakayochochea ongezeko la thamani kwa mazao ya kilimo maeneo ya
vijijini.
Bw. Malik aliongeza kuwa Mfuko huo
utawezeshwa kwa kupatiwa mtaji wa Fedha za Kimarekani (USD) zipatazo
Milioni 5 ambazo zitatolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania kwa
ushirikiano na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).
“Fedha hizi zimelenga kukuza
ongezeko la upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi waishio
vijijini kupitia njia mbalimbali za utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja na
huduma za mitandao ya simu ambazo zimekuwa kiungo muhimu katika kuongeza
ushirikishwaji wa kifedha kwa watu wasiotumia huduma za kibenki,”
aliongeza.
SHARE
No comments:
Post a Comment