WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa chakula kwenda
nje ya nchi kuanzia leo. “Kuanzia leo, ni marufuku kwa mtu yoyote
kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali. Serikali
inahamasisha uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda nchini. Kama tutatoa
vibali, ni lazima mtu alazimike kusaga nafaka ili kutoa ajira nchini,”
amesema.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 26, 2017) wakati akitoa
nasaha kwenye Baraza la Eid lililofanyika kitaifa kwenye msikiti wa
Masjid Riadha, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuswali
sala ya Eid.
“Jana
nimeona kwenye televisheni taarifa kuhusu malori 10 yaliyokamatwa
Tarakea yakiwa na mahindi tayari kuvushwa mpaka. Mheshimiwa RC akasema
chakula hicho ni lazima yarudishwe kwa ajili ya usagaji.”
“Mimi
nasema kuanzia leo, yeyote atakayekamatwa akitorosha chakula kwenda nje
ya nchi, chakula hicho kitataifishwa na kupelekwa ghala la Taifa na
gari lake tutalitaifisha na litaishia Jeshi la Polisi. Tunafanya hayo
kwa lengo la kuwalinda Watanzania tusikumbwe na baa la njaa.”
Akitoa
tahadhari kuhusu uuzwaji wa chakula nje ya nchi, Waziri Mkuu amesema
kumekuwa na wimbi kubwa la usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi
bila kibali. “Hilo ni kosa kubwa kwa sababu litasababisha nchi yetu
kupata baa la njaa huko mbele,” amesema.
Amesema
mipaka ya Tarakea, Holili, Mwanga, Horohoro, Siha, Namanga na Sirari
imekuwa inapitisha kiasi kikubwa cha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi
jambo ambalo ni hatari sana. “Hii ni kwa sababu chakula cha ndani
hakitoshelezi mahitaji. Kwa sababu nchi zote za jirani hazina chakula
cha kutosha. Tusipokuwa makini, tutabaki tunalia njaa.”
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wafanyabiashara wa ndani, wachukue
mahindi kutoka maeneo yenye mavuno mengi na kuyapeleka kwenye sehemu
zenye mavuno kidogo. “Watanzania tushirikiane, kama ni biashara tutoe
huku kwenye mavuno mengi na tuyapeleke Shinyanga na Geita ambako
wanayahitaji au tukanunue Sumbawanga na kuyapeleka kwenye mikoa mingine
yenye upungufu,” alisisitiza.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa dini waisadie
Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kupitia kwenye
nyumba za ibada. “Naomba tuendelee kushirikiana kupambana na janga hili
la dawa za kulevya kwa ustawi wa nchi yetu. Naamini viongozi wa dini
mnayo nafasi kubwa katika mapambano haya, kwa kuwafunda vijana wetu
kuishi katika maadili ya kidini na kutojiingiza kwenye janga hilo.”
Alisema
Serikali kwa upande wake itaendeleza mapambano hayo bila ajizi wala
mzaha. “Tunaomba wananchi wote watuunge mkono kwa kutoa taarifa sahihi
za wanaojihusisha na uzalishaji, utengenezaji, usambazaji na utumiaji wa
dawa za kulevya pindi tu wanapowabaini.”
Wakati
huo huo, akitoa tafsiri ya Qur’aan tukufu kwenye Baraza la Eid, Sheikh
wa Mkoa wa Arusha, Sheikh Shaaban Juma alisema kila nguzo katika Uislamu
inapaswa kufuatwa na kwamba mtu akiharibu nguzo moja tu anakuwa
ameharibu nguzo zote tano.
Alisema
siku ya kiyama, watatokea watu wenye thawabu kama milima ya Usambara
ama Upareni na akawataka Waislamu wote nchini wadumu katika kutenda mema
ili wapate thawabu.
Mapema,
akitoa khutba katika swala ya Eid el Fitr iliyoswaliwa kwenye msikiti
huohuo wa Masjid Riadha, Sheikh Mlewa Shaban alisema sikukuu ya Eid ni
siku ya kujiepusha na madhambi kama ulevi, kamari na lugha chafu, bali
aliwataka waumini wote waitumie siku hiyo kuwapa furaha maskini, yatima
na wajane.
“Mtu
asiseme mwezi wa Ramadhan umepita, sasa narudia mambo yangu ya zamani.
Adhabu za Mwenyezi Mungu hazina mipaka na wale waliotulizana watapata
thawabu yao, kumbukeni neema na Mwenyezi Mungu na mcheni Mwenyezi
Mungu.”
“Kitu
tunachopaswa kufanya kila wakati ni kumcha Mwenyezi Mungu. Lazima
tupendane, tuondoe tofauti zetu na tuujenge Uislam. Hatuwezi kuujenga
uislam kama hatupendani. Lazima tuilinde ibada yetu kwa sababu hatuna
garantii, ni lini tutaondoka,” alisema.
Sherehe
hizo zilihudhuriwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar
Zubeir bin Ally; Wajumbe wa Baraza la Ulamaa, Waziri wa Maliasili na
Utalii, Prof. Jumanne Maghembe; Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna
Mghwira; IGP Mstaafu, Bw. Said Mwema; Mbunge wa Moshi Mjini, Bw. Jaffary
Michael; Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo na viongozi mbalimbali wa dini na
Serikali.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akitoa nasaha kwa waumini (hawapo pichani)
waliohudhuria Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa kwenye
msikiti wa Masjid Riadha mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni,
2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waumini
wa dini ya Kiislamu waliohudhuria Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid
Kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro
wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa nasaha za Eid,
tarehe 26 Juni, 2017.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akiteta jambo na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania,
Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally wakati wa stafutahi kwenye Ikulu ndogo
ya Moshi, mara baada ya Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa
mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akiagana na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania,
Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally mara baada ya stafutahi kwenye Ikulu
ndogo ya Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akisaini kitabu cha maombolezo, nyumbani kwa
marehemu Dk. Philemon Ndesamburo, eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani
Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akitoa pole na neno la faraja kwa wanafamilia,
nyumbani kwa marehemu Dk. Philemon Ndesamburo, eneo la Kiboriloni,
Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akimpa pole mjane wa marehemu, mama Ndehorio P.
Ndesamburo alipofika nyumbani kwao eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani
Kilimanjaro kuwafariji kutokana na msiba wa Dk. Philemon Ndesamburo, leo
tarehe 26 Juni, 2017.
Kaka
wa marerehemu Dk. Philemon Ndesamburo, Bw. Zablon Sindato Kihwelu
akimshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyefika nyumbani kwao eneo la
Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro kuwafariji kutokana na msiba wa
Dk. Philemon Ndesamburo, leo tarehe 26 Juni, 2017.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bibi Anna Mgwira (wa
tatu kushoto), mjane wa marehemu na Kaka wa marehemu wakiomba dua na
wanafamilia kwenye kaburi la Dk. Philemon Ndesamburo, aliyezikwa
nyumbani kwake eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro. Wa kwanza
kulia ni mtoto wa marehemu.
SHARE
No comments:
Post a Comment