
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa
Kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd anayejenga barabara ya Uyovu-Bwanga
KM 45 kwa kiwango cha lami, mkoani Geita.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akizungumza na waandishi wa habari mara
baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya
Bwanga-Biharamulo yenye urefu wa KM 67, mkoani Geita.

Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS), Mkoa wa Geita Eng. Harun Senkuku akifafanua jambo kwa Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, kuhusu
maendeleo yaliyofikiwa ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga
yenye urefu wa KM 45, mkoani Geita.
………………………………………………………………………………..
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema mradi wa ujenzi wa barabara ya
Uyovu-Bwanga-Biharamulo yenye urefu wa KM 112 inayojengwa na mkandarasi
wa Kampuni ya Synohydro Corporation itakamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Prof. Mbarawa amezungumza hayo
mkoani Kagera, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na
kumtaka mkandarasi aongeze kasi ili barabara hiyo iweze kukamilika kwa
wakati.
“Hakikisheni mnaongeza kasi ya ujenzi ili muweze kukamilisha ujenzi huu kwa wakati iwezekanavyo”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amemsisitiza mkandarasi
kuzingatia viwango vilivyopo katika mkataba kwani mwisho wa siku lazima
watanzania wapate barabara inayokidhi mahitaji yao na ubora wake.
Amewapongeza wasimamizi wa
barabara hiyo ambao ni kutoka kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS)
kupitia kitengo chake maalum cha wahandisi washauri wazawa (TECU), kwa
kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi M/S Sinohydro Corporation kwa
ukaribu.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala
wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Geita Eng. Harun Senkuku
amemueleza Waziri Prof. Mbarawa kuwa changamoto ya fidia iliyokuwa
inawakabili sasa imemalizika na kiasi cha shilingi milioni 700
zimetumika kukamilisha ulipaji fidia kwa wakazi wote.
Amemhakikishia Waziri kuwa
TANROADS itaendelea kumsimamia mkandarasi huyo ili kuhakikisha thamani
halisi ya fedha ya Serikali inapatikana.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya
Uyovu-Bwanga-Biharamulo KM 112 umehusisha ujenzi wa barabara ya
Uyovu-Bwanga yenye urefu wa KM 45 na barabara ya Bwanga-Biharamulo yenye
urefu wa KM 67.
SHARE








No comments:
Post a Comment