Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka akizungumza katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi
kati ya uongozi wa Mkoa huo, wataalam wa kilimo, mifugo na ushirika na
Uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Francis Assenga akizungumza
na Uongozi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na wataalam wa Kilimo, ushirika na
Mifugo (hawapo pichani) Mjini Bariadi.
Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo,
Augustino Matutu Chacha wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB),
akizungumza na Uongozi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na wataalam wa Kilimo,
ushirika na Mifugo (hawapo pichani) Mjini Bariadi.
Mkuu wa Idara ya kilimo wa
Halmashauri ya Wilaya ya Busega Juma Chacha akichangia katika kikao
kilichofanyika katika uongozi wa Mkoa wa Mkoa wa Simiyu na Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) Mjini Bariadi.
Mkuu wa Idara ya Kilimo wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Wilbert Siogopi akichangia katika
kikao kilichofanyika kati ya Uongozi wa Mkoa wa Mkoa wa Simiyu na Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wataalam na Wanahabari
wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika kikao
kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Baadhi ya Wataalam na Wanahabari
wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika kikao
kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB).
………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu, Simiyu
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) imeuhakikishia uongozi wa Mkoa wa Simiyu kuwa itafanya
kazi kwa karibu katika kutoa fursa ya mikopo itakayowasaidia wakulima
mkoani humo kulima kilimo chenye tija.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Anthony Mtaka pamoja na Wakurugenzi na Wataalam kilimo na
umwagiliaji, ushirika na mifugo kutoka Halmashauri zote za Simiyu,Kaimu
Mkurugenzi wa Banki hiyo Francis Assenga amesema wapo tayari kukopesha
na kufanya kazi na Mkoa wa Simiyu kutokana na utayari wao na uwepo wa
mwongozo elekezi wa shughuli za kilimo zilizofanyiwa utafiti.
Amesema Benki hiyo ambayo ina
lengo la kuleta mapinduzi ya kilimo Tanzania imeridhia kutoa mikopo
katika miradi ya kilimo kwa wakulima, vikundi vilivyosajiliwa, vyama vya
ushirika na kupitia Benki na taasisi nyingine za kifedha ambazo
zinaweza kuwakopesha wakulima, ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini
kwa wakulima mkoani humo.
Ameongeza kuwa ili kufanikisha
azma ya Mkoa wa Simiyu ya kukifanya kilimo kuwa ni biashara na kukuza
uchumi wa wakulima wake , Benki ya TADB itasaidia kutoa mikopo
itakayoambatana na mafunzo ya kuwajengea uwezo wakopaji hususani
wanawake na vijana.
Ameeleza kuwa benki yake
imekwisha tenga kiasi cha shilingi milioni 650 kwa ajili ya mafunzo ya
kuwajengea uwezo na Bil 42 za mkopo kwa wanawake na vijana, hivyo
amezisisitiza Halmashauri za Mkoa wa Simiyu kuwahamasisha vikundi vya
wakulima vilivyosajiliwa kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo yenye riba
ndogo na masharti nafuu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe.
Anthony Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu uko tayari kufanya kazi na Benki ya
TADB kupitia vikundi vya uzalishaji, Halmashauri na Miradi mbalimbali
inayotekelezwa mkoani humo, ikiwa ni pamoja na miradi ya umwagiliaji ya
Mwamanyili Wilayani Busega ulio katika hatua ya upembuzi yakinifu na
Mwasubuya wilayani Bariadi ambao uko katika hatua ya ujenzi wa
miundombinu ya umwagiliaji.
“Tungehitaji kuwa Mkoa ambao
kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo tungetengeneza namna ambayo
ingewasaidia wakulima na ikasaidia mikoa mingine kuja kuona maendeleo ya
kilimo ambayo ni matokeo ya Serikali kuwekeza katika Benki ya Kilimo”
amesema Mtaka.
“Sisi kama Mkoa tumejipanga, tumetoa Elimu ya utayari na
namna ya utekelezaji wa shughuli zote kwa wataalam wetu pamoja na wananchi na isitoshe
tayari tumeshafanya utafiti na kuandaa mwongozo wa uwekezaji ndani ya
mkoa, hivyo tunawakaribisha kuwekeza,” Amesema Mtaka.
Aidha Mtaka ameongeza kuwa Mkoa
wa Simiyu unatekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda chini ya Kauli Mbiu ya
“Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja” ambapo hadi sasa kuna kiwanda
cha chaki na maziwa na miradi mingine minne ya viwanda iko katika
upembuzi yakinifu, hivyo benki inaweza kuwekeza katika miradi hii kwa
kuwawezesha wakulima na wafugaji kuzalisha malighafi ya Viwanda hivyo au
kuwa mdau katika viwanda hivyo.
Naye Mkurugenzi wa Biashara na
Mikopo wa TADB Augustino Matutu Chacha amesema wamefurahishwa na
utayari wa Mkoa wa Simiyu juu ya kuwawezesha wakulima na Benki hiyo iko
tayari kutoa mikopo pia kwa wakulima wa zao la pamba ambao wanazalisha
zaidi ya asilimia 60 ya pamba yote nchini ili izalishwe kwa wingi zaidi
na katika ubora wa hali ya juu.
Chacha amesema wataalam wa kilimo
wa Mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na wataalam wa benki ya Maendeleo ya
kilimo Tanzania (TADB) watakutana ili kuona namna watakavyofanya kazi
kwa pamoja ili mikopo itakayotolewa iweze kuwa wa manufaa kwa wakulima
na nchi kwa ujumla.
Aidha amewaeleza Wakurugenzi wa
Halmashauri zote kuwa, Halmashauri zinaweza kupatiwa mikopo ili ziweze
kuendesha miradi ya kilimo itakayoweza kuwa vyanzo vipya vya mapato kwa
Halmashauri zao.
SHARE
No comments:
Post a Comment