Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuweka mikakati endelevu ili kuwezesha kiwanja cha ndege cha Tabora kujisimamia na kujiendesha kutokana na miundombinu bora na ya kisasa inayoendelea kujengwa kiwanjani hapo.
Amezungumza
hayo jana mkoani humo, mara baada ya kuanza ziara ya kikazi ambapo
pamoja na mambo mengine Waziri Prof. Mbarawa amekagua na kujionea
maendeleo ya mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho ambapo mpaka sasa ujenzi
wake umefikia asilimia 96 na umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 27.
“Hivi
sasa huduma ya usafiri wa ndege katika kiwanja hichi unaridhisha, hivyo
ongezeni ubunifu ili kuvutia abiria wengi na kuwezesha kiwanja
kujiendesha”, amesema Prof. Mbarawa.
Amesisitiza
kuwa gharama za usafiri wa anga zitaendelea kupungua kadri huduma na
ubora zitavyokuwa zinaendelea kuongezeka ili kuwezesha abiria wengi
zaidi kutumia usafiri huo na hivyo kuwezesha pato la Taifa kuongezeka.
Kwa
upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mkoani Tabora Eng.
Danstan Komba amemueleza waziri kuwa idadi ya abiria wanaotumia kiwanja
cha ndege hicho imeongezeka kutoka asilimia 10 kwa mwaka 2011 hadi
kufikia asilimia 62.3 mwaka 2016 kutokana na ndege za ATCL kuanza safari
zake mkoani humo.
Aidha,
ameongeza kuwa baada ya mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho kukamilika,
mashirika ya ndege yataongeza safari zake mkoani humo kwa kuzingatia
uwepo wa miundombinu bora yenye kukidhi mahitaji na hivyo itatoa chachu
ya maendeleo kwa wakazi wake na kuboresha shughuli za kiuchumi na
kijamii.
Naye,
Meneja wa Mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho Eng. Neema Joseph,
amemuahidi Waziri Prof. Mbarawa kumsimamia mkandarasi kumalizia kazi
zilizobaki uwanjani hapo ndani ya siku 14 na kwa kuzingatia viwango na
ubora.
Katika
hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amezungumza na viongozi na
wafanyakazi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake na kusisitiza kufanya
kazi kwa kuzingatia uaminifu, weledi, kasi na uzalendo ili kuendeleza
azma ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta maendeleo kwa wananchi
wake na kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025.
Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua miradi ya miundombinu iliyopo mkoani Tabora.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia),
akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Kaya-Ceytun JV Eng. Ifran
Sakrak (kushoto), wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi ya
kiwanja cha ndege cha Tabora, jana.
Muonekano wa Taa za kuongozea ndege wakati wa kutua zilizojengewa katika Kiwanja cha Ndege cha Tabora.
Muonekano
wa Mtambo wa kisasa wa kuongoza ndege unaonesha mwelekeo na umbali wa
zaidi ya Kilomita 200 uliopo katika kiwanja cha ndege cha Tabora.
Meneja
wa Mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Tabora Eng. Neema Joseph,
akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa, kuhusu maendeleo ya ujenzi yaliyofikiwa kiwanjani hapo,
wakati akikagua ujenzi wake, mkoani humo jana.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akitoa
maelekezo kwa Meneja wa Mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Tabora
Eng. Neema Joseph, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi ya kiwanja hicho
uwanjani hapo, jana.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akiwasili na
ndege aina ya Bombadier Q400 ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),
mkoani Tabora katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo jana
SHARE
No comments:
Post a Comment