Mjumbe wa Marekani anawasili Israel kuusawazisha mgogoro
wa eneo tukufu lenye mzozo la Temple Mount mjini Jeruslaem, baada ya
Israel kuimarisha usalama katika eneo hilo na kuwakasirisha Wapalestina.
Mjumbe maalumu wa Rais wa Marekani Donald Trump anawasili nchini
Israel leo hii ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza mvutano
uliotokana na hatua mpya za kiusalama zilizowekwa na Israel katika eneo
tukufu linalozozaniwa kati yao na Palestina katika mji wa Jerusalem.Ziara ya Jason Greenblatt imekuja baada ya zaidi ya wiki moja ya mvutano juu ya uwanja wa Haram al-Sharif, unaojulikana na Wayahudi kama Temple Mount ambao ndiyo kitovu cha mzozo kati ya Israeli na Palestina.
Israel iliweka mtambo wa umeme wa ukaguzi katika mlango wa kuingilia katika eneo hilo, ambamo ndani yako unapatikana pia msikiti wa Al-Aqsa, kufuatia shambulio la Julai 14 lililosababisha vifo vya maafisa wawili wa polisi.
Israel imesema mtambo huo wa ukaguzi unahitajika kama njia ya kuzuia mashambulizi katika siku za baadae. Hata hivyo, serikali ya Israel inakabiliwa na ukosoaji mkali na baadhi ya wakosoaji wanasema kwamba Israel haikufikiria athari za kuanzisha hatua mpya za kiusalama katika eneo lenye utata katika mgogoro mzima kati ya Israel na Palestina.
Wapalestina wanaiangalai hatua hiyo ya kuimarisha ulinzi kama njia ya Israel ya kutaka kuwa na udhibiti zaidi wa eneo hilo. Wapalestina waligoma kuingia ndani na kusali barabarani nje ya uwanja huo.
Netanyahu adai ni hatua ya kudumisha usalama
Waziri Mkuu wa Isarel Benjamin Netanyahu hapo jana alisema kuwa hali hiyo wanaishughulikia na wataendelea kufanya hivyo ili kudumisha usalama katika eneo hilo.
"Tangu yalipoanza matukio haya, nilifanya mfululizo wa mikutano ya kutathmini hali ilivyo na bodi tafautu za usalama, ikiwa ni pamoja na maafisa wa usalama waliopo katika eneo husika.Tunapokea tathmini za hali ilivyo kutoka kwao na namna ya kuiboresha hali hiyo, pamoja na mapendekezo ya hatua sahihi za kuchukua. Tutaendelea kufanya hivyo ili kudumisha usalama, " amesema Benjamin Netanyahu.
Wakati huo huo raia wawili wa Jordan wameuwawa kwa kupigwa risasi karibu na ubalozi wa Isarael wa mjini Amman nchini Jordan, kulingana na taarifa za shirika la habari la Jordan la Petra.
Risasi zilianza kufyatuliwa jana Jumapili katika jengo mmoja liliopo karibu na ubalozi huo na kumjeruhi pia mlinzi wa Kiisrael. Sababu za shambulio hilo bado hazijulikani.
Ijumaa iliyopita raia wa Jordan walifanya maanadamano makubwa mjini Amman na maeneo mingine ya nchi, dhidi ya Israel na hatua yake ya kuimarisha usalama katika msikiti wa al-Aqsa mjini Jerusalem, likiwa ni eneo la tatu kwa utukufu kwa waumini wa dini ya Kiislam.
SHARE
No comments:
Post a Comment