HARARE, ZIMBABWE
RAIS wa Zimbabwe, Robert Mugabe (93), amekimbizwa tena Singapore kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa Gazeti la Sunday Mail, Rais Mugabe aliondoka nchini hapa Ijumaa kwenda nchini humo kwa ajili ya matibabu ya kawaida. Inaelezwa kuwa atarejea Zimbabwe katikati ya wiki hii.
Siku za hivi karibuni Rais huyo amekuwa na safari za mara kwa mara kwenda nchi za Asia kwa ajili ya matibabu huku wapinzani wake wakishinikiza ajiuzulu. Safari yake ya mwisho nje ya nchi kwa ajili ya matibabu ilikuwa Mei mwaka huu.
Itakumbukwa kuwa mwaka 2011 na 2014 alifanyiwa upasuaji wa jicho Singapore. Kwa sasa Rais Mugabe inaelezwa anatembea kwa shida huku akitegemea msaada mkubwa wa wasaidizi wake.
Afya ya Rais huyo ambaye siku za karibuni aliuza ng'ombe wake 300 ili kusaidia Umoja wa Afrika (AU), inadaiwa inazidi kutetereka siku hadi siku.
Mwaka 2016 kulikuwa na taarifa amefariki akiwa nje ya nchi, lakini Serikali ilisema si kweli. Pamoja na afya yake kuwa katika hali hiyo, Rais Mugabe haonekani kuachia madaraka na badala yake inaelezwa atawania tena nafasi ya urais mwakani.
Pamoja na umri wake mkubwa, chama tawala cha ZANU-PF kimempitisha kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.
Viongozi wengine wa Afrika ambao wamekuwa wakitibiwa nje ya nchi siku za hivi karibuni ni pamoja na Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari ambaye amekuwa Uingereza tangu Mei 7 kwa ajili ya matatibu.
Pia yumo Rais wa Angola, Jose Eduardo dos Santos ambaye alitumia takriban mwezi mmoja akiwa Hispania kwa matibabu.
SHARE
No comments:
Post a Comment