Chama
cha ACT Wazalendo kinasikitishwa na mwenendo mbovu wa usimamizi wa zoezi la
ugawaji na usambazaji wa pembejeo za zao la korosho kwa msimu unaoendelea wa
mwaka 2017/18. Ikumbukwe kuwa kwa sasa, zao la korosho ndilo linaloongoza
katika kuliingizia taifa mapato likifuatiwa na tumbaku. Mathalani, Kwa Takwimu
za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) za mwezi Februari mwaka 2017, zao Korosho
lililiingizia Taifa fedha za Kigeni, Dola za Kimarekani milioni 346.6,
ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka 2016, ambapo tulipata Dola za
Kimarekani milioni 184.9. Kuongezeka kwa mapato haya kulichangiwa kwa sehemu
kubwa na ongezeko la uzalishaji na kupaa kwa bei ya korosho kwenye msimu wa
mwaka 2016/207. Mathalani, kwa msimu wa mwaka 2016/2017, uzalishaji wa zao la
korosho nchini ulikuwa tani 260,000 ukilinganisha na tani 155,416 za mwaka
2015/2016 sawa na ongezeko la zaidi ya tani 100000. Kwa upande wa bei, Kikao
cha Wadau wa Bodi ya Korosho kilichoketi Bagamoyo mwezi Agosti 2016 kilipanga
bei elekezi ya Tsh. 1300 kwa kilo. Lakini, bei halisi ilipaa hadi kufikia Tsh.
4000 kwenye baadhi ya maeneo hapa nchini.
Sababu
kuu ya kupaa kwa bei ya korosho nchini ni kuongezeka kwa wazabuni wapya mbali
na wanunuzi wa jadi kutoka nchini India. Kwa mfano, nchini Vietnam (inayozalisha
58% ya korosho zote duniani), uzalishaji ulipungua kwa asilimia 11 mwaka jana
kutokana na ukame, huku mahitaji yake yakiongezeka kwa asilimia 53 tangu 2010. Hivyo
haikushangaza kwa mara ya kwanza katika historia ya soko la korosho nchini,
kushuhudia ushiriki mkubwa wa wazabuni kutoka nchi za Vietnam, China na
Singapore na Vietnam.
HALI HALISI YA UPATIKANAJI WA PEMBEJEO KWA HIVI
SASA
Mwezi
Mei mwaka huu, kwenye kikao cha mwaka cha wadau wa zao la korosho
kilichofanyika mjini Dodoma, Serikali ilitangaza uamuzi wa kugawa pembejeo bure
kwa wakulima wote wa zao la korosho. Uamuzi huo ulitangazwa na waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, ndugu Charles Tizeba mbele ya Waziri Mkuu, ambaye alikuwa
mgeni rasmi kwenye mkutano huo. Kutangazwa kwa uamuzi huu kuliibua shangwe
kubwa kwa wakulima wa korosho ambao walifurahia kupunguziwa mzigo wa kununua
pembejeo.
Uamuzi
huu ulileta matokeo yafuatayo:
- Mfumo wa Pembejeo ya ruzuku ulifutwa.
Kabla
ya mfumo wa kugawa pembejeo bure kutangazwa, kulikuwa na mfumo wa pembejeo
uliokuwa ukiendeshwa na Vyama vya Msingi vya ushirika (Amcos). Vyama hivi vya
msingi vya ushirika vilikuwa vinakusanya fedha kwa wakulima wakati wa mauzo (kiasi
cha shilingi 15,000 tu kwa mfuko), kununua pembejeo nje ya nchi na kugawa kwa
wakulima.
- AMCOS Walirudisha Fedha za Wakulima
Kabla
ya kutangazwa kwa uamuzi huu, vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) vilikuwa
vimeshakusanya fedha kwa wakulima na vinajipanga kununua Salfa nje ya nchi. Kwa
uamuzi huu wa serikali, vyama vya ushirika viliamriwa kuwarudishia wakulima
fedha zilizokusanywa kwa sababu “Pembejeo ya bure” ingeletwa.
- Wakulima Walizitumia Fedha Zilizorejeshwa Kutoka Amcos
Baada
ya wakulima kurejeshewa fedha zao kutoka kwa vyama vyao vya msingi vya ushirika
(Amcos), wengi wao walizitumia fedha hizo kwa matumizi mengine kwa kuwa
walikuwa na uhakika wa kupata pembejeo ya bure kutoka serikalini.
- Waagizaji Binafsi “Waliufyata”
Mbali
na vyama vya ushirika, pembejeo huuzwa pia kwenye soko na wafanyabiashara
binafsi. Kwa msimu wa mwaka 2016/2017, pembejeo aina ya Salfa, ambayo ndiyo
maarufu zaidi, iliuzwa kati ya shilingi 3000 - 35,000 kwa mfuko mmoja, na
wauzaji binafsi. Kutangazwa kwa ujio wa Salfa ya bure kuliwafanya wafanyabiashara
wengi binafsi kukhofia kukosa soko la Salfa na pembejeo nyingine muhimu walizoagiza
na hivyo kupata hasara.
Kinyume
na ahadi ya serikali ya kuleta pembejeo ya bure, ya kutosha na kwa wakati, hali
imekuwa tofauti mno. Matatizo makubwa yametokea kama ifuatavyo;
- Pembejeo Hazikuletwa kwa Wakati
Mfano,
Juni 22, 2017 wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara, mbele ya mkuu wa wilaya
ya Nachingwea, Rukia Muwango, uliofanyika katika kijiji cha Mpiruka A, mkutano
ambao viongozi wa ACT Wazalendo walihudhuria, wakulima hawa walionyesha
kukatishwa tamaa na uchelewehwaji wa pembejeo, na matumaini yao ya uzalishaji
mkubwa kama msimu uliopita yameanza kufifia kabisa.
- Pembejeo Zilizoletwa ni Kidogo Mno.
Hata
baada ya pembejeo hizo kuletwa, mwezi huu (Julai) mwanzoni, bado kasma
iliyopelekwa haikidhi haja na mahitaji yaliyopo, maana ni ndogo mno. Kwa mfano,
Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma, yenye mahitaji ya tani 5,000 za Salfa kwa
msimu huu wa uzalishaji, imepewa mgao wa tani 1000 tu za Salfa, ambayo ni 20%
ya mahitaji yote.
Mfano
mwengine ni Wilaya ya Nachingwea ambayo mahitaji halisi ya dawa ya Salfa ya unga
ni tani 20,000. Hata hivyo mgao ulitolewa na bodi ya korosho ni tani 1300 tu,
ikiwa ni 6.5% ya mahitaji ya wilaya nzima.
Hii
imesababisha wakulima wengi kutopata kabisa Salfa, na hivyo kuwaacha bila
pembejeo kwa mikorosho yao. Hata kwa waliopatiwa Salfa, wengi wao wamepata
wastani wa mfuko mmoja unaotosha kupulizia hekari moja tuu yenye mikorosho 30
tu. Hii ni kinyume na ahadi ya serikali kugawa Salfa, na hivyo hata kwa mkulima
mdogo tu mwenye hekari chache kutopata pembejeo za kutosha. Kinyume na ahadi ya
Serikali ya kutoa bure pembejeo za kutosha.
- Pembejeo Zilizoletwa Kutokuwa na Ubora
Yapo
madai kutoka katika wilaya za mikoa yote mitano ambazo Viongozi na Watafiti wa
ACT Wazalendo walizungumza na wananchi, wakulima pamoja na viongozi wa vyama
vya msingi vya ushirika (Amcos) kuwa Salfa husika iliyosambazwa, pamoja na
kutofikishwa kwa wakati na kuwa kidogo mno, bado ina ubora duni kwa sababu ya
kujaa chengachenga zinazopunguza ufanisi wakati wa kupulizia.
- Bei ya Pembejeo imepanda maradufu
Baada
ya kugundua kuwa serikali imefeli kutekeleza ahadi yake ya kugawa Salfa yenye
ubora bure, kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa, wakulima wameamua
kupambana binafsi ili kunusuru mikorosho yao, mustakabali wao na kujiepusha na
kuzama kwenye ufukara, kwa kila mmoja kwa nafasi yao kujaribu kununua Salfa
kutoka kwa wafanyabiashara binafsi. Kwa wafanyabiashara binafsi, jambo hili
limegeuka fursa kwao, baada ya kugundua kuwa Serikali imefeli katika kutimiza
ahadi yake wafanyabiashara hawa wametumia fursa hiyo kujitajirisha, kwanza kwa
sababu ya uhaba wa Salfa, pili kwa kuwa wanajua wakulima hawana njia mbadala ya
kupata Salfa tofauti na kwao wao.
Bei
ya Salfa inapanda kila uchwao kwa kasi ya roketi. Kwa mfano, kwa Wilaya ya
Tunduru, kwa kipindi cha mwezi mmoja tu wa Julai, bei ya mfuko mmoja wa Salfa
imepaa kutoka 35,000 hadi 8,0000. Kiwango hicho cha bei juu ya Salfa hakijawahi
kushuhudiwa tangu kilimo cha korosho kianze nchini, uzembe wa Serikali
unawaletea mateso wananchi.
Wakulima wachache wenye akiba ya fedha wanatumia
akiba yao ambayo wangeitumia kwenye shughuli za maendeleo kununulia Salfa kwa
matumaini hafifu kuwa “Dhahabu ya Kusini” itawalipa. Wengi wanayatazama
mashamba yao waliyoyapalilia kwa uchungu kwa sababu hawana namna ya kufanya.
Furaha yao ya awali ya kupata Salfa ya bure imegeuka kilio kikuu.
Jedwali lifuatalo linaonesha bei za Salfa katika
baadhi ya Wilaya zinazozalisha zao la korosho zaidi nchini.
Eneo
|
Bei
ya Salfa (Amcos)
|
Bei
ya asili ya Wafanyabiashara
|
Bei
ya sasa ya Wafanyabiashara
|
|
Nachingwea
|
|
30,000
|
80,000
|
|
Kilwa
|
15,000
|
35,000
|
Pembejeo
ya Salfa haipatikani kabisa kwa sasa
|
|
Liwale
|
15,000
|
35,000
|
53,000
|
|
Tandahimba
|
15,000
|
35,000
|
55,000
|
|
Masasi
|
15,000
|
30,000
|
90,000
|
|
Newala
|
15,000
|
30,000
|
70,000
– 80,000
|
|
Tunduru
|
15,000
|
35,000
|
70000-80000
|
|
Mtwara
Mjini
|
15,000
|
30,000
|
50,000
|
|
Mtwara
Vijini
|
15,000
|
35,000
|
55,000
|
|
Ruangwa
|
15,000
|
35,000
|
60,000
– 80,000
|
|
Lindi
Mjini
|
15,000
|
35,000
|
60,000
– 80,000
|
|
Lindi
Vijijini
|
15,000
|
35,000
|
60,000
– 100,000
|
|
Nanyumbu
|
15,000
|
35,000
|
90,000
|
|
Ndanda
|
15,000
|
35,000
|
90,000
|
|
Rufiji
|
15,000
|
35,000
|
70,000
|
|
Mkinga
|
15,000
|
35,000
|
70,000
|
|
Mkuranga
|
15,000
|
35,000
|
70,000
|
|
Kisarawe
|
15,000
|
35,000
|
70,000
|
|
Nanyamba
|
15,000
|
35,000
|
90,000
|
Tujiulize
maswali haya:
- Je Serikali Ilikuwa na hakika au ilikuwa inafanya mzaha na siasa tu kwa ahadi yake hewa ya pembejeo za bure inayogharimu maisha ya wakulima?
- Je Serikali Ilifanya uchambuzi wa kina kuhusu mahitaji halisi ya pembejeo ya wakulima wa korosho nchini, na uwezo wa Serikali au ilikurupuka tu?
- Waziri Mkuu, Waziri wa kilimo na Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho walipohakikishia wakulima kuwa pembejeo itapatikana kwa wingi, walimaanisha hii hii iliyokuja kwa kuchelewa, isiyo na ubora na iliyogawiwa kwa uchache au kuna nyingine inakuja?
- Serikali ilipovunja mfumo wa pembejeo ya ruzuku chini ya vyama vya msingi vya ushirika vya walikuwa na nia njema na wakulima?
Ni
dhahiri kuwa Serikali hii imeshindwa kuwajali wakulima hawa, ni dhahiri kuwa
kuwa Serikali imeshindwa kuendesha uchumi wa nchi hii.
MAPENDEKEZO YA ACT WAZALENDO
Chama
cha ACT Wazalendo kinatoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka
kurekebisha mambo, ikiwemo:
HATUA ZA DHARURA:
- Serikali ifanye haraka kutimiza ahadi yake ya kufikisha pembejeo ya bure kwa wakulima wa korosho, kwa kuhakikisha inafikisha kiwango cha pembejeo kinacholingana na mahitaji yaliyoko. Taarifa juu ya mahitaji ya wakulima ziko Serikalini, ni muhimu serikali ipeleke pembejeo kulingana na mahitaji. Serikali ichukue hatua za dharura kuagiza pembejeo kuondosha uhaba wake.
- Serikali inunue pembejeo zote kutoka kwa wafanyabiashara binafsi, na kuigawa bure kwa wananchi kama ilivyoahidi wakati, au itoe ruzuku kuhakikisha kuwa wakulima watanunua kwa bei ya Amcos ya 15,000 au bei ya soko isiyozidi 35000 kwa mfuko mmoja.
- Serikali ichukue hatua kali dhidi ya wauzaji wa pembejeo wanaopandisha bei ya pembejeo kila siku bila huruma. Ongezeko la sasa la hadi kufikia Tsh. 800,000 kwenye maeneo kadhaa kwa mfuko mmoja wa Salfa halina utetezi wowote wa kibiashara zaidi ya uchu wa kutumia uhaba wa pembejeo uliosababishwa na uzembe wa serikali kujitajirisha.
- Serikali ichunguze ubora wa Salfa inayogawiwa ambayo inalalamikiwa na wakulima kuwa na ubora duni.
- Serikali ichukue hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wanaolalamikiwa kuchanganya unga wa nafaka kwenye sulphur ili kujipatia faida maradufu.
HATUA ZA MUDA WA KATI:
- Serikali ifanye uchambuzi wa kina wa mahitaji halisi ya kila mkulima na kuwa na uhakika wa bejeti yake ndipo itangaze na kutekeleza mfumo wa Salfa ya bure. Isikurupuke tu kwa lengo la kutaka sifa.
- Serikali itoe taarifa za uhakika mapema kuhusu upatikanaji wa pembejeo badala ya kutoa taarifa za hadaa. Kwa miaka mingi wananchi wamekuwa wakijinunulia pembejeo wenyewe. Ni bora serikali ieleze wazi juu ya uwezo wake ili wakulima waweze kujiandaa mapema kwa kujiwekea akiba kwa ajili ya kununua pembejeo.
- Iwapo serikali serikali itakuwa haina uwezo wa kugawa Salfa yote bure, kama ilivyoonekana, ieleze kwa undani kiwango inachoweza kutoa bure, na iimarishe mfumo wa pembejeo kupitia Amcos kama ilivyokuwa kawaida.
HATUA ZA MUDA MREFU:
- Kufungamanisha sekta ya korosho na hifadhi ya jamii ili kupitia fao la bei kuweza kuweka uimara wa bei za mazao na pembejeo. Fao la bei litalinda ustawi wa wakulima wa korosho na kuwaepusha na hasara iwapo bei ya korosho ya msimu huu itaanguka tofauti na msimu uliopita. Hilo litawezekana kwa kutunga Sheria kuwezesha mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa mafao ya Bima ya Afya, Bima za Mazao na majanga (Crop Insurance) kwa kilimo na mifugo na Fao la Bei (Price Stabilization Benefit).
- Kuwaunganisha wakulima wote wa korosho nchini katika hifadhi ya jamii, na hivyo kuwa na uhakika wa akiba uzeeni kama ilivyo kwa wafanyakazi wa sekta rasmi pamoja na kupata faida ya Bima ya Afya, na hivyo matibabu bure yatokanyo na mifuko ya hifadhi ya jamii. Mchango kwa watu walio nje ya sekta rasmi ni shilingi 20,000 tu kwa mwezi.
- Kupanua hifadhi ya jamii na kuwafikia wakulima, wafugaji na wananchi wengine waliojiajiri kwa kutunga sheria itakayopelekea Serikali kuchangia theluthi moja ya kila mchango wa mwananchi atakayechangia kima cha chini cha michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Kwa sasa mchango wa 20,000 wa mtu asiye kwenye sekta rasmi unabaki kama ulivyo tu bila kujaliziwa.
- Serikali ichochee Tija kwenye Kilimo cha korosho kwa kuhakikisha tunaongeza thamani ya mazao ya korosho hapa nchini kwa kuhimiza kupunguza uuzaji wa korosho ghafi. Jambo hilo litawezekana kwa uwekezaji mkubwa wa viwanda vya ubanguaji wa korosho.
- Kutumia Hifadhi ya Jamii kuwezesha wakulima kujiwekea akiba kupitia vyama vyao vya msingi vya ushirika (Amcos) na kupata mikopo ya gharama nafuu ili kuanzisha upanuzi wa kilimo chao, uongezaji thamani wa mazao na kupata Bima ya Afya.
- Kutumia Hifadhi ya Jamii kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama miundombinu ya kilimo, viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, vyuo vya ufundi na miundombinu ya usafirishaji mazao kama reli kwani kwa uasili wake madai dhidi ya mifuko (liabilities) ni ya muda mrefu.
Hitimisho:
Sisi kama chama cha siasa, kwa kuzingatia falsafa ya chama chetu ya Siasa ni
Maendeleo, tunaendelea kusisitiza kuwa Serikali ni lazima itimize wajibu wake
wa kulinda maisha na hali za wananchi kwa kuhakikisha hakuna uhaba wa pembejeo
kwa wakulima hawa wa korosho nchini, kuhakikisha kuwa pembejeo husika znapatikana
katika bei ambayo watanzania wanaimudu, na zinapatikana kwa wakati. Ni muhimu
tukumbuke kuwa unapohujumu zao la korosho, unawahujumu wakulima zaidi ya 50000
wanaojishughulisha na kilimo cha zao la korosho; mamilioni ya wanakaya
wanaotegemea zao la korosho; mikoa zaidi ya 11 inayojishughulisha na kilimo cha
korosho na taifa kwa ujumla linalotegemea sana zao la korosho kwa uhai wake.
Sisi hatuwezi kukalia kimya hujuma hiyo
Ado Shaibu – Katibu, Kamati
ya Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi
ACT Wazalendo
Julai 30, 2017
Dar es salaam, Tanzania
SHARE
No comments:
Post a Comment