Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation Tawi la Tanzania Sibtain
Meghjee kulia, akimkabidhi Elizabert Tungu baiskeli (Wheel chair) kwa
ajili ya mwanaye Malale Mihayo (aliyekaa) ambaye ana tatizo la mtindio
wa ubongo.Kushoto ni Abass Meghjee mmoja wa wafadhili na kiongozi wa
taasisi hiyo yenye makao makuu nchini Uingereza.
Mwenyekiti
wa The Desk & Chair Foudation Tawi la Tanzania Sibtain Meghjee
akimsaidia kumsukuma Malale Mihayo mkazi wa Wilaya ya Kishapu mkoani
Shinyanga baada ya kumkabidhi msaada wa baiskeli (Wheel chair)
itakayomsaidia kwa usafiri. Mtoto huyo ana tatizo la mtindio wa ubongo.
Na Baltazar Mashaka, Mwanza
Familia
ya mtoto Malale Mihayo (12) yenye makazi yake katika Wilaya ya Kishapu
mkoani Shinyanga imeishukuru Taasisi ya The Desk & Chair Foundation
(TD&CF) Tawi la Tanzania kwa msaada wa baiskeli (Wheel Chair ) kwa
ajili ya mtoto wao mwenye tatizo la Cerebral Polse (mtindio wa ubongo).
Akizungumza
na mtandao huu baada ya kukabidhiwa baiskeli hiyo mama mzazi wa mtoto
huyo Elizabert Tungu alisema itampunguzia adha ya kumbeba mwanaye huyo
ambaye hana uwezo wa kufanya chochote kutokana na tatizo alilonalo.
“
Mwanangu alizaliwa mwaka 2008 akiwa mzima wa afya, alipata tatizo hili
baadaye akiwa na umri wa miaka 3 na nusu.Nilimpeleka kutibiwa
hospitali huko Arusha na Moshi madaktari wakanieleza anasumbuliwa na
tatizo la uti wa mgongo, licha ya kutibiwa hakupata nafuu.Nawashukuru
Desk & Chair kwa msaada huu,”alisema.
Bi.
Tungu mwenye familia ya watoto sita alisema alimpeleka kwa waganga wa
tiba za jadi nako hakupata nafuu na hivyo akalazimika kurejea nyumbani
ambapo mwanaye huyo aliendelea kukakamaa viungo vya mwili wake na
kupoteza uwezo wa kukaa wala kutembea.
Mtaalamu
wa viungo (Physiotherapy) Prisla Paul Mselle alisema Malale alipata
tatizo la kukosekana hewa ya oksjeni kwenye ubongo linalosababishwa na
uzazi pingamizi na homa kali kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano
na kushambulia tishu ya ubongo kwa kuwa ubongo unakuwa haujakomaa.
Alisema
kuwa mtoto huyo kupinda mgongo kumesababishwa na kuchelewa kupata tiba
haraka na hivyo anaweza kupata nafuu kwa kupata vifaa saidizi vya
kuchechemua misuli yake ambavyo kwa kitaalamu ni standing board,
stratching na standing table lakini hawezi kupona.
“
Baada ya kumbaini mtoto huyo niliangalia uwezo wake na kumwanzishia
mazoezi ya kumnyoosha viungo kama magoti, vifundo vya miguu kwa kutumia
vifaa vya kitaalamu ambavyo baadhi ni changamoto.Watoto wenye matatizo
haya ni wengi changamoto ni kuwabaini,”alisema.
Mtaalamu
huyo alieleza kuwa inahitajika elimu ya kutosha kwa jamii nyumba kwa
nyumna ili kuweza kuwafichua na kuwabaini watoto wengi wenye ulemavu
ambao wanafichwa kwa sababu ya mila potofu kuwa kuzaa mtoto mlemevu ni
laana, mikosi pamoja na imani za ushirikina.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation Sibtain
Meghjee alisema mtoto huyo ingawa amesaidiwa baiskeli hiyo anakabiliwa
na changamoto ya mavazi na mahitaji mengine na kumtaka mzazi wake
kumfungulia akaunti huku akiwaomba wadau wengine wajitokeze kumsaidia
mtoto huyo kwa hali na mali kwa sababu matunzo yake ni tofauti na ya
watoto wengine.
Alisema
taasisi hiyo itaendelea kumsaidia lakini kutokana na changamoto ya
kuwaibua watoto wenye matatizo hayo aliishauri serikali kuwa na mpango
mahsusi wa kuwabaini watoto wenye matatizo ya aina hiyo na kuweka
takwimu zao ili kurahisisha jinsi ya kuwahudumia na kuwapa misaada.
SHARE
No comments:
Post a Comment