Rais wa Marekani Donald Trump amemteua Waziri wa
Usalama wa Ndani John Kelly kuwa mkuu wa utumishi wa serikali baada ya
kumwachisha kazi Reince Priebus aliyehudumu katika wadhifa huo kwa miezi
sita
Baada ya miezi kadhaa ya uvumi kuhusu hatima ya Priebus, Trump
alitangaza uamuzi wake kwenye mtandao wa Twitter wakati aliwasili mjini
Washington baada ya kutoa hotuba jijini New York ambayo aliitumia
kummwagia sifa Kelly kwa kazi anayofanya katika wizara ya Usalama wa
Ndani.Alisema "nna furaha kuwafahamisheni kuwa nimemteua Jenerali/Waziri John F Kelly kuwa Mkuu wa Utumishi wa serikali katika Ikulu ya White House".
Wakati ujumbe huo ulianza kusambaa mjini Washington, Priebus aliondoka katika ndege ya rais Air Force One wakati mvua kubwa ikinyesha na akaingia kwenye gari pamoja na maafisa waandamizi wa Ikulu ya White House Steven Miller na Dan Scavino.
Muda mfupi baadaye, Miller na Scavino walitoka nje ya gari hilo na kuingia kwenye gari jingine. Gari lililombeba Priebus kisha likaondoka pamoja na msafara wa rais.
Priebus, kiongozi wa zamani wa Kamati ya Kitaifa ya chama cha Republican, amekuwa akilengwa na uvumi wa mara kwa mara kuhusu usalama wa kazi yake wakati kukiwa na malumbano ya kindani na sintofahamu ndani ya Ikulu ya White House.
Mnamo siku ya Alhamisi, alishambuliwa hadharani na mkurugenzi mkuu mpya wa mawasiliano katika Ikulu ya White House aliyeteuliwa na Trump, Anthony Scaramucci ambaye alimtuhumu Prebius kwa kutoa habari za kumharibia jina kwa vyombo vya habari.
Priebus alisema aliwasilisha ombi la kujiuzulu kwake siku ya Alhamisi na kuwa rais alikubali ijapokuwa wale walio karibu na rais huyo walisema kutimuliwa kwake kumekuwa kukishughulikiwa kwa wiki kadhaa sasa.
"nadhani rais alitaka kwenda mkondo tofauti," Priebus aliiambia televisheni ya CNN saa chache tu baada ya kutangazwa kutimuliwa kwake. Aliongeza kuwa anakubali kwamba Ikulu ya White House huenda ikanufaika na hatua ya kufanyiwa marekebisho na akasema "mimi daima ntakuwa shabiki wa Trump. Niko kwenye Team Trump."
Kelly ataapishwa rasmi kuchukua wadhifa huo siku ya Jumatatu. Wizara yake ya Usalama wa Ndani inahusika na kuweka usalama mipakani na amechukua msimamo mkali kuhusu wahamiaji walioko ndani ya Marekani.
Tangu alipoingia katika Ikulu ya White House miezi sita iliyopita, Trump amewaachisha kazi mshauri wake wa usalama wa taifa, naibu mshauri wa usalama wa taifa, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Upelelezi la Marekani – FBI, msemaji wa ikulu, mkurugenzi wa mawasiliano, naibu mwaneshiria mkuu, naibu mkuu wa utumishi wa serikali na sasa mkuu wa utumishi wa serikali, mabadiliko ya viongozi wakuu ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia ya kisiasa nchini Marekani.
SHARE
No comments:
Post a Comment