KWA
muda mrefu nimekuwa nikiandika makala zinazohusiana na rushwa katika
soka la nchi yetu kwa lengo la kuutahadharisha umma juu ya masahibu
yanayoendelea ambayo hakuna ubishi kwamba yanaharibu mfumo mzima wa
kiuendeshaji wa soka kwa ngazi zote kuanzia chini mpaka timu ya taifa.
Duniani
kote vitendo vya rushwa michezoni vimekuwa vikipigiwa kelele na
mamlaka za soka lakini bado wahusika wamekuwa wakitumia mbinu nyingi za
kuendeleza jambo hilo kwa kificho, huku wakitambua kwamba kufanya hivyo
ni kosa kubwa ambalo halihitaji kusamehewa kwa namna yoyote ile ili
kulinda hadhi ya soka.
Tumeshuhudia
katika mataifa mengi tu duniani vitendo hivyo vikivuruga taswira nzima
ya soka kwa baadhi ya wanafamilia kupanga matokeo, kuhonga waamuzi na
hata kuhonga viongozi wanaosimamia michuano fulani kwa lengo la
kujipatia ushindi wasiostahili.
Wengine
huenda mbali zaidi kiasi cha kufikia hatua ya kuzihujumu klabu zao
wenyewe kwa kurubuni wachezaji kadhaa ndani ya kikosi ili wacheze chini
ya kiwango ili kujifurahisha wao na wale waliowakusudia, lakini
wakitambua kuwa kufanya hivyo hakuleti maendeleo yoyote ya kuisogeza
mbele nchi yetu kufika katika viwango vya juu vya soka.
Ukichunguza
kwa makini mzizi wa hayo yote utagundua kuwa, unaanzia kwenu viongozi
mliopewa dhamana ya kusimamia soka letu ambao mmeaminiwa na wapiga kura
kwa kuwachagua kwa kura nyingi baada ya kutamba na maneno matamu ya
kuleta matumaini wakati wa kampeni zenu za kuomba ridhaa ya uongozi
katika chaguzi.
Agosti 12, mwaka huu taifa litashuhudia patashika za uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)utakaowaweka
madarakani rais, makamu wake na wajumbe kadhaa walioomba ridhaa ya kuwa
viongozi wa taasisi hiyo nyeti iliyo na dhamana ya kusimamia na
kuratibu shughuli zote zinazohusiana na soka katika nchi yetu.
Sasa
wakati tukisubiri uchaguzi huo kufanyika, tayari imesharipotiwa kuwepo
na vitendo vya rushwa kwa baadhi ya wagombea wa uchaguzi huo ambapo
wapiga kura wake wameanza kuwekwa kwenye kisahani cha kurubuniwa kwa
kitu kidogo ili wawachague bila kujali uwezo wao wa kuongoza, weledi,
uadilifu na nia iliyowasukuma mpaka kufikia hatua ya kujitosa kwenye
kinyang’anyiro kuomba ridhaa ya kuongoza.
Kwa
mtindo huo unaweza ukajiuliza ni kwa kiasi gani Tanzania inaweza kupiga
hatua katika maendeleo ya mpira wa miguu kama watachaguliwa viongozi
waliopigiwa kura kwa kutoa rushwa? Swali hili lina majibu rahisi tu
kwamba Tanzania haiwezi kupiga hatua yoyote kwa kuwa mfumo mzima wa
uendeshaji utagubikwa na vitendo vya rushwa na kukosekana kwa ushindani
wa kweli unaozingatia vigezo.
Ifike
wakati tuache kuoneana aibu katika masuala muhimu yanayobeba maslahi ya
taifa zima, kama kweli tunahitaji kupiga hatua ya kimaendeleo ya soka
kama yalivyo mataifa mengine duniani ambayo yamedhamiria kwa vitendo
kujiletea mafanikio kupitia medani hiyo, vinginevyo basi tutaishia kuwa
wasindikizaji kila kukicha na kuwaacha wenzetu wakizidi kuchanja mbuga.
Nitumie
makala haya pia kuipongeza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru) kwa kuthubutu kwa vitendo kutimiza wajibu wenu, kwani kwa
muda mrefu wadau wamekuwa wakiwanyooshea kidole kwa kufumbia macho
matukio mengi ya rushwa yaliyojitokeza ambayo yamekuwa yakiziumiza
klabu nyingi.
Klabu
zinaweza kuwa na mikakati mizuri ya kupata ushindi katika michuano ili
kufikia malengo waliyojiwekea lakini harakati hizo zimekuwa
zikikwamishwa kwa makusudi na watu wachache ambao hawana nia njema
katika maendeleo ya soka kwa taifa hili.
Madhara
ya rushwa katika soka ni mengi mno ikiwemo kufifisha ndoto za
wachezaji wanaotamani kuvuka mipaka kwenda kucheza soka la kulipwa nje
ya nchi, kukatisha tamaa hata watoto wadogo wenye nia ya kucheza mpira
na kudumaza mawazo na mbinu za watu wenye nia ya kutuletea mafanikio ya
kweli kwenye soka kwa kutumia njia zinazokubalika duniani kote.
Ushauri
wangu kwenu Takukuru, msije mkalegeza kamba kwenye ufuatiliaji ili
kuwabaini hata wale waliojificha kwenye vichaka sugu vya rushwa, naamini
kwa kufanya hivyo mnaweza mkawa nguzo muhimu na chachu kwa taifa
kuelekea maendeleo ya kweli katika soka.
SHARE
No comments:
Post a Comment