TRA

TRA

Monday, July 17, 2017

Tumewatesa watoto wetu vya kutosha

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !




 Watoto wasitumiwe vitani 


Julian Msacky

RIPOTI iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), inasikitisha.

Inaonesha namna watoto wanavyoishi maisha ya mateso barani Afrika na kujiingiza katika vitendo visivyofaa.

Shirika hilo limesema vurugu zimesababisha mamilioni ya watoto kukimbia makazi yao huku wengi wao wakiishi katika mazingira magumu. 
 
Ripoti hiyo inalaani ukosefu wa upatikanaji wa huduma muhimu kwa watoto ambapo takriban watoto milioni 50 duniani kote wanaishi katika mazingira hayo. 

Tatizo hili linasababisha watoto wajione wapweke na kutofurahia maisha ya utoto kama walivyo wengine. 

Ni wakati muafaka sasa kwa nchi za Afrika kuweka mazingira bora ya watoto ili waweze kuishi salama na kupata haki zao za msingi.

Haki hizo ni pamoja kutunzwa, kupatiwa elimu, chakula, malazi na huduma nyingi muhimu ambazo kimsingi anastahili kila mtoto.

Ili kufikia hatua hiyo lazima viongozi wa kisiasa waache kugeuza nchi zao uwanja wa vita na ngome za mapambano.

Viongozi wetu wafahamu kuwa kwa namna moja ama nyingine wamechangia kwa kiwango kikubwa mateso ya baadhi ya watoto.

Baadhi yao wameweka madaraka mbele kuliko utu. Wanaangalia namna wanavyopoteza maisha kwa kukosa chakula au dawa.

Lakini wao wenyewe hawapo tayari kukosa fedha za uchaguzi au kuendesha maisha yao. Kwa mfumo huo uko wapi upendo tunaohubiri?


Wapo tayari kuwapatia watoto wao tiba nzuri wanapokohoa au kupiga chafya, lakini wengine wanakufa kwa matatizo hayo hayo. Kweli?

Hapa tena, usawa uko wapi? Kama hiyo haitoshi viongozi hao hao wapo tayari kuingiza nchi zao kwenye vita bila kujali watu watakavyoathirika, wakiwemo watoto.

Katika hili nchi mmoja inapokuwa haina vita haina maana hakuna watoto wanaoteseka, wapo wanaotaabika kwa namna nyingine.

Kwa msingi huo chimbuko la mateso kwa watoto linatakiwa kuangaliwa kwa undani badala ya kuangalia juu juu. 

Kutokana na vita watoto wamekuwa waathirika wa kukimbia huku na kule kunusuru maisha yao huku hatima yao ikiwa haijulikani. 

Inasikitisha pia kuona kwamba madaraka yanapewa kipaumbele zaidi kuliko uhai wa watu, zikiwemo haki zao za msingi.

Hebu tujiulize ni kiongozi gani leo hii ana habari na watoto ambao wanakimbia huku na kule ili kuepuka vita katika nchi zao? 

Ni kweli tumefikia hatua ya kutoona thamani ya watoto ambao tuliwatafuta kwa jasho tena tukiomba Mungu usiku na mchana?

Kama kweli hivyo ndivyo ni kwa nini tunawaacha watoto wateseke na kufanya kazi za kutumishwa na wengine kuwa watumwa wa kingono? 

Tukiwa kama wazazi, walezi na viongozi ni lazima tubadilike. Pili ni lazima tuhakikishe tunawaandaa watoto wetu vizuri na kuhakikisha haki zao za msingi zinaheshimiwa. 

Kama ni migogoro ya kisiasa ndiyo inasababisha wazazi washindwe kutunza watoto wao hatuna budi kuachana nayo.

Kama ni ndoa kuvunjika ni lazima wazzai wabadilike na kuhakikisha wanalinda ndoa kwa ustawi wa watoto.

Tukumbuke kuwa migogoro ya ndoa inachangia pia matatizo kwa watoto, hivyo ni vizuri tuheshimu ndoa zetu kwa ustawi wa watoto wetu.

Kwa kufanya hivyo watoto watalelewa katika mazingira mazuri na kutoa fursa kwao kupata huduma muhimu za kijamii ambazo kwa leo hii hawazipati.

Ndiyo maana tunasikia watoto wakikimbilia migodini ambako wanafanya kazi za kutumishwa huku wakiathiriwa na kemikali ambazo ni hatarishi kwa maisha yao.

Kama tunawapenda watoto wetu ni lazima tuwakinge na kila lililo baya. Ni lazima tuhakikishe wanapata elimu nzuri.

Ni lazima tuhakikishe wanapata chakula bora ili kulinda afya zao na kukuza miili yao inavyotakiwa.
Tuna kila sababu ya kuhakikisha wanapata elimu ambayo ndiyo msingi muhimu wa maisha. 

Tukiwanyima elimu tunawaharibu.
Bila elimu watashindwa kutoa mchango unaostahili katika kuharakisha maendeleo yao pamoja na nchi kwa ujumla.

Watoto wakikosa elimu madhara yake ni mengi maana watashindwa kupanga aina ya maisha wanayotaka na hii ni hatari kubwa. 

Sisi kama Waafrika na Watanzania tusikubali watoto wetu waishi maisha ambayo yatakuwa mateso kwa siku zao za usoni. 

Tunasema hivi kwa sababu tunazo mali za kutosha kuwaondoa watoto wetu katika matatizo wanayokumbana nayo leo hii.    

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger