WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewashauri
walimu kuisaidia Benki ya NMB kutoa elimu ya masuala ya kibenki na hasa
umuhimu wa kujiwekea akiba kwa jamii wakiwemo watoto ili iweze
kuwasaidia hapo baadaye. Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam
na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Eleuther
Mwageni alipokuwa akimwakilisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia kufungua semina ya walimu Mkoa wa Dar es Salaam
iliyoandaliwa na Benki ya NMB. Akizungumza kabla ya kufungua semina hiyo, Prof. Mwageni alisema
mpaka sasa idadi ya wananchi wanaotumia huduma za kibenki haizidi
asilimia 20 jambo ambalo linaonesha bado kuna idadi kubwa ya Watanzania
hawatumii mfumo rasmi wa kibenki licha ya manufaa mbalimbali
yanayopatikana kwa watumiaji. Aliipongeza Benki ya NMB kwa hivi sasa kuwa na programu ya kuzunguka
mashuleni kutoa elimu za kibenki kwa wanafunzi na wazazi wao na kuonesha
manufaa ya kujiwekea akiba kwa wazazi na wanafunzi, hivyo kuwataka
waalimu kushirikiana katika kueneza elimu hiyo zaidi kwa jamii nzima.
“Hadi sasa si zaidi ya asilimia 20 ya Watanzania wanaotumia huduma rasmi
za kibenki…hivyo kuna haja ya kuwaunga mkono NMB kuendelea kutoa elimu
za kibenki ili idadi ya watumiaji huduma hizo iongezeke,” “Nawapongeza pia kwa huduma nzuri za kibenki mnazozitoa kwa walimu,
mikopo mbalimbali imekuwa msaada mkubwa kwa walimu pamoja na familia
zao…naomba sasa ongezeni na kuwapa mikopo ya kujiendeleza kielimu. Elimu
kwao itakuwa msaada mkubwa kwani sasa kuna ushindani wa kila kitu,”
alisema Profesa Eleuther Mwageni. Akizungumza awali kabla ya mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi wa Wateja
wadogo na wakati NMB, Abdulmagid Nsekela alisema walimu ni wateja muhimu
wa NMB na wametoka mbali na benki hiyo hivyo wataendelea kuwajali kwa
kutoa huduma ya kipekee kwao. Alisema wanatambua pia ni watu muhimu
katika taifa na jamii kwa ujumla, hivyo kitendo cha kukutana nao kwenye
semina hiyo watatoa maoni ambayo yataboresha zaidi benki hiyo. Alisema NMB itaendelea kuboresha huduma zake kiteknolojia ili
kumrahisishia mteja kupata huduma hizo muda wowote na popote. Aliongeza
kuwa benki hiyo ni ya kwanza kuja na huduma za simu za kibenki ambazo
zimewarahisishia wateja kujihudumia wenyewe kwa baadhi ya huduma.
alibainisha hivi karibuni ilileta huduma za NMB wakala ambayo pia
imeendelea kuboresha huduma kwa wateja. Katika semina hiyo iliyowakutanisha walimu wa shule za msingi,
sekondari na baadhi ya vyuo na wataalam anuai wa NMB, washiriki watapata
fursa ya mafunzo ya kibenki na kutoa maoni mbalimbali yatakayopokelewa
na kwenda kufanyiwa kazi lengo ikiwa kuboresha zaidi huduma za wateja wa
benki hiyo.
No comments:
Post a Comment