TRA

TRA

Saturday, July 15, 2017

Watanzania mil. 27 sasa wanapata huduma bora za maji

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !
Ripoti mpya iliyotolewa Alhamis wiki hii na Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNICEF, imesema upatikanaji wa huduma za msingi za maji na zenye kusimamiwa vema zimeimarika nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hivi sasa nchini Tanzania, mtu 1 kati ya 2, au Watanzania milioni 27 wanapata huduma za msingi za maji—kwa maana ya kwamba zinapatikana ndani ya mwendo wa dakika 30 kwenda na kurudi kuteka maji ukiwemo muda wa kupanga mstari.
Hata hivyo, bado kuna kasi ndogo ya maendeleo katika usafi wa mazingira na mwili kwani asilimia 63 ya Watanzania hawana huduma bora za kujifanyia usafi.
Ulimwenguni kote, walau watu 3 katika 10 au watu bilioni 2.1 hawapati maji salama na kwa kiasi cha kutosha nyumbani na watu 6 katika 10, au watu bilioni 4.4 hawana huduma za usafi zinazosimamiwa kwa usalama.
Ripoti ya Programu ya Usimamizi wa Pamoja, Maendeleo katika Huduma za Maji ya Kunywa, Usafi wa Mazingira na Mwili: Taarifa Mpya za 2017 na Kigezo cha Lengo la Maendeleo Endelevu (Progress on Drinking Water, Sanitation and Hygiene: 2017 Update and Sustainable Development Goal Baselines), inaonyesha tathmini ya kwanza ya ulimwengu ya huduma za maji ya kunywa na usafi “zinazosimamiwa kwa usalama”.
Katika ngazi ya ulimwengu, ripoti inaonyesha kwamba mabilioni ya watu wamepiga hatua katika kupata huduma za msingi za maji ya kunywa na usafi wa mazingira tangu mwaka 2000, lakini huduma hizi si lazima kwamba zinatoa maji na mazingira safi yaliyo salama. Makazi mengi, vituo vya afya na shule nyingi bado hazina sabuni na maji kwa ajili ya kunawa mikono. Jambo hili linaziweka afya za watu wote—hasa watoto wadogo—katika hatari ya kupata magonjwa, kama vile kuhara.
Matokeo yake, kila mwaka kote ulimwenguni, watoto 361,000 wenye umri wa chini ya miaka 5 wanakufa kwa kuhara. Huduma duni za maji, usafi wa mazingira na mwili (WASH) zinaendelea kuathiri uwezekano wa kuishi na afya ya watoto. Nchini Tanzania, asilimia 8 ya vifo vya watoto chini ya miaka 5 vinasababishwa na kuharisha ambao ni ugonjwa unaozuilika.
“Siyo tu kwamba usafi duni, kujisaidia popote, na ukosefu wa maji salama na mifumo ya usafi ndiyo vyanzo vikuu vya magonjwa na vifo vya watoto, bali yanachangia pia katika utapiamlo na kudumaa, na haya yanakuwa vikwazo kwa elimu ya wasichana na fursa za kiuchumi kwa watu maskini,” alisema Maniza Zaman, Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania. “Takwimu hizi mpya zinatoa picha halisi na kuonyesha tofauti kubwa kabisa za ukosefu wa usawa wenye haki, ikiwemo nchini Tanzania, kwa maana ya nani ananufaika na huduma za maji salama na usafi. Huu ni wito wa kuanzisha vuguvugu la kitaifa ambalo kweli litaimarisha huduma za maji, usafi wa mazingira na wa mwili ili kwamba kila mmoja afikiwe hasa katika maeneo yaliyo nyuma, jamii maskini kabisa na watoto walio hatarini sana, wakiwemo watoto wenye ulemavu,” aliongeza.
Ripoti inazidi kufafanua kwamba bado kuna ukosefu wa usawa kati ya jamii za vijijini na mijini. Kwa mfano, nchini Tanzania, ni asilimia 37 tu ya wakazi wa vijijini wanaopata huduma bora za msingi za maji (mwendo wa dakika 30 kwenda na kurudi) kulinganisha na asilimia 80 ya wakazi wa mijini.  
Akizungumzia umuhimu wa maji na usafi kwa afya bora, Dkt. Matthieu Kamwa, Mwakilishi wa WHO nchini Tanzania anasema, “Upatikanaji wa maji salama na usafi wa kutosha unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha ubora wa maisha na uzalishaji kwa ajili ya maendeleo endelevu. Lengo la SDG la 6 linatoa wito wa kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji na usimamizi endelevu wa maji na usafi kwa wote. Ni wito mtukufu wa kuleta hakikisho kwamba hakuna mtu yeyote anayeachwa nyuma kama kanuni muhimu ya kufikia kila lengo lililoainishwa katika SDGs”.
Hakujawahi kuwepo hapo kabla haja kuu ya kutetea haki za kupata maji, usafi wa mazingira na mwili kwa raia wote na hasa kwa watoto wetu kama ilivyo sasa. Uwekezaji, uanzishwaji ushirika, uchukuaji hatua madhubuti na uwajibikaji mkubwa unaosukumwa na data ili kuleta matokeo unahitajika ili kwamba haki hii ya msingi ifanyike kweli kwa wote.

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger