TRA

TRA

Friday, July 28, 2017

WAZIRI ATOA TAMKO LA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HOMA YA INI DUNIANI

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !


 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akitoa tamko katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya  Homa ya Ini Duniani wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo asubuhi. Kushoto ni Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Bakari Kambi.

 Tamko likitolewa kwa wanahabari.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
 Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakiwa kazi wakati wa tamko hilo.
Tamko likitolewa.
Ndugu wananchi
Tarehe 28 Julai ya kila mwaka, ni siku iliyoteuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama siku ya Homa ya Ini (World Hepatitis Day). Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuielimisha na kuikumbusha jamii kutambua athari za ugonjwa wa Homa ya Ini, jinsi ugonjwa huu unavyoambukizwa, na namna ya kujikinga na ugonjwa huu. Ni jambo muhimu kwa nchi zote duniani kushirikiana katika kupambana na ugonjwa huu. 
Ndugu wananchi
Katika kuadhimisha Siku hii, kila mwaka  Shirika la Afya Duniani hutoa kauli mbiu yenye ujumbe maalum, unaolenga kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu madhara yanayotokana na ugonjwa huu. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani kwa mwaka huu wa 2017 ni:- “Tokomeza Homa ya Ini” (“Eliminate Hepatitis”). Kauli mbiu hii inatulazimu Serikali kuweka mikakati ya pamoja na wananchi  ili kuweza kudhibiti ugonjwa huu nchini na hatimaye kuweza kuutokomeza kabisa.
Ndugu wananchi
Maadhimisho haya pia yanatoa fursa ya nchi yetu kuongeza juhudi za kutekeleza Mpango Mkakati wa kwanza wa Dunia wa Homa ya Ini (Global Health Sector Strategy on Viral Hepatitis) kwa mwaka 2016-2021, ambao tuliuridhia ukiwa na lengo la  kuziwezesha nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani kufikia lengo la kuutokomeza ugonjwa wa Homa ya Ini. 
Ndugu wananchi
Ugonjwa wa Homa ya Ini ni tatizo linalohitaji juhudi za dhati kupambana nalo. Ugonjwa huu umetajwa kuwa wa hatari na unaoua idadi kubwa ya watu pole pole.
Kati ya watu 100, watu 8 wanaweza kuwa na maambukizi sugu ya ugonjwa huu na wanaweza wasionyeshe dalili. Aidha, maambukizi ya ugonjwa huu ni makubwa mara 10 zaidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na kwamba asilimia kubwa ya wagonjwa huugundua ugonjwa huu kwenye hatua za mwisho na hivyo kushindwa kupata matibabu mapema na kupelekea  mgonjwa kupoteza maisha. 
Ndugu wananchi,
Maambukizi ya Homa ya Ini husababishwa na virusi ambavyo vinapoingia mwilini mwa binadamu, hushambulia ini na hivyo kulifanya wakati mwingine lisinyae na kushindwa kufanya kazi vizuri. 
Katika hatua za mwishoni mwathirika wa ugonjwa huu anaweza kupata saratani ya ini. Homa hii inaenezwa kwa njia mbalimbali kulingana na kundi la virusi hivi. Virusi vya homa ya ini vipo katika makundi matano, yaani  A, B, C, D na E. 
Pamoja na virusi hivi pia homa ya ini inaweza kusababishwa na matumizi ya dawa kiholela, vilevi kupita kiasi, aina mbalimbali za sumu na pia magonjwa mengine ambayo yanashambulia kinga za mwili na ini. 
Uhakika wa mgonjwa kuwa na maambukizi haya hupatikana kwa kufanyiwa vipimo maalum vya kimaabara.
Ndugu wananchi
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa, vifo vitokanavyo na Homa ya Ini vinaendelea kuongezeka. Mnamo mwaka 2015 kulikuwa na vifo milioni 1.34 kutokana na Homa ya Ini ambavyo vilikuwa sawa na vile vitokanavyo na Kifua Kikuu na zaidi ya vile vitokanavyo na ugonjwa wa UKIMWI ambavyo vilikuwa milioni 1.1.  Mwaka 2015 kulikuwa na maambukizi mapya milioni 1.75 kwa watu wazima kutokana na virusi aina ya C, hususan kutokana na matumizi ya sindano yasiyo salama. 
Ndugu wananchi,
Kwa Tanzania tafiti na takwimu chache zilizopo zinaonyesha uwepo wa maambukizi ya virus vya Hepatitis B na C. Mfano kati ya wachangiaji damu 200,000 kwa mwaka 2016, asilimia 6 kati yao (takriban watu 12,000) walikuwa na maambukizi ya Hepatitis B.  Aidha, tafiti zinaonyesha kuwa, kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini Homa ya Ini inayosababishwa na virusi vya aina B (Hepatitis B) inakadiriwa kuwepo kwa asilimia asilimia 16-50. Kwa upande wa Homa ya Ini inayosababishwa na virusi aina ya C (Hepatitis C) inakadiriwa kuwepo kwa asilimia 2% miongoni mwa wanajamii. 
Aidha maambukizi ya homa ya Ini ya aina ya B na C (Hepatitis B na C) ni tatizo kubwa miongoni mwa watu wenye maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. 
Ndugu wananchi
Matibabu ya Homa ya Ini ni ya gharama kubwa na ndio maana tunasema ni bora kinga kuliko Tiba. Tiba kwa Wagonjwa waliopata kirusi aina ya A na E, mara nyingi hutolewa kutokana na dalili zinazoambatana na ugonjwa huu. 
Kwa wagonjwa waliogundulika kuwa na Hepatitis B au C, matibabu hutegemea hatua mgonjwa aliyofikia. Wakati mwingine magonjwa hulazimika kupewa dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa huo kwa kipindi chote cha uhai wake. 
Gharama za dawa hizi ni kubwa sana. Kwa mgonjwa aliyepata maambukizi ya Homa ya Ini kupitia Virusi aina ya C, gharama ya dawa ni kati ya shilingi Milioni Tatu hadi Tano kulingana na muda wa tiba. Kupitia mradi maalum wa awali (“Hepatitis B and C Pilot project”), matibabu kwa wagonjwa walioathirika hapa nchini yanatolewa bila malipo katika hospitali maalum ya Muhimbili. 
Hadi sasa hakuna dawa maalum inayotumika kutibu virusi vya  aina ya Hepatitis D.
Ndugu wananchi
Ugonjwa huu unaweza kukingwa kwa kutumia chanjo ambayo hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya virusi hivyo. Kwa maambukizi ya kirusi aina ya B, chanjo ya ugonjwa huo hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya virusi hivyo na hutoa kinga kwa kipindi chote cha maisha yake. 
Hapa nchini chanjo hii kwa sasa hutolewa kwa watoto wachanga bila malipo. Chanjo hii ambayo ilianza kutolewa kwa watoto wachanga nchini waliozaliwa kuanzia mwaka 2003 ipo kwenye mchanganyiko wa Pentavalenti. 
Hadi kufikia mwaka 2015, inakadiriwa kuwa asilimia 97% ya watoto wote waliozaliwa kuanzia mwaka 2003 walipata chanjo hiyo. 
Chanjo ya Hepatitis A ipo na inatumika kwa baadhi ya nchi lakini hapa nchini kwetu hatujaanza utaratibu wa kutoa chanjo hiyo kwasababu tatizo kubwa zaidi linalotukabili kwa sasa ni Hepatitis B. Hakuna chanjo dhidi ya  Hepatitis C, D na E.  Hata hivyo Ugonjwa wa Hepatitis D unaweza kuzuilika kwa kuwachanja watu dhidi ya Hepatitis B. 
Ndugu wananchi,
Kama wajibu wa waajiri kuwakinga watumishi wao sehemu za kazi, chanjo ya kuzuia maambukizi ya Hepatitis B hutolewa kwa watumishi wa sekta ya Afya kwa gharama ya serikali. Wizara imekuwa ikiratibu utoaji wa chanjo ya homa ya ini kwa watoa huduma za afya kwa lengo la kuwakinga watumishi wa afya ambao wana hatari mara mbili ya kupata ugonjwa huu. 
Kwanza kwa kupata maambukizi wawapo kazini katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ya kutoa huduma za afya na pia wanapokuwa katika jamii kama sehemu ya jamii. Kwa upande mwingine, sekta binafsi zina utaratibu wao wa kugharamia chanjo kwa ajili ya kuwakinga watumishi wao sehemu za kazi.  
Ndugu wananchi
Kwa sasa Wizara inaangalia namna ya kufikia jamii iliyobaki ili kuweza kuwapatia chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B. Wizara imeshafanya mchanganuo rasmi ambao unaonesha kiasi cha gharama ya kununua chanjo na vitendanishi vya vipimo vya awali, kutunza chanjo, kusambaza chanjo na shughuli yenyewe ya uchanjaji. 
Wizara pia inaangalia uwezekano wa kupata wadau kwa ajili ya kushirikiana nao katika kazi ya kutoa chanjo hii. Kwa sasa, mtu binafsi anayetaka kupata chanjo ya kujikinga na Hepatitis B, inabidi alipie. Katika sekta binafsi, chanjo ya Hepatitis B inapatikana kwa shilingi 50,000 hadi 75,000 kwa mtu mmoja kwa dozi moja. Vituo vinavyotoa chanjo hii ni pamoja na Premier Care Clinic, IST na Hindu Mandal kwa mkoa wa Dar es salaam. 
Ni matarajio yetu kuwa gharama hizi zitapungua kwa kiasi kikubwa na kuwezesha chanjo kupatikana katika vituo vingi vya kutolea tiba hasa vya umma baada ya uamuzi wa serikali kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ambapo bei ya chanjo ya Homa ya Ini katika Bohari ya Dawa (MSD) sasa inauzwa shillingi 5,300  kutoka shillingi 22,000.
Ndugu wananchi
Hatua zinazofanyika na Wizara katika kudhibiti Homa ya Ini ni pamoja na :-  1. Kuunda kikosi kazi cha Taifa kinachojumuisha wataalam kutoka taasisi mbalimbali. Kikosi kazi hiki kimepewa jukumu la kuandaa Mpango Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti na Kutokomeza Ugonjwa wa Homa ya Ini nchini. Aidha kamati hii inakamilisha Mpango Mkakati wa kudhibiti ugonjwa wa Ini nchini wa 2017-2021
2. Kuandaa vielelezo vinavyohusu ugonjwa wa Homa ya Ini (Viral Hepatitis), ili kuuelimisha umma juu ya ugonjwa huu na namna gani maambukizi yanaweza kuzuiwa.


3. Kuendelea kutoa chanjo kwa watumishi wa afya ambapo katika mwaka 2015 Wizara ilinunua dozi zaidi ya 650,000 ya chanjo dhidi ya Hepatitis B kwa ajili ya kuwachanja watumishi walio katika mazingira hatarishi na chanjo hiyo imekwishasambazwa katika mikoa yote.


4. Aidha, Wizara inakamilisha mipango ya uwezekano wa kuhakikisha chanjo hii ya Hepatitis B inapatikana kwa watu wote wanaohitaji na kwa gharama nafuu.


Ndugu wananchi,


Kwa sasa hakuna ushahidi wa mlipuko wa homa ya ini nchini. Hata hivyo, wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki wapo katika hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu, hususan Hepatitis B na C, kuliko aina nyingine, yaani A, D na E kutokana na kuwa njia za maambukizi ya Virusi vya aina ya B na C hufanana kwa kiasi kikubwa na zile za maambukizi ya VVU. 


Leo tunapoadhimisha Siku ya Homa ya Ini, na ili tuweze kwenda sambamba na mataifa mengine duniani na katika kufanikisha Ajenda ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, Msisitizo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni kwa wananchi na wadau wote kuendelea kuona umuhimu na kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Ini  hususan kwa kutumia fursa zilizopo na  kuwekeza katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu.


Naomba nihitimishe kwa kuwataka wafanyakazi wa Mpango wa Damu Salama kuendelea na kazi nzuri ya kupima damu zote za wachangiaji, kuwataka wafanyakazi wa sekta ya afya kuzingatia kanuni za usalama, kuwashauri jamii kuepuka na kujidunga madawa ya kulevya, kuepuka ngono zembe, na mwisho kabisa kuwaomba wadau wote kushirikiana na Serikali katika juhudi za kuondoa ugonjwa wa Homa ya Ini hapa nchini.

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger