Katibu
Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amemjibu Msajili wa Vyama vya
Siasa nchini Mhe. Jaji Francis S.K.Mutungi kuhusu sakata la kufukuzwa
uanachama wanachama saba wa CUF na kuhusu kutomtambua yeye kama Katibu
wa CUF.
Maalim
Seif amedai kuwa wao kama CUF hawakubaliani na maamuzi ya Jaji Mutungi
kumtambua Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF kwa kuwa wao tayari
walishamfukuza uanachama hivyo si mwanachama wa CUF na wala hana sifa ya
kuwa kiongozi katika chama hicho.
"Mheshimiwa
Msajili unafahamu fika kuwa Profesa Ibrahim H. Lipumba mwenyewe aliamua
kujiuzuilu uenyekiti wa taifa wa Chama cha CUF. Pamoja na kuniandikia
mimi nikiwa Katibu Mkuu na pia Katibu wa Mamlaka iliyomchagua (Mkutano
Mkuu wa Taifa) kunijulisha kuwa amejiuzulu, pia alikwenda kwenye mkutano
na waandishi wa habari akatangaza hadharani kuwa amejiuzulu"
Maalim Seif alizidi kufafanua
"Hatimaye
Mkutano Mkuu wa Taifa wa CUF ukaitishwa na Katibu Mkuu akatoa taarifa
ya kupokea barua ya kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Lipumba nafasi yake ya
Uenyekiti wa Taifa wa Chama. Nikaisoma barua yake mbele ya Mkutano Mkuu
wa Taifa, na baada ya mjadala wa kina maamuzi yakachukuliwa kwa mujibu
wa matakwa ya Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014) kwa kupiga kura.
Wajumbe 437 wakakubali kujizulu kwa Profesa Lipumba dhidi ya Wajumbe 14
waliokataa. Hivyo Profesa Ibrahim H. Lipumba kuanzia siku aliyojiuzulu
si Mwenyekiti wa Taifa wa CUF. Profesa Lipumba hana mamlaka ya
kukiongoza Chama chetu" alisisitiza
Aidha
Maalim Seif anasema kutokana na maamuzi hayo ya CUF baadaye Profesa
Lipumba alikuwa akilalamika kwa Msajili wa Vyama Vya Siasa kufuatia
maamuzi hayo na baadaye Msajili alitoa msimamo wake kuwa anamtambua
Lipumba kama Mwenyekiti wa Taifa wa CUF ingawa Katibu Mkuu wa CUF
anasema msajili hana uwezo huo wa kumrudisha Lipumba kama Mwenyekiti wa
CUF
"Najua
kuwa alikulalamikia, ukaniletea barua zake za malalamiko na ukataka
maoni ya Chama. Nikakujibu kwa maandishi. Kwenda na kurudi ukatoa kile
ulichokiita Msimamo wa Msajili juu ya kadhia iliyokikumba Chama! Huo ni
Msimamo sio hukumu. Maana kama ni hukumu ningetarajia katika huo ulioita
msimamo ungeeleza kuwa kwa uwezo uliopewa na kifungu Na. kadhaa cha
Sheria ya Vyama vya Siasa Na.5 ya 1992, au kwa mujibu wa uwezo uliopewa
na Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014) katika kifungu Na. kadhaa
umeamua kumrudisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa
CUF. Lakini hukuweza kuonyesha uwezo wako wa kisheria au kikatiba
kumrudisha Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Taifa CUF kwa sababu huna
uwezo huo kwa mujibu wa sheria za nchi wala kwa mujibu wa Katiba ya CUF" alisema Maalim Seif
Katibu
Mkuu wa CUF amesema wao wanazidi kumshangaa msajili wa vyama vya siasa
nchini Jaji Mutungi kuendelea kushirikiana na Profesa Lipumba hata
katika mambo ambayo yanatia aibu kama kutaka kutoa ruzuku za chama na
kumpa Lipumba na genge lake.
"Tunaloshuhudia
ni kila kukicha unaendelea kumuunga mkono Profesa Lipumba hata katika
mambo ya aibu ya kula njama na Profesa Lipumba kumuwezesha atoe ruzuku
ya CUF kinyume na matakwa na taratibu zilizowekwa katika Katiba ya CUF
ya 1992 (Toleo la 2014). Narudia kusema kuwa Prof. Lipumba si Mwenyekiti
wa Taifa wa CUF. Lakini kutokana na vitendo vyake vya kukosa nidhamu
katika kusababisha vurugu katika kikao cha dharura cha Mkutano Mkuu wa
Taifa wa chama chetu, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kwa uwezo lillonao
kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya CUF, lilimfukuza Profesa Ibrahim
Lipumba uanachama wa CUF. Taarifa hiyo pia nilikuletea, lakini umeamua
kuitia kapuni ili kutimiza matakwa yako binafsi. Ikiwa Profesa Ibrahim
H. Lipumba sio mwanachama wa CUF, hawezi kabisa kuwa kiongozi wa Chama,
hasa nafasi ya juu kabisa katika Chama. Kinachotokea kikiongozwa nawe na
Ofisi yako ni ubabe, kutojali sheria za nchi wala Katiba ya Chama chetu
ilimradi mufikie lengo lenu" alisema Maalim
Mbali
na hilo Maalim Seif aliweka msimamo wake kuwa Chama Cha Wananchi CUF
hakiendeshwi na hisia za mtu wala hakiwezi kupangiwa kiongozi na kudai
ni CUF ni taasisi inayoongozwa na sheria za nchi na Katiba na si
vinginevyo.
"Mheshimiwa
Msajili napenda utambue kuwa CUF ni taasisi, tena Taasisi makini.
Kinaendeshwa na kuongozwa kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba ya
Chama hicho pamoja na Kanuni ambazo hutungwa na mamlaka husika kila
inapohitajika. Sisi viongozi wa CUF tunajitahidi kuongozwa na sheria za
nchi, Katiba ya Chama na Kanuni zake katika kukiendesha chama.
Hatuongozwi na matakwa ya mtu yeyote, hata kama mtu huyo ni Msajili wa
Vyama vya Siasa. Ninavyofahamu Msajili hana mamlaka ya kupandikiza watu
anaowataka kuwa viongozi wa chama chetu. Msajili hana uwezo wa kuingilia
maamuzi halali ya vikao halali vya Chama chetu. Viongozi huchaguliwa
/kuteuliwa na wanachama wenyewe/viongozi halali wa chama" alisisitiza Maalim Seif
SHARE
No comments:
Post a Comment