Serikali ya Kenya
imeanza kutekeleza marufuku ya mifuko ya plastiki nchini humo baada ya
juhudi za miaka mingi za kutaka kuipiga marufuku bila mafanikio.
Yeyote anayepatikana akitengeneza, kuuza au kutumia mifuko hiyo ya plastiki anaweza kupigwa faini ya hadi dola 40,000 au kufungwa jela hadi miaka minne.
Mahakama Kuu iliamua kuwa maslahi ya mazingira yanazidi maslahi ya kibiashara
Serikali imesema marufuku hiyo itasaidia kulinda mazingira.
Lakini watengenezaji wa bidhaa wamesema marufuku hiyo itasababisha kupotea kwa nafasi 80,000 za kazi.
Wakenya hutumia takriban mifuko 24 milioni ya plastiki kila mwezi, kwa mujibu wa takwimu za serikali.
Nchi nyingine kadha za Afrika zimepiga marufuku mifuko hiyo zikiwemo Afrika Kusini, Rwanda na Eritrea.
Tanzania pia imekuwa ikifanya juhudi kupiga marufuku mifuko hiyo ingawa hatua hiyo imekuwa ikiahirishwa.
Hili ni jaribio la tatu la kupiga marufuku mifuko hiyo nchini Kenya katika kipindi cha miaka kumi.
Ingawa wengi Nairobi wamekuwa wakiunga mkono marufuku hiyo, kuna shaka kuhusu jinsi Wakenya watazoea maisha bila mifuko hiyo ambayo hutolewa bila malipo madukani wateja wanaponunua bidhaa.
Serikali imekuwa ikihimiza wateja kuanza kutumia mifuko mbadala ambayo haijaundwa kwa kutumia plastiki.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Taifa ya Mazingira Kenya, wasafiri wanaopakiwa bidhaa walizonunua katika maduka yasiyotozwa kodi watalazimika kuiacha mifuko hiyo ya plastiki uwanja wa ndege kabla ya kuruhusiwa kuingia.
Serikali ilikuwa imetoa muda wa miezi sita kwa wadau kujiandaa kabla ya kuanza kutekelezwa kwa marufuku hiyo.
Watengenezaji bidhaa wanaotumia mifuko ya plastiki kupakia bidhaa viwandani hata hivyo hawajaathiriwa na marufuku hiyo.
CHANZO: BBC
SHARE









No comments:
Post a Comment