Na Agness Moshi – MAELEZO
Ni jambo la kawaida katika miaka
hii kuona takwimu za tafiti mbalimbali zikitolewa na Taasisi , Serikali ,
Mashirika au baadhi ya watu kwenye vyombo vya habari au mitandao ya
kijamii ambayo kwa sasa imejizolea umarafu kutokana ongezeko la
watumiaji wake Nchini.
Takwimu hizo zimekua zikitolewa
kwa lengo la kutoa taarifa, kuelimisha au kusaidia katika kupanga
mipango mbalimbali kwa maendeleo ya Taasisi, Shirika husika au Nchi kwa
ujumla . Wakati mwingine zimekua zikiibua hisia za wananchi kutaka
kujua zaidi kuhusiana na taarifa hizo hivyo kupelekea vyombo vya habari
kufuatilia taarifa hizo kwa undani.
Si jambo la ajabu kuona taarifa
za takwimu kwenye magazeti, televisheni, mitandao ya kijamii au
kuzisikia kwenye redio. Mtakua mashahidi wangu kwenye hili. Lakini je,
takwimu hizi tunazozisikia na kuziona zinafuata Sheria na taratibu za
utoji takwimu?
Ni wazi kila kitu kina utaratibu
na sheria zake, vivyo hivyo utoaji takwimu una sheria na taratibu zake
kuanzia ukusanyaji data hadi uwasilishwaji wake kwa jamii au taasisi
husika.
Uwepo wa taratibu za utoaji
taarifa za takwimu umethibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa
Ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa alipokua akiongea na waadishi wa
Habari Jijini Dar es Salaam mapema wiki hii, kufuatia taarifa zisizo
sahihi zilizotolewa na Kampuni ya Utafiti ya Geopoll yenye Ofisi ya
Kanda Ya Afrika, mjini Nairobi, Kenya kuhusiana na viwango vya idadi ya
watazamaji wa vituo vya habari hapa nchini.
“Taarifa zozote zinazohusu
utafiti ni lazima zizingatie vigezo vyote vinavyotakiwa na
vilivyoidhinishwa na mamlaka inayotambulika kisheria”,alisema Dkt.Chuwa.
Alivitaja baadhi ya vigezo hivyo
ambavyo ni uwazi na ukweli, uhusishwaji wa wahusika na wadau mbalimbali ,
ushirikishwaji wa mamlaka husika na kuzingatiwa kwa weledi.
“Takwimu zinazotolewa bila
kuzingatia taratibu zinazohitajika hazitatambulika na Serikali kwani
utoaji wa Takwimu haufanywi kama unavyohesabu migomba shambani, ni
lazima wahusika wafuate taratibu zote”, alifafanua Dkt.Chuwa.
Dkt. Chuwa amesisitiza kuwa, ni
vyema Taasisi yoyote inayotaka kukusanya taarifa zozote za takwimu
kuhakikisha wanashirikisha wahusika ili kuepusha mkanganyiko na
upotoshwaji kama ilivyofanywa na Kampuni hiyo kutoka Nairobi, Kenya.
Aliendelea kwa kusema, Serikali
haitatambua Takwimu zitakazotolewa bila kufuta sheria ya takwimu na
kukidhi vigezo rasmi kwani zinaweza kuwa chanzo cha maafa.
“Takwimu si kitu cha masihara, takwimu ni vita” aliongeza Dkt.Chuwa.
Kufuatia kuathiriwa kwa mahusiano
ya kiutendaji baina ya vyombo vya habari hapa nchini yaliyosababishwa
na taarifa iliyotolewa na kampuni ya Geopoll hivi karibuni kupitia
mitandao ya kijamii.
Ofisi ya Takwimu nchini inapenda
kuzijulisha Taasisi zinazojihusisha na utoaji wa taarifa zinazotokana na
utafiti kuwa, Sheria ya takwimu ya mwaka 2015 kifungu cha 6 imeipa
NBS mamlaka ya kutoa, kusimamia na kuratibu upatikanaji wa takwimu
rasmi kwa ajili ya matumizi ya Serikali na Wadau wa Takwimu.
“Hapo awali Ofisi ya Taifa ya
Takwimu haikua na meno lakini mara baada ya marekebisho ya Sheria hiyo,
sasa inayo meno ya kuiwezesha kudhibiti utoaji holea wa Takwimu nchini”
Alisema Dkt. Chuwa.
Dkt.Chuwa ametoa rai kwa watoa
takwimu kufuta kanuni na taratibu kama watashindwa hawana budi kuacha
mara moja kwani shughuli ya utoaji takwimu si lelemama kama
inavyodhaniwa.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa
Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa amewataka Waandishi wa
Habari kuacha kuandika taarifa za takwimu ambazo
hazijahazijathibitishwa na kutambulika na NBS,pia zisizo na mashiko
kwa Wananchi na Serikali kwa ujumla.
“Vyombo vya habari nchini viache
kushabikia taarifa zinazotolewa na Taasisi zozote zisizo tambulika na
kuthibitishwa na NBS hususani katika maswala ya Takwimu”, alisisitiza
Bi. Zamaradi.
Wahenga walisema “Mchelea mwana
kulia hulia mwenyewe” wakimaanisha mzazi anapozembea kulea mtoto wake
baadae anapoharibikiwa inakua hasara kwake.Hivyo basi, NBS imefanya
jambo jema kukemea watoa takwimu wasiofuata sheria ili kuepusha madhara
yoyote yanayoweza kusababishwa na takwimu zisizo rasmi.
Kwa watumiaji wa mitandao ya
kijamii, ni vyema kutoamini na kujiepusha na usambazaji wa taarifa
ambazo hazina uhakika kwasababu wanaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa
Amani ambayo ndio msingi wa maendeleo ya nchi .
SHARE
No comments:
Post a Comment