RAIS wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliwahi kusema umaskini unatengenezwa na wa kuundoa ni wananchi wenyewe.
Kauli hiyo imerudiwa tena na viongozi mbalimbali, wakiwemo wa hapa kwetu kuonesha namna gani umaskini unasumbua vichwa vya watu wengi.
Swali ni je, tuanzie wapi? Tutegemee wanasiasa kuondoa umaskini au kila mtu kwa nafasi yake apambane kadiri inavyowezekana kuusambaratisha katika jamii yetu.
Ni lazima nikiri kuwa kwa nchi kama yetu ambayo inapambana kujitoa kwenye lindi la umaskini, njia pekee ya wananchi kuondokana na tatizo hilo ni kutumia vizuri kila fursa inayopatikana ili kujiletea maendeleo.
Kuwakodolea macho viongozi wetu ili kukabiliana na adui huyo ambaye Hayati Mwalimu Julius Nyerere alimtangaza mwaka 1967 ni kujidanganya. Hii ni kwa sababu fursa za kujiletea maendeleo zipo nyingi kinachohitajika ni watu kujituma na kuacha uvivu.
Zinapotokea fursa kama za kuandika michanganuo ya biashara hili lipo ndani ya uwezo wa mtu mmoja mmoja na si kusubiri wanasiasa wanasema nini. Pia, ili kupata mikopo ni lazima tuzichangamkie fursa zilizopo badala ya kukaa vijiweni tukilalamika.
Zikitokea fursa za kuandika insha ni lazima tufanye hivyo hima. Ndicho anachosisitiza Rais John Magufuli na kaulimbiu yake ya Hapa Kazi Tu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa maendeleo hayapatikani kwa kuchekeana.
Wala umaskini haondolewi kwa watu kulalamika na badala yake kujikita katika fursa za kuufuta. Yanapotokea mashindano ya kuandika mawazo mbalimbali ya biashara au ujasiriamali ni jambo jema kushiriki.
Wenzetu wa mataifa yaliyopiga hatua na hata hapa nchini kwetu wamefanya hivyo na kujiondoa kwenye umaskini wa kujitakia (adjacent poverty). Kwa hiyo vita ya kuondoa umaskini si ya lelemama. Si ya kusubiri viongozi wa kisiasa waseme hivi au vile.
Kusema kweli ili kupata maendeleo ya kweli ni lazima kuvuja jasho. Ni lazima kupinda mgongo na kusumbua ubongo. Ni lazima na ikibidi kufanya kazi za ziada. Ni lazima kuzitumia fursa zilizopo vizuri kwa ustawi wa maisha yetu.
Hata Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alipoahidi maisha bora kwa kila Mtanzania hakuwa na maana ya kuwapa watu fedha. Nchi inapoweka mazingira bora ya kazi, ikajenga barabara, watu wakapate elimu kinachobaki ni watu wenyewe kujituma.
Kwa maana kuwa afanye nini kutumia barabara zilizopo kujiletea maendeleo. Auuze mkaa au nyanya? Auuze samaki au mbao? Barabara hazipo kwa ajili ya kusafiri tu. Barabara ni chombo cha kukuza uchumi wa nchi na watu wake. Ni chombo cha maendeleo.
Kwa hiyo ndugu zangu mwenye mamlaka ya kuondoa umaskini ni sisi wenyewe baada ya Serikali kuweka mifumo mizuri ya kutuwezesha kufika huko. Naam. Kwa hiyo ninapozungumzia umaskini ni pamoja na kupanua wigo wa kufikiri na kuwa wabunifu.
Mfano, Kampuni ya Total Tanzania imezindua shindano la "Startupper of the year by total". Shindano hili limebuniwa na kundi la kampuni za total likishirikisha mataifa 34 ya Afrika, ikiwemo Tanzania.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Uhusiano wa Kampuni ya Total Tanzania, Marsha Msuya-Kilewo shindano lina lengo la kutambua, kuzawadia na kuwezesha utekelezaji wa miradi bora ya biashara ya ujasiriamali inayoanza au iliyobuniwa chini ya miaka miwili kwa ajili ya maendeleo ya jamii na taifa.
"Washindi wa miradi bora watapewa tuzo ya "Startupper of the year 2016 by Total" itakayoambatana na fedha taslimu itakayotumika kama mtaji wa kuendeleza, na kusimamia uendelezaji wa miradi hiyo," anasema Msuya.
Kwa mujibu wa Msuya shindano hilo ni bure kwa Watanzania wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 35 na kwamba fomu za kujiunga zinapatikana startupper.total.com na shindano litakuwa wazi hadi Januari 31, mwakani.
Anasema shindano hilo ni juhudi za kampuni katika kuhamasisha maendeleo kiuchumi na kijamii ili kusaidia nchi zote duniani ambako kampuni hiyo ipo. Anasema shindano hilo ni hatua madhubuti kuvumbua uvumbuzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Miradi ya kuangia uanzishwaji wa viwando vidogo vitakavyotoa ajira na kuchangia maendeleo ya jamii na Afrika kwa ujumla. Shindano linalenga kuibua miradi mipya iliyotokana na wananchi wenyewe ambayo inaendana na malengo ya kampuni," anasema.
Kama hiyo haitoshi, anasema kampuni hiyo imeanzisha miradi kabambe ya utafutaji wa mafuta na gesi ili kupata nishati endelevu kwa ajili ya Afrika ya sasa na baadaye. Pia, kuendeleza vijana ili wawe msaada mkubwa kwa bara hilo siku za usoni.
"Jopo la majaji linalohusisha wataalamu wa biashara litachagua miradi kumi bora nchini itakayoingia fainali kwa kuzingatia vigezo vya ubunifu, uhalisia na uwezo wa mradi katika kuleta maendeleo na kuboresha hali ya maisha ya Watanzania," anasema.
Kwa hatua hiyo ninaamini kila mwananchi akitumia nafasi zinazojitokeza kwa kutumia ubunifu na uwezo wake bila shaka vita ya kukabiliana na umaskini itakuwa rahisi. Muhimu hapa ni kufahamu kuwa umaskini hautaondoka kwa maneno bali kwa vitendo.
SHARE
No comments:
Post a Comment