Sisi
Mtandao wa Wanawake wa Katiba na Uchaguzi kwa uratibu wa TGNP Mtandao,
tunampongeza Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa juhudi zake anazozionesha katika kudhibiti matumizi
mabaya ya rasilimali za umma ikiwa ni pamoja na kupunguza ukubwa wa
serikali na kusimamia kikamilifu utendaji kazi katika ofisi za umma ili
kuongeza ufanisi ikiwamo kuokoa upotevu na ubadhirifu wa pesa za walipa
kodi.
Pamoja na kumpongeza Mhe. Rais kwa
jitihada za serikali yake za kurejesha utawala bora na serikali yenye
safu za viongozi waadilifu, tumeanza kuwa wasiwasi kuhusu dhamira ya
kutambua nguvu kubwa za wanawake katika kuwezesha jitihada za awamu hii
hasa katika kuleta mabadiliko katika maisha ya Watanzania, wanawake kwa
wanaume.
Mtandao wa Wanawake wa Katiba na
Uchaguzi tumekuwa tukifuatilia kwa karibu Uchaguzi na Uteuzi wa viongozi
katika nafasi mbalimabli za kimaamuzi serikalini. Hii ni pamoja na
uteuzi wa Makatibu Wakuu, Mawaziri na Wakuu wa Idara/Taasisi mbalimbali
uliofanywa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika uteuzi huo jumla ya makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu
walioteuliwa ni 50 idadi ambayo ni pungufu kidogo ikilinganishwa na
mwaka 2014 ambako jumla yao ilikuwa 53; ambapo idadi ya Makatibu Wakuu
imeongezeka kutoka 23 mwaka 2014 hadi 29 wakati Manaibu Katibu Wakuu
imepungua kutoka 30 mwaka 2014 hadi 21 mwaka huu. Kati ya nafasi zote 50
za walioteuliwa na Mhe. Rais, wanawake ni 10 pekee ambayo ni sawa na
asilimia 20.
Tathmini yetu ya jumla ni kuwa,
ikilinganishwa na awamu iliyopita, idadi ya Makatibu wakuu na Manaibu
Katibu Wakuu wanawake imepungua kwa kiasi kikubwa. Takwimu za mwaka 2014
zinaonesha kuwa, idadi ya wanawake waliokuwa Makatibu wakuu au Manaibu
Katibu Wakuu ilikuwa 20 sawa na asilimia 37.7 huku wanaume wakiwa 33
sawa na asilimia 62.3. Katika uteuzi uliofanyika mwaka huu, jumla ya
wanawake Makatibu Wakuu na Manaibu ni 10 sawa na asililimia 20 tu huku
asilimia 80 inayobakia ikishikiliwa na wanaume. Kwa kuzingatia takwimu
hizo, ni dhahiri kuwa, idadi ya Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu
wanawake imepungua kutoka asilimilia 37.7 mwaka 2014 hadi asilimia 20
mwaka 2015. Hii ni tofauti ya asilimia 17.7 ambayo ni kubwa sana na
hivyo kuongeza pengo la jinsia katika nafasi za kufanya maamuzi.
Kwa kuangalia nafasi hizo mbili,
utagundua kuwa, kwa upande wa Makatibu Wakuu, kati ya 29 walioteuliwa,
wanaume ni 26 sawa na asilimia 89.7% huku wanawake wakipungua kutoka 5
(asilimia 21.7) mwaka 2014 hadi 3 (asilimia 10.3) kwa sasa hivyo
wanawake katika nafasi hizo wamepungua kwa asilimia 10. Kwa upande wa
Manaibu Katibu Wakuu, idadi ya wanawake imepungua kwa kiasi kikubwa pia.
Kati ya Manaibu Katibu Wakuu 21 walioteuliwa wanawake ni 7 tu sawa na
asilimia 33.3 ikilinganishwa na asilimia 50 mwaka 2014.
Sisi wanaharakati wa masuala ya
jinsia tumeshtushwa na uteuzi huo kwani tulitarajia kuwa kwa kuzingatia
usawa wa kijinsia uliofanyika katika nafasi za juu za Serilikali (Rais
na Makamu wake) teuzi za nafasi za uongozi zingezingatia usawa wa
kijinsia kama suala la msingi hasa katika kuhakikisha kuwa wanawake na
makundi mengine wanashiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi.
Tanzania kupitia (Tanzania Development Vision 2025) ukurasa wa 16) imetambua kuwa mojawapo ya vichocheo vya ukuaji wa uchumi ni pamoja na jamii yenye muono wa kimaendelea ambapo pamoja na mengine unakuwa na tamaduni wezeshi hususani kwa wanawake na makundi mengine. Sambamba na hilo Mpango wa Miaka mitano wa Maendeleo wa nchi yetu (Tanzania FYDP 2011/12 hadi 2015/16- 2.3.5) unatambua kutokuwepo kwa usawa wa jinsia ni moja ya vikwazo vya maendeleo ya kiuchumi, siasa na kijamii licha ya kwamba wanawake wanaunda zaidi ya asilimia 50 ya idadi yote ya watu nchini. Vile vile MKUKUTA II kupitia kipengele cha 2 imeweka lengo la kuhakikisha haki za binadamu na za makundi maalum kama wanawake, wanaume masikini na watoto zinaendelezwa na zinalindwa. Hii inahusisha haki ya kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Tanzania kupitia (Tanzania Development Vision 2025) ukurasa wa 16) imetambua kuwa mojawapo ya vichocheo vya ukuaji wa uchumi ni pamoja na jamii yenye muono wa kimaendelea ambapo pamoja na mengine unakuwa na tamaduni wezeshi hususani kwa wanawake na makundi mengine. Sambamba na hilo Mpango wa Miaka mitano wa Maendeleo wa nchi yetu (Tanzania FYDP 2011/12 hadi 2015/16- 2.3.5) unatambua kutokuwepo kwa usawa wa jinsia ni moja ya vikwazo vya maendeleo ya kiuchumi, siasa na kijamii licha ya kwamba wanawake wanaunda zaidi ya asilimia 50 ya idadi yote ya watu nchini. Vile vile MKUKUTA II kupitia kipengele cha 2 imeweka lengo la kuhakikisha haki za binadamu na za makundi maalum kama wanawake, wanaume masikini na watoto zinaendelezwa na zinalindwa. Hii inahusisha haki ya kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka
2015-2020, ambayo serikali iliyoko madarakani inaitekeleza katika aya ya
167 (a), kuhusu wanawake, kimeweka lengo la kuendelea kuweka utaratibu
wa kikatiba na kisheria utakaowawezesha wanawake kushika nafasi sawa
(50/50) za uongozi katika vyombo vya maamuzi katika ngazi zote.
Tunasisitiza kueheshimiwa na kutekelezwa kwa vitendo kwa malengo hayo
ili wanawake wapate fursa sawa za kutoa maamuzi juu ya masuala muhimu ya
taifa letu. Tunaitaka serikali kutekeleza ahadi zake za kuzingatia
usawa wa Kijinsia kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya chama chake.
Tunatoa rai kwa Mhe. Rais na
viongozi wote kusimamia kikamilifu utekelezwaji wa mikataba mbalimbali
iliyosainiwa na Tanzania hususani ile inayohusu usawa wa kijinsia ili
kupunguza pengo lililopo kuelekea usawa wa 50/50 katika nafasi za
uongozi. Mikataba hiyo ni pamoja na Mpango Kazi wa Beiging (1995),
Mkataba wa Maputo, Mkataba wa Nyongeza wa Jinsia na Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC Gender Protocol) na Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za
Binaadamu (1948). Mikataba hii mingi husisitiza mataifa husika
kuhakikisha uwepo wa asilimia 50 (au 30 kama kiwango cha chini) kwa
wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi.
Ni matarajio yetu kuwa nafasi za
uteuzi zilizobaki zitafanyika kwa kuzingatia hayo. Nafasi hizo ni pamoja
na uteuzi wa Wabunge (ambao walishaanza kuteuliwa), Mabalozi, Wakuu wa
Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wakuu
wa taasisi na mashirika ya umma kadhalika uteuzi wa wajumbe wa Bodi na
Tume mbalimbali katika mashirika na taasisi hizo. Ni muhimu teuzi zote
katika mihimili mikuu mitatu ya Bunge, Mahakama na Serikali zizingatie
usawa wa jinsia.
Mwisho kama Mtandao wa Mashirika
yanayotetea haki za wanawake tutazidi kuendelea kufuatilia, kukumbusha
na kushirikiana na serikali ya awamu ya tano katika kuleta maendeleo ya
Taifa letu yanayozingatia haki za binadamu na usawa wa jinsia.
Imetolewa na:
Lilian Liundi
Lilian Liundi
Mkurugenzi Mtendaji
TGNP Mtandao
Kny: Mtandao wa Wanawake wa Katiba na Uchaguzi.
Januari 5, 2016
SHARE
No comments:
Post a Comment