

Picha na Ally Daud- Maelezo
……………………………………………………………….
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
SERIKALI za Tanzania na Uganda
zinatarajia kuanzisha mradi wa uwekezaji wa ujenzi wa mradi wa bomba la
mafuta unaolenga kuongeza pato la taifa na uchumi wa nchi hizo.
Mradi huo unatarajia kugharimu kiasi cha Dola za Marekani bilioni nne na utekelezaji wake utaanza mwanzoni mwa mwaka 2017.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu
(Machi 28, 2016) Jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa alipokuwa na akiongea na
waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wake na
wafanyabiashara wa sekta ya mafuta nchini.
Prof. Ntalikwa amezitaja fursa
ambazo zitanufaisha taifa kuwa ni pamoja na kodi zitakazolipwa,
kuongezeka kwa wigo wa ajira kupitia miradi huo pamoja na tenda
mbalimbali zitakazotolewa wakati na baada ya kukamilika kwa ujenzi wa
mradi huo.
“Tanzania ina kila sababu ya
kupata mradi huo kwa kuwa ina uzoefu wa kuwa na mabomba kama hayo manne
nchini na tunajivunia bandari yetu ya Tanga yenye kina kirefu kuliko
bandari zote Afrika Mashariki” alisema Prof. Ntalikwa.
Prof. Ntalikwa amesema kuwa
mwitikio wa wafanyabishara wa sekta ya mafuta nchini ni mzuri na
kubainisha kuwa wanatarajia kusafiri kuelekea nchini Uganda kujionea
fursa mbalimbali zinazopatikana nchini humo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
wafanyabiashara wa sekta ya mafuta nchini Dkt. Gideon Kaunda amesema kwa
upande wao wataitumia vyema fursa ya uwekezaji katika ujenzi wa mradi
huo na kuendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt.
John Pombe Magufuli.
SHARE
No comments:
Post a Comment