Mkulima
wa vitalu vya karafuu wa Kitope Mzee Sheha Khamis akimuelezea Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la ZSTC changamoto anazokabiliana nazo katika
kutekeleza kazi hiyo wakati Mkurugenzi huyo alipofanya ziara katika Mkoa
Kaskazini Unguja na Wilaya Kati.
Mfanyakazi
wa kitalu cha Mikarafuu cha Donge Bi Fatma akitayarisha udongo kwa
ajili ya kuatika miche katika shamba hilo linalomilikiwa na Wizara ya
Kilimo na Mali Asili.
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Shirika
la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) kwa kushirikiana na Wizara ya
Kilimo na Mali Asili linakusudia kuongeza mashirikiano na kuwasaidia
wananchi wanaoanzisha vitalu vya mikarafuu Unguja na Pemba.
Mkurugenzi
Mwendeshaji wa ZSTC Bibi Mwanahija Almasi ametoa ahadi hiyo baada ya
ziara yake ya siku mbili kutembelea vitalu vya mikarafuu vya Serikali na
vya watu binafsi katika vijiji vya Kitope, Kidimni, Machui Selem na
Donge kuona matatizo yanayowakabili katika kutekeleza kazi zao.
Amesema
vitalu vya watu binafsi vinamchango mkubwa katika kuimarisha zao la
karafu Zanzibar kwa kuziba pengo linalojitokeza wakati wa ugawaji wa
miche ya mikarafuu kwa wakulima kutoka vitalu vya Serikali
Amesisitiza
kuwa kutoakana umuhimu huo na kazi kubwa wanayochukua wakulima hao
huku wakikabiliwa na upungufu wa nyenzo muhimu, Shirika litatoa
pembejeo zitakazosaidia kufanikisha kazi zao kwa ufanisi.
Wakati wa
ziara hiyo wakulima wanaomiliki vitalu vya mikarafuu walimueleza
Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC kwamba wanakabiliwa na tatizo la vifuko
vya kuatikia miche (policing), mabero, pauro na maji hasa wakati wa
kiangazi.
Mkurugenzi
Mwendeshaji amewataka wakulima hao kutovunjika moyo na changamoto
wanazokabiliana nazo na waendelee kushirikiana na maafisa wa Kilimo
wakati Shirika linafanya juhudi za kupunguza changamoto zao.
Hata
hivyo Bi Mwanahija amewashauri wenye vitalu vya mikarafuu baada ya
kupata msaada kutoka ZSTC kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya
kuuzia miche ya mikarafuu kwa wakulima ambapo hivi sasa wanauza
shilingi 1000 kwa mche mmoja.
Amesema
Serikali itaendelea kutoa miche ya mikarafuu bure kwa wakulima lakini
vitalu vya Serikali viliopo hivi sasa haviwezi kukidhi mahitaji ya
wakulima wote wa zao hilo, hivyo vitalu vya watu binafsi vitaendelea
kuwa tegemeo kwa wakulima
“Wakulima
wa vitalu vya Mikarafuu mumekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza
na kuimarisha zao la karafuu Zanzibar lakini wapunguzieni wakulima
bei ya miche ingawa gharama mnazotumia ni kubwa,” Bi Mwanahija
aliwashauri.
Bibi
Mwanahija amewaelekeza maafisa Kilimo kuwapa wakulima miche ya
mikarafuu wanayoweza kuihudumia kwani uzoefu unaonyesha wakulima
huchukua miche mingi wasiyoweza kuitunza na hatimae inakufa mara tu
baada ya kumaliza mvua za masika.
Mkuu wa
Vitalu kutoka Wizara ya Kilimo Rashid Nassor Rashid alimueleza
Mkurugenzi Muendeshaji wa ZSTC kwamba vitalu vya Serikali
vinakabiliwa na upungufu mkubwa wa wafanyakazi baada ya wengine
kustaafu na baadhi yao kuzeeka hivyo wanampango wa kuajiri
wafanyakazi wa muda kwa kazi za dharura kuziba pengo liliopo.
Amesema
kazi ya kutafuta mbegu (matende) kwa ajili ya vitalu vya mikarafuu
zinachukua muda mfupi kabla ya mvua za masika kuanza na ikiwa kazi
hiyo haitofanywa kipindi cha sasa kazi hiyo itashindwa kutekelezwa.
Mkuu wa
usimamizi wa zao la Karafuu kutoka Wizara ya Kilimo na Mali Asili Badru
Kombo Mwemvura amemuhakikishia Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC kwamba
iwapo wakulima watafuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo lengo la
Serikali la kuongeza uzalishaji wa Karafuu litafika muda mfupi ujao.
Amesema
tatizo la wakulima wa zao la karafu ni kuchukua miche mingi bila ya kuwa
na uwezo wa kuihudumia na baadhi yao huchelewa kuipanda baada ya
kuchukua hatimae hufa huku wengine wakikosa kabisa.
Ameongeza
kuwa mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa yakiathiri sana nchi za
visiwa nayo imekuwa changamoto kubwa kwa kilimo cha zao la Karafuu na
mazao mengine Zanzibar.
Wizara ya
Kilimo ilipanga kutoa miche ya Mikarafuu milioni moja kwa wakulima wa
zao hilo Unguja na Pemba, kuanzia mwezi wa April, lakini kutokana na
ukosefu wa mbegu ulijiotokeza mwaka jana kiwango hicho huenda
kikapungua . (P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment