Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Seleman Jafo
akitoa maelekezo baada ya kukagua mradi wa maji wa Wilunze Wilaya ya
Chamwino.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Seleman Jafo
akimsikiliza Mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa maji Wilunze Enock
Masanja.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Seleman Jafo
akikagua mradi wa maji Wilunze wilaya ya Chamwino.
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Seleman Jafo amefanya ziara ya
kutembelea mradi wa maji katika kijiji cha Wilunze wilaya ya Chamwino
na kutoa mwezi mmoja kwa Mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo kukamilisha
kutokana na utekelezaji wake kuwa wa muda mrefu.
Jafo alitoa agizo hilo jana alipokuwa akikagua mradi huo ambao ujenzi wake umeanza mwaka 2013.
Akizungumza katika ukaguzi huo,
Jafo alisema utekelezaji wake umesuasua hali inayosababisha wananchi wa
eneo hilo waendelee kupata adha ya maji na kuiagiza Halmashauri ya
Chamwino kuzuia fedha ya mkandarasi huyo zilizosalia kwa kipindi cha
miezi mitatu mpaka ubora wa mradi huo utakapoonekana.
Hata hivyo alisema mkandarasi
aitwaye M/S Kijima fedha aliyopewa hadi sasa haiendani na kazi
iliyofanyika huku akitilia mashaka mabomba yaliyowekwa kwamba yapo chini
ya kiwango.
“Mkandarasi umepewa Sh. Milioni
305.7, gharama ya mradi kwa ujumla ni Sh.Milioni 347.9, umebakisha fedha
kidogo ambayo ni Sh.milioni 42.1 tukiangalia kazi iliyofanyika hata
haiendani na fedha ulizopewa, unachokifanya hapa ni kama maigizo huu
mradi haujafikia asilimia 90 na haya mabomba yanaonekana yapo chini ya
kiwango maana yameanza kupasuka,”alisema Jafo
Aidha alisema Halmashauri hiyo
imekuwa na uzembe katika usimamizi wa miradi ya maji hali inayosababisha
wananchi kukosa huduma ya maji kwa wakati.
Jafo alimtaka Mkandarasi huyo
kukamilisha mradi huo na kwamba ifikapo Aprili 3, mwaka huu atarudi
kukagua na kuiagiza serikali ya wilaya hiyo kuwakamata watu
watakaoharibu miundombinu ya maji.
Hata hivyo alisema katika miradi
mingi ya maji aliyotembelea amekutana na changamoto ya wakandarasi
kuweka mabomba ambayo yapo chini ya kiwango na kusababisha wananchi
wanapokabidhiwa mradi kushindwa kuiendesha.
Naye, Mmoja wa wakazi wa kijiji
hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Camp A, Waziri Sengoli,
alisema wananchi wa kijiji hicho wamekuwa wakipata adha ya maji ka
takriban miaka saba huku akiwaumbua viongozi wa Halmashauri hiyo kwamba
wamekuwa hawatembelei kukagua mradi huo.
Kwa upande wake, Mkandarasi huyo
Enock Masanja, alijitetea kuwa ameshindwa kukamilisha mradi kwa wakati
kutokana na kutopata fedha kwa wakati.
SHARE
No comments:
Post a Comment