RAIS Dk. John Magufuli ametengua
uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Shirika Elimu Kibaha Dkt. Cypirian
Mpemba ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za kiutendaji
zinazomkabili.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo mjini Dodoma,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa(Tamisemi), George Simbachawene amesema kufuatia tuhuma
mbalimbali za uendeshaji, zinazolikabili Shirika hilo ambazo zimekuwa
zikiandikwa kwenye vyombo vya habari kwa muda mrefu sasa.
Simbachawene amesema Mnamo Machi, 4
mwaka huu Rais Magufuli ametengua rasmi nafasi ya Mtendaji huyo ili
kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.
Amefafanua kuwa kumekuwepo
malalamiko dhidi ya Mtendaji Mkuu wa wa shirika la Elimu Kibaha ambapo
Ofisi ya Rais TAMISEMI iliunda kikosi kazi ili kufanya uchunguzi
dhidi ya malalamiko hayo na kugundua kuwepo kwa changamoto katika
uendeshaji wa Shirika hilo.
“Ni kweli tuhuma juu ya
uendeshaji wa Shirika la Elimu Kibaha likiwemo suala la Mikataba
iliyoingiwa na Shirika hilo zimekuwepo kwa muda mrefu sasa. Sisi kama
Wizara hatukutaka kukurupuka kufanya maamuzi na tukaamua kuunda kikosi
kazi ili kufanya uchunguzi na matokeo ya uchunguzi huo yanapelekea
kuwepo kwa hoja zinazohitaji uchunguzi zaidi,” ameeleza Waziri
Simbachawene
Ameongeza kuwa ili uchunguzi huo
uweze kufanyika kwa uhuru Mhe. Rais ameamua kumsimamisha kazi Mtendaji
Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha ili kupisha uchunguzi wa kina dhidi
yake.
Waziri amesema uamuzi wa
kumsimamisha umechukuliwa kwa kuwa tuhuma na malalamiko mengi ya awali
yaliyojitokeza dhidi yake yanajenga hoja ya kuhitajika kufanyika kwa
uchunguzi zaidi ambapo kwa sasa nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Shirika la
Elimu Kibaha inakaimiwa hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.
SHARE
No comments:
Post a Comment