NA LILIAN
LUNDO – MAELEZO
Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikalipicani juu) wametoa
misaada ya vifaa vya kufundishia, kujifunzia pamoja na vyakula yenye thamani ya shilingi milioni 12 kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Buigiri
Wasioona iliyopo wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Akikabidhi
vifaa na vyakula hivyo kwa wanafunzi hao kwa niaba ya Mkurugenzi Idara ya
Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara
hiyo, Zamaradi Kawawa alisema kuwa wamewiwa kutoa misaada kwa wanafunzi hao ili
waweze kujifunza vema na kufikia malengo yao.
“Kila
mwaka tunapokutana katika mkutano wa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini
huwa tunatembelea watu wenye mahitaji mbalimbali na kutoa misaada. Kwa mwaka
huu tumefanya mkutano wetu hapa Dodoma, hivyo tumeona misaada yetu tuilete
Shule ya Msingi Buigiri Wasioona,” alifafanua Zamaradi Kawawa.
Akifafanua
zawadi zilizotolewa Zamaradi alisema kuwa Chama cha Maafisa Mawasiliano
Serikalini (TAGCO) kwa kushirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo wametoa msaada wa mashine Nne za nukta nundu (Perkins Brailler
Machine), Rimu 40 za karatasi za kuchapa nukta nundu (Brailler Paper), Mchele,
Maharage, Sukari, Unga na Juice.
Kwa
upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Samwel Jonathan amewashukuru Maafisa
Habari hao kwa msaada waliotoa na kusema utatua kwa kiasi kikubwa changamoto za
ukosefu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia shuleni hapo.
Mwalimu
Samwel Jonathan amesema, licha ya shule hiyo kuwa na changamoto mbalimbali
zikiwemo ukosefu wa mashine za nukta nundu, viti, meza pamoja na uchakavu wa madarasa
na majengo lakini shule hiyo imekuwa ikifaulisha wanafunzi wake kwa asilimia
100 katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kwa zaidi ya miaka kumi sasa.
Vilevile amesema shule hiyo inapokea fedha toka
Serikalini ikiwa ni utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo ambayo
hutumika kununua chakula na uendeshaji wa kila mwezi shuleni hapo. Ambapo kwa
mwaka wa fedha 2016/17 shule hiyo imepokea shiligi 150,000,000 kwa ajili ya
maendeleo ya shule.
Akitoa shukrani ya misaada waliopokea shuleni hapo mwanafunzi
Joseph Richard amesema elimu ndio msingi wa maisha hivyo na wao
wanahitaji elimu kama ambavyo watoto wasio na ulemvu wanavyohitaji. Aidha,
alishukuru kwa misaada iliyotolewa na kuwaombea baraka wote waliofanikisha
kupatikana kwa misaada hiyo.
Shule ya Msingi Buigiri Wasioona ni miogoni mwa shule
Kongwe nchini, ambayo ilianzishwa Aprili 30, 1950 na Mzungu aliyeitwa Captain
Fred Valley ambapo ilikuwa ikiongozwa na kumilikiwa na kanisa la
Anglikani ikiwa na lengo la kuwawezesha watu wazima wasioona wajue kusoma neno
la Mungu.
Baada ya nchi kupata uhuru mwaka 1961 Serikali iliamua
kushirikiana na kanisa katika kuendesha shule hiyo, ambapo mpaka sasa shule
hiyo inahudumiwa na Serikali na Kanisa.
Shule
hiyo ni ya bweni na kutwa ambapo ina jumla ya wanafunzi 115, wavulana 70
na wasichana 45 wakiwa wamechanganywa na wanafunzi wasio walemavu ambao
hawazidi wanafunzi 31 ili wanafunzi wenye ulemavu wasijione kuwa wanatengwa.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Bibi
Zamaradi Kawawa akikabidhi moja ya mashine za nukta nundu kwa mwanafunzi wa
Shule ya Msingi Buigiri iliyopo Mjini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Bibi
Zamaradi Kawawa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Buigiri iliyopo
Mkoani Dodoma wakati Maafisa Mawasilaino serikalini walipoenda kutoa msaada
Shuleni hapo wenye thamani ya Sh Mil 12 zikiwemo mashine za nukta nundu na
karatasi maalum.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Mawasiliano
Serikalini (TAGCO) Bibi Sylivia Lupembe akitoa neno kwa niaba ya wanachama wa
TAGCO kabala ya kukabidhi msaada Shuleni hapo wenye thamani ya Sh Mil 12
zikiwemo mashine za nukta nundu na karatasi maalum.
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Buigiri Samwel Jonathan
akisoma risala kwa wageni Maafisa Mawasiliano kabla ya kupokea msaada kutoka
Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) wenye thamani ya Sh Mil 12
zikiwemo mashine za nukta nundu na karatasi maalum.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Buigiri
wakiimba wimbo maalum wa kuwakaribisha wageni kutoka Chama cha Maafisa Mawasiliano
Serikalini (TAGCO) walipowatembelea na kuwapa msaada wenye thamani ya Sh
Milioni 12 zikiwemo mashine za nukta nundu na karatasi maalum.
Mmoja ya Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Buigiri Joseph
Richard akitoa neno la shukrani kwa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini
(TAGCO) mara baada ya kupata msaada wenye thamani ya Sh Milioni 12 zikiwemo
mashine za nukta nundu na karatasi maalum.
SHARE
No comments:
Post a Comment