Serikali ya Uturuki imeitaka serikali ya Uholanzi iombe radhi na
kutishia wakati huo huo kulipiza kisasi , baada ya kufukuzwa waziri wa
familia Fatma Betul Sayan Kaya , kisa kilichosababisha maandamano na
watu kadhaa kukamatwa mjini Rotterdam. Akizungumza baada ya kuwasili
katika uwanja wa ndege wa Ataturk , waziri Sayan Kaya ameituhumu
serikali ya Uholanzi kuzuwia uhuru wa mtu kwenda akutakako, uhuru wa mtu
kutoa maoni yake na aina zote nyengine za uhuru. Waziri Sayan alipanga
kwenda Rotterdam, kufanya kampeni kuunga mkono kura ya mageuzi ya katiba
yatakayompatia madaraka makubwa zaidi rais Recep Tayyip Erdogan. Kabla
ya hapo waziri wa mambo ya nchi za nje Mevlut Cavusoglo alikataliwa
ruhusa ya kutuwa nchini Uholanzi. Akiwa ziarani Metz nchini Ufaransa
waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki ameitaja Uholanzi kuwa ni
kitovu cha ufashisti. Mevlut Cavusoglo ameahidi hatua kali za kulipiza
kisasi zitachukuliwa na serikali yake. Danemark imeshauri ziara ya
waziri mkuu wa Uturuki nchini humo iakhirishwe kutokana na mvutano kati
ya Uturuki na Uholanzi. Na Ufaransa imezitolea wito Uturuki na nchi za
umoja wa Ulaya zipunguze mivutano.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment