Mkuu wa majeshi ya Uturuki anakutana na wenzake wa Marekani na Urusi
katika mkoa wa kusini mwa Uturuki wa Antalya ili kujadili kuhusu usalama
wa kikanda, hasa nchini Syria na Iraq. Hakuna maelezo zaidi
yaliyotolewa kuhusu mkutano huo unaoandaliwa na Jenerali Hulusi Akar.
Mwezi Agosti, wanajeshi wanaoongozwa na Uturuki walianzisha operesheni
ya kulifurusha kundi linalojiita Dola la Kiislamu kutoka mpaka wa
Uturuki na Syria na kuwazuia wapiganaji wa Kikurdi wa YPG kulikamata
eneo hilo. Tangu walipowaondoa wapiganaji hao katika ngome yao ya
al-Bab, mapigano yamelenga vijiji vya magharibi mwa Manbij,
yakiwakutanisha waasi wanaoungwa mkono na Uturuki na Baraza la Kijeshi
la Manbij, ambalo ni sehemu ya wanajeshi wanaoungwa mkono na Marekani wa
Syrian Democratic Forces - SDF na ambao wanajumuisha kundi la YPG.
Uturuki inaliona kundi la YPG kuwa sehemu ya chama cha wafanyakazi wa
Kikurdi - PKK ambacho kinaendesha uasi nchini Uturuki
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment