Julian Msacky
AKIZUNGUMZA na viongozi wa Kanisa la Mary-Knoll nchini
Marekani mwaka 1970, Mwalimu Julius Nyerere alitoa hotuba yenye msisimko.
Aliwaambia kuwa tatizo la dunia ya leo si umaskini bali
mgawanyo mbaya (usio na haki) wa rasilimali za nchi.
Wakiwa wamemkazia macho, Nyerere aliendelea kusisitiza kuwa
hali hiyo imesababisha matabaka kati ya walio nacho na wasio nacho.
Mwalimu alikuwa sahihi. Leo hii mgawanyo mbaya wa rasilimali
za nchi umesababisha wenye fedha waendelee kuwa matajiri na maskini waendelee
kuzama kwenye umaskini.
Hii ni kwa sababu ya mgawanyo mbaya wa rasilimali za nchi
kutumiwa na kikundi kidogo cha watu wenye meno makali kama msumeno kwa ajili ya
maslahi yao na familia zao.
Angalia namna ambavyo Afrika ni tajiri wa rasilimali lakini
watu wake wanaendelea kunuka umaskini kana kwamba nchi zao hazina kitu.
Wakati watu wao wakitaabika kwa umaskini, wao wanazidi kuishi
maisha ya anasa wakijenga majumba ya kifahari.
Mgawanyo huu mbaya umesababisha tajiri na maskini waonekana
maadui kwa sababu upande mmoja unaishi kwa jasho la wengine.
Katika mazingira ya aina hii ni vigumu kusema haki
inazingatiwa. Ni vigumu wananchi kufurahia maisha yao kwa sababu wengi
wamepigika.
Ili jamii iendelee kuishi kwa amani na upendo ni lazima
viongozi wetu wahakikishe kuna mgawanyo mzuri wa rasilimali za nchi.
Kwa kufanya hivyo tutaepuka migogoro mingi ambayo
imesababisha Afrika iendelee kugubikwa na mizozo isiyoishi kwa watu kukosa
haki.
Ni ukweli usiopingika kuwa vikundi vya kihalifu (kigaidi)
vinaibuka kwa sababu ya mgawanyo mbaya wa keki ya nchi. Nani anabisha?
Vijana wakiangalia namna watawala wanavyoishi kana kwamba
wapo peponi wanachukia.
Wakiangalia namna wasivyo na ajira, lakini kikundi kidogo
kinaishi kwa matanuzi lazima wanune.
Hadi hapo viongozi watakapozingatia mgawanyo mzuri wa
rasilimali za nchi kwa wananchi wao ndipo amani ya kweli itajengea.
Tofauti na hapo viongozi hawataongoza kwa amani. Wataona
uongozi ni mzigo kwa sababu ya kuwapo pengo kubwa kati ya maskini na matajiri.
Ni muda muafaka sasa kwa viongozi wetu kuangalia namna ya
kuondoa tofauti za vipato zilizopo kati ya mtu na mtu ili kila mmoja aweze
kunufaika na utajiri uliopo katika nchi husika.
Kama Afrika imezungukwa na utajiri wa kila aina ni lazima
tujiulize ni kwa nini wananchi wanazidi kuishi maisha ya shida? Je, wanastahili
kuishi hivyo?
Ni kwa nini pale penye utajiri watu waishi maisha ya hohe
hahe, lakini nchi ambazo hazina utajiri wa aina hiyo raia wao waishe maisha
kama ya mfalme?
Inasikitisha kuona madini ya almasi, dhahabu, tanzanite na
mengine mengi ambayo yapo Afrika yameshindwa kutumiwa kuondoa watu wao katika
umaskini.
Wakati wananchi wakishindwa kabisa kunufaika na utajiri huo,
viongozi wao wanatajirika kwa pupa na kuzua maswali mengi kuliko majibu.
Wote ni mashahidi kwamba viongozi wetu wanapoingia madarakani
wanakuwa hawana hili wale lile, lakini ndani ya kipindi kifupi wanakuwa
matajiri ghafla. Wanaupata wapi?
Hali hiyo ndiyo iliyomshtua mwandishi Tonn Burgis katika
kitabu chake cha “The Looting Machine” akishangaa namna Afrika inapozidi
kufukarika wakati ina utajiri wa kila aina.
“Ni kwa nini bara hili ni maskini wakati limesheheni utajiri
wa kina aina,” anasema Burgis katika kitabu hicho cha mtambo wa uporaji.
Anachosema Burgis ni kwamba ni aibu Afrika kuwa maskini kwa
sababu ina kila kitu cha kuifanya iwe tajiri.
Swali ni je, viongozi wetu wanafahamu ni wapi tulipokwama?
Wanajua njia ya kutuondoa hapo wakati wamefunga fungate na mataifa ambayo yana
mitambo ya uporaji?
Nani wa kuwaokoa Waafrika wasiendee kuzama kwenye umaskini?
Ni kiongozi gani mwenye ujasiri wa kusimamia mgawanyo sawa wa utajiri uliopo
ili ulete neema kwa wote badala ya laana?
Kusema kweli wanahitajika viongozi wenye sauti na ujasiri wa
kusema imetosha kwa maana ya kutuondoa kwenye utumwa wa umaskini.
Tunataka tuone mgawanyo huo ukiwa sawa ili kwamba
tunapoaambiwa uchumi umekua uonekana kwa wananchi na si kwa maneno.
Tunapoambiwa tumedhibiti utoroshaji wa mali za nchi, faida
yake ionekana kwa wananchi.
Tunapoambiwa makusanyo ya kodi yameongezeka maradufu gharama
za maisha zipungue badala ya kuendelea kupaa.
Kinyume chake tunarudi kule kule alikosema Mwalimu Nyerere
kuwa tatizo la dunia ya sasa si umaskini bali mgawanyo mbaya wa utajiri wetu.
Ni kwa msingi huo dunia yetu imekuwa si mahali salama pa
kuishi kwa sababu haki za watu zinakandamizwa na kuporwa hata kile kidogo
walichonacho.
SHARE
No comments:
Post a Comment