Uturuki: Yumkini kura milioni 2.5 'zilichakachuliwa'
Waangalizi wa Baraza la Ulaya katika kura ya maoni
iliyopigwa Jumapili Uturuki wamesema yumkini kura zipatazo milioni 2.5
zilichakachuliwa. Matokeo ya mwisho yalimpa Rais Recep Tayyip Erdogan
ushindi wa asilimia 51.41.
Uwezekano kuwa kura zipatazo milioni 2.5 zilichakachuliwa katika kura ya maoni ya Uturuki umebainishwa leo na Alev Korun, mjumbe wa Austria katika ujumbe wa waangalizi wa Baraza la Ulaya. Korun amekiambia kituo cha Redio cha ORF kwamba kulingana na sheria ya Uturuki, kura zilizo katika bahasha rasmi za uchaguzi ndizo huhesabiwa, lakini ameendelea kusema afisa huyo, afisa wa ngazi ya juu serikali aliamua kinyume na sheria, kwamba hata kura ambazo hazikuwa katika bahasha hizo, pia zihesabiwe.
Mjumbe huyo wa Austria amesema uwezekano wa kuchezewa kura kiasi hicho ni suala lenye uzito mkubwa, ambalo lineweza kubadilisha matokeo.
Awali, Chama kikuu cha upinzani cha Republican People's Party, au CHP pamoja na chama cha wakurdi cha HDP vimesema vitayapinga matokeo kutoka baadhi ya vituo, vikidai kulikuwepo udanganyifu.
Mashirika ya waangalizi wa kimataifa wamekubaliana na upinzani kuwa pande zote hazikupata nafasi sawa, na kwamba zoezi la kuhesabu kura liligubikwa na kuondolewa kwa vigezo muhimu vya kimataifa na taratibu za kuvilinda.
Rais Erdogan atupilia mbali mbali ukosoaji
Alipokuwa akiwahutumia maelfu ya wafuasi wake jana, Rais Erdogan aliwashambulia vikali waangalizi wa shirika la amani na usalama barani Ulaya, OSCE.
'' Kuna shirika moja linaloitwa OSCE, ambalo linaandaa ripoti yake lenyewe, inayosema uchaguzi wa Uturuki ulienda hivi au vile. Kwanza nawambia, ''jueni nafasi yenu''. Hatuoni, hatusikii, wala hatuitambui ripoti yenu, tutaendelea katika njia yetu. Nyamazeni! Nchi hii imekwishafanya chaguzi nyingi za kidemokrasia ambazo hazijaonekana katika nchi yoyote ya Magharibi''. Amesema Erdogan.
Lakini licha ya malalamiko hayo ya upinzani na waangalizi wa kimataifa, na hata wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Rais Donald Trump wa Marekani amempongeza Rais Erdogan, akisifu ushirikiano kati ya nchi zao, katika vita dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, na katika juhudi za kumaliza vita nchini Syria.
Sheria ya hali ya hatari yarefushwa
Huku hayo yakiarifiwa, Baraza la Mawaziri la Uturuki jana Jumatatu liliidhinisha kurefushwa kwa sheria ya hali ya hatari, baada ya pendekezo lililotoka katika Baraza la Usalama wa taifa ambalo mwenyekiti wake ni Rais Recep Tayyip Erdogan. Bunge la Uturuki, ambalo linadhibitiwa na chama cha Haki na Maendeleo, AKP cha Rais Erdogan linatarajiwa kuridhia kurefushwa huko baadaye leo.
Tangu kuwekwa kwa sheria hiyo Julai mwaka jana imekuwa ikirefushwa kila baada ya miezi mitatu. Amri nyingi za rais zilizopitishwa katika kipindi hicho zina msingi wake katika sheria hiyo, kama vile kuwafuta kazi maelfu ya wafanyakazi katika sekta ya umma, na kuwatia kizuizini maelfu wengine wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa kiongozi wa kidini anayeishi uhamishoni Fethullah Gulen.
SHARE
No comments:
Post a Comment