Jengo
la Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria
lililozinduliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Desalegn tarehe 2
Julai, 2015 Kibaha, Pwani.
Mtaalam
wa Maabara ya Uandaaji Bakteria katika Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu
vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria kilichopo Kibaha Mkoani Pwani Bw.
Fumbuka Pauline akiwaeleza Waandishi wa habari baadhi ya kazi
wazifanyazo wakati wa kuwaandaa bakteria 15 Mei, 2017. Kushoto ni Kaimu
Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho, Bw. Samwel Mziray.
Mmoja
wa Waandishi wa Habari (kulia) akipiga picha ya bakteria wanaoonekana
kwa kifaa maalum cha kuangalia bakteria (Microscope) katika Maabara ya
kuaandaa bakteria 15 Mei, 2017 Kibaha, Mkoani Pwani.
Mtaalam
wa Maabara ya Uandaaji bakteria katika Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu
vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria kilichopo Kibaha Mkoani
akiangalia bakteria kwa kutumia kifaa maalum (Microscope) kabla ya
kuwapeleka sehemu inayohusika kwa ajili ya hatua nyingine, 15 Mei, 2017.
Kaimu
Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya
Mbu wa Malaria, Bw. Samwel Mziray (kulia) akiwaeleza Waandishi wa habari
baadhi ya kazi zinazofanywa katika moja ya mitambo iliyopo kiwandani
hapo 15 Mei, 2017.
Baadhi
ya mitambo iliyopo katika Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua
Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria kilichopo Kibaha, Mkoani Pwani.
Kaimu
Meneja Masoko na Mauzo wa Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua
Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria, Bw. Frank Mzindakaya akiwaeleza Waandishi
wa habari (hawapo pichani) namna kiwanda hicho kinavyoandaa madumu ya
dawa kwa ajili ya kuyasambaza kwa wateja wake 15 Mei, 2017 Kibaha,
Mkoani Pwani.
Mtaalam
wa Uthibiti wa Ubora wa Dawa wa Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua
Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria, Dkt. Nicholaus Banzi akiwaelezea
Waandishi wa habari namna hatua za ukuaji wa mbu na namna dawa
zinazotengenezwa na kiwanda hicho zinavyoweza kuua mazalia ya viluwiluwi
vya mbu wa malaria.
(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)
………………….
Na Benedict Liwenga-WHUSM.
Halmashauri
nchini zimetakiwa kuitikia wito wa kununua dawa za kuua viluwiluwi vya
mbu wa malaria zilizoanza kuzalishwa hapa nchini ili kukabiliana na
ugonjwa wa malaria.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Kaimu Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Kuzalisha
Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria cha Tanzania Biotech
Products Limited kilichopo Kibaha Mkoani Pwani, Bw. Samwel Mziray wakati
alipokutana na Waandishi wa habari na kufanya nao mazungumzo juu ya
shughuli zinazofanywa katika kiwanda hicho.
Bw.
Mziray amesema kuwa, dawa za kuua viluwiluwi vya mbu wa malaria
zinapaswa kununuliwa na kila Halmashauri nchini kwa maagizo yaliyotolewa
na Serikali kupitia waraka wake kwa kuwa kiwanda hicho kinachomilikiwa
na serikali kwa asilimia 100 kilijengwa ikiwa ni sehemu ya mkakati wa
serikali katika kupambana na malaria nchini. Hata hivyo amebainisha
kwamba mpaka sasa mwitikio wa halmashauri umekua mdogo kwani ni
halmashauri mbili tu za Geita pamoja na Mbogwe ndizo zimeshanunua dawa
hizo.
“Lengo
la Serikali kuja na mpango huu ni kupunguza vifo vitokanavyo na malaria
nchini na kupunguza gharama kubwa ya kununua dawa na vifaa tiba vya
kupambana na malaria”, alisema Mziray.
Amesema
kwamba iwapo kama halmashauri zitanunua dawa hizo na kuzitumia, ugonjwa
huo utapungua kwa kiasi kikubwa nchini na hivyo serikali kuelekeza
fedha zake katika shughuli za maendeleo.
Amesema
kwamba, kwa Afrika kiwanda hicho ni moja ya kiwanda kilichobahatika
kujengwa Tanzania ambapo nia ya Serikali ni kutokomeza ugonjwa wa
malaria kwa kuharibu mazalia ya mbu.
Ameongeza
kuwa, kiwanda hiki kitazalisha mbolea ya kibaiolojia (Bio fertilizer)
siku za usoni, lakini kwa sasa kiwanda kinazalisha dawa za aina mbili
ambazo ni Bactivec na Griselesf ambazo hutumika kwa kunyunyuzia katika
mazalia ya mbu.
Amefafanua
kwamba, kwa sasa kiwanda hicho kinaweza kuzalisha kwa wingi dawa hizo
ambapo ametaja moja ya nchi iliyonunua dawa hizo ni Niger ambayo tayari
imenunua lita 91,000 na nchi nyingine za Serbia na Srilanka ziko katika
mazungumzo ya kununua dawa hizo.
“Niiombe
Serikali iweze kutoa msukumo zaidi kwa halmashauri ambazo bado
hazijanunua dawa hizi kukitumia kiwanda hiki kufikia malengo kwani jamii
inapoteza wapendwa wao kutokana na ugonjwa wa malaria”, alisema Mziray.
Amefafanua
kuwa, dawa hizo zinaweza kutumika katika kipimo cha mililita moja kwa
lita 50 za maji na bei ya lita moja ni shilingi 13,000/= na zina uwezo
mkubwa wa kuangamiza viluwiluwi vya mbu wa malaria.
Kuhusu
agizo la Serikali la kuzitaka halmashauri nchini kununua dawa hizo
amesisitiza kwamba utekelezaji wa halmashauri hizo kuja kiwandani
unapaswa kuwekewa kipaumbele na Serikali na halmashauri hazinabudi
kuitikia wito huo.
“Serikali
imeshatoa waraka kwa halmashauri zote nchini kuweza kutumia kiwanda
hiki kununua dawa, kwahiyo sasa kilichobaki ni utekelezajina suala la
bei sio kisingizio, suala kubwa ni utayari na kuona umuhimu wa kufikia
malengo ya kutokomeza malaria kwa jamii”, alisema Mziray.
Aidha,
amebainisha kuwa, jukumu la kununua dawa hizo liko chini ya halmashauri
husika na inatakiwa kupanga bajeti yake ya kununua dawa hizo.
Kuhusu
suala la usalama wa dawa hizo amesema kwamba, dawa hizo ni salama kwa
binadamu na Kiwanda kinafanya mawasiliano na vyombo vya habari ili kutoa
elimu na mkazo mkubwa wa kununua dawa hizo.
Kwa
upande wake Kaimu Meneja Masoko na Mauzo wa Kiwanda hicho, Bw. Frank
Mzindakaya amesema kwamba, Serikali hainabudi kutenga bajeti ya kutosha
ili kuziwezesha halmashauri kununua dawa hizo.
Ameongeza
kuwa, dawa za kiwanda hicho wanaziweka katika vipimo mbalimbali ikiwemo
vya lita 20 na ujazo wa miligramu 30 na katika matumizi makubwa mteja
mkubwa ni Serikali yenyewe kwakuwa ndiyo inayonunua kupitia Halmashauri
na kwenda kuzinyunyuzia katika madimbwi. Kwa mwananchi wa kawaida
anaweza kununua miligramu 30 ili aweze kutumia kwa matumizi ya kifamilia
ya kujikinga yeye na familia yake.
“Serikali
haijamtwisha mzigo mwananchi yeyote wa kununua dawa hizi ndiyo maana
tunazisisitiza kuwa halmashauri zije kununua dawa hizi ili ziende
kuwasaidia wananchi kwa kuziweka katika madimbwi makubwa na hatimaye
kuwalinda wananchi dhidi ya malaria”, alisema Mzindakaya.
Tanzania
Biotech Products Limited (TBPL) ni Kampuni tanzu ya Shirika la
Maendeleo (NDC) iliyopewa dhamana ya kusimamia na kuendesha kiwanda cha
kuzalisha bidhaa za kibaiolojia zikiwemo viuadudu vya kuua viluwiluwi wa
mbu waenezao malaria (Biolarvicides). Kiwanda hiki kipo eneo la TAMCO
Kibaha, Mkoa wa Pwani.
SHARE
No comments:
Post a Comment