Meneja wa Kanda ya Kaskazini kutoka Tigo,
Aidan Komba, akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu
uzinduzi wa huduma ya 4G LTE mkoani Singida, kushoto ni Meneja Mauzo wa
Mkoa wa Singida Raymond Royer.
Waandishi wa habari wakichukua matukio kwenye mkutano huo wa uzinduzi wa Huduma ya 4G LTE mkoani singida mapema leo.
Singida, Mei 22, 2017-Wateja wa Tigo mkoani Singida hivi sasa
wanaweza kufurahia kuunganishwa na huduma ya intaneti ya kasi kufuatia
kampuni hiyo kupanua huduma yake ya 4G LTE katika mji huo uliopo
katikati ya Tanzania. Teknolojia ya 4G ina takribani kasi ya mara tano
zaidi ya teknolojia ya 3G ambayo inapatikana hivi sasa katika soko.
Kwa mujibu wa Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini Aidan Komba ni kwamba
upanuzi wa huduma hiyo unafuatia mafanikio yaliyopatikana baada ya
kuizindua katika mji mingine mikubwa nchini.
Komba alisema kwa kuifanya huduma ya 4G kupatikana Singida, “Tigo kwa
mara nyingine tena imeonesha kujikita kwake katika kuboresha
mabadiliko katika mtindo wa maisha ya kidijitali na inavyoongoza katika
kutoa teknolojia ya kisasa na ubunifu katika soko hili.”
Alitangaza kuanza kwa enzi mpya za kidijitali katika historia ya
mawasiliano ndani ya Singida akibainisha kwamba Tigo 4G LTE
itahakikisha kunakuwepo uwezo mkubwa na muhimu katika kuwaunganisha
wateja ndani ya mkoa huo.
“Singida ni kituo muhimu kibiashara kwa mikoa ya kati na kaskazini mwa
Tanzania. Tunaamini kwamba wakazi wa Singida, jumuiya ya kibiashara na
wadau wataufurahia huduma Tigo 4G LTE na hivyo kuzifanya shughuli zao
kwa njia ya mtandao kuwa rahisi zaidi.”
“Mawasiliano ya simu ni nguzo muhimu kwa jamii iliyoendelea. Kwa hiyo
mtandao wa 4G utachangia katika maendeleo ya sekta mbalimbali zikiwemo
elimu, fedha na huduma za afya na hali kadhalika kukuza uchumi na
biashara”, alisema Komba.
“Kama mnavyojua, Tigo imekuwa mstari wa mbele katika kuzisaidia jamii
zinazotuzunguka, na mfano mzuri ukiwa ni uchimbaji wa visima 12 ambavyo
tulivitoa kama msaada kwa vijiji vya Singida mwaka jana,” Komba
alibainisha.
Aliongeza kwamba gharama ya vifurushi vya 4G LTE ni sawa na ile ya
vifurushi vya 3G na kufafanua kuwa wateja wanachotakiwa ni kuwa na
kifaa kinachowezesha 4G LTE ama simu ya kisasa (Smartphone) au modemu
ikiwa na kadi ya simu ya 4G LTE ili kuwawezesha kupata muunganisho na 4G
LTE. Alieleza kuwa wateja wanaweza kubadilisha au kununua kadi ya simu
ya 4G LTE kutoka katika duka la Tigo la huduma kwa wateja lililopo
Singida Mjini.
Akizungumzia uwekezaji katika mtandao, Komba alisema kwamba Tigo
imewekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya kisasa, ikilenga
kusaidia katika maendeleo endelevu ndani ya mkoa.
Alihitimisha kwa kusema, “Mipango imo njiani katika kupanua huduma kwa
ajili ya mikoa iliyobakia ili hatimaye kuisambaza nchi nzima.”
Kwa upande wake, Meneja wa mkoa wa Singida wa kampuni ya Tigo, Raymond
Royer alibainisha umuhimu wa huduma ya 4G na mchango wake katika
kuboresha huduma za uwanda mpana wa simu za mkononi.
Royer alisema, “Katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwepo ongezeko
kubwa la idadi ya wateja pamoja na matumizi ya data; simu za kisasa
idadi yake imeongezeka kwa asilimia 90 na hivyo kubadilisha namna
tunavyowasiliana.”
Aliongeza, “Kwa hiyo teknolojia ya Tigo 4G LTE inampatia mteja faida
mbili za data zilizo na kasi kubwa na kupunguza ucheleweshaji. Ni
nguvu ya mabadiliko ambayo itaboresha mtindo wa maisha ya kidijitali
kwa wateja wetu.”
Mtandao wa 4G LTE unamaanisha kasi kubwa katika kurambaza (Surf) na
kupakua mada kutoka katika intaneti na kupiga miito ya mawasiliano ya
kuonana (Skype). Kwa kiwango kikubwa inaboresha uzoefu wa wateja katika
kutiririsha video au kufanya mikutano. Hali kadhalika inaweza
kuhifadhi zana nyingi kama vile mkutano wa video, muonekanao wa hali ya
juu, blogu za video, michezo na kutiririsha video kutoka katika
mitandao ya kijamii.
SHARE
No comments:
Post a Comment