Wananchi wa Brazil wamefanya maandamano makubwa ya
kumshinikiza rais wao Michel Temer ajiuzulu baada ya Mahakama Kuu kutoa
amri ya kumchunguza kutokana na kuhusishwa kwake na rushwa
Madai yanayomkabili Rais Timer yamelitumbukiza taifa hilo kubwa
katika eneo la Amerika Kusini katika mzozo kwa mara nyingine tena. Rais
Temer analaumiwa pia kwa visa vinavyohusiana na rushwa hali ambayo
inazihujumu juhudi za serikali yake za kujiondoa kwenye hali mbaya ya
uchumi katika historia ya Brazil.Maandamano hayo yalifanyika katika miji tofauti ikiwemo Sao Paulo na Rio de Jenairo, ambapo mamia ya waandamanaji walitembea kandoni mwa fukwe za bahari huku wakiimba na wengine wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa ''Temer Nje!''. Maandamano hayo yamesabaisha kushuka kwa sarafuya nchi hiyo na pia hasara kwenye soko la hisa. Mzozo huu mpya sasa umesababisha kuzorota kwa mageuzi kadhaa yaliyowekwa kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo kutoka kwenye hali mbaya ya uchumi wake ulioporomoka.
Hata mwaka mmoja haujatimia tangu Rais Temer alipochukua madaraka baada ya rais aliyemtangulia, Dilma Rousseff, kuvuliwa madaraka. Kwa sasa miito ya kutaka Temer aondoke madarakani au avuliwe madaraka inaendelea, wa karibuni kabisa ukiwa mwito kutoka jopo la wanasheria ambao siku ya Jumamosi walipiga kura ya kuwasilisha bungeni hoja ya kumtaka Rais Timer ang'olewe
madarakani. Mmoja wa waandamanaji alisema alitegemea hali ingeimarika baada ya rais wa zamani Dilam Rousseff kuondolewa madarakani, lakini sivyo ilivyokuwa, amesema Wabrazil lazima wafikirie upya wakati wa kupiga kura kwenye uchaguzi ujao ili kuweza kuwachagua viongozi wazuri katika siku za usoni. Wengi kati ya watu walioshiriki kwenye maandamano hayo katika jiji la Sao Paulo walisema wakati wote walikuwa wakimpinga Rais Temer tangu alipochukua hatamu za uongozi na wanafikiri kuwa rais wa zamani, Dilma Rousseff, alidhulumiwa kung'olewa madarakani na kwamba hatua hiyo ilichochewa kisiasa na haikuwa halali.
Katika jiji la Rio de Janeiro, hata hivyo, idadi ya watu walioshiriki kwenye maandamano hayo haikuwa kubwa. Takriban waandamanaji 150 walijitokeza. Wakati huo huo, Rais Temer anaendelea kusema hataachia madaraka kwa sababu haoni kosa alilolifanya. Temer anadai kuwa mkanda uliorekodiwa ukimuonyesha akitia saini ruksa ya kupewa fedha aliyekuwa spika wa bunge, Eduardo Cunha, kwa ajili ya kufunga mdomo wake umetengezwa makhsusi kumuharibia sifa. Cunha yuko kifungoni baada ya kuhukumiwa kwa makosa ya rushwa. Temer vile vile amemtaka jaji wa mahakama kuu asimamishe mara moja uchunguzi aliouamuru dhidi yake, jambo ambalo, hata hivyo halitakuwa rahisi kutimizwa.
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment