Rais Donald Trump wa Marekani amewasili leo nchini
Israel akitokea Saudi Arabia. Akizungumza baada ya kuwasili, Trump
amesema eneo la Mashariki ya Kati linayo fursa adimu ya kupata amani.
Kesho ataizuru Palestina.
Ndege inayomsafirisha Rais Trump imetua muda mfupi uliopita katika
uwanja wa ndege wa David Ben Gurion mjini Tel Aviv, na kiongozi huyo
kupata mapokezi ya heshima za Kijeshi. Uwanjani hapo amepokelewa na
waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na rais wa nchi hiyo Reuven
Rivlin.Trump na Netanyahu wametoa hotuba fupi wakati wa sherehe ya
mapokezi, kabla ya Trump kusafiri kwa helikopta kwenya mjini Jerusalem.Wote wawili wamezungumzia suala la amani; Netanyahu akitaka ziara ya Trump kuwa hatua ya kihistoria kuelekea amani na maridhiano, naye Trump akitaja kuwepo kwa fursa adimu ya kupata amani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Hapo kesho Rais huyo wa Marekani anatarajiwa kuyatembelea maeneo ya wapalastina yanayokaliwa na Isarael katika Ukingo wa Magharibi, ambako atafanya mazungumzo na rais wa Palestina Mahmoud Abbas.
Hatua za kujengeana imani
Kabla ya kuwasili kwa Trump nchini Israel, serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imechukua hatua zisizo za kawaida za kuwanufaisha wapalestina, ikiwa ni pamoja na kutoa vibali vya ujenzi katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi ambayo yako chini ya ukaliaji kamili wa Israel, vibali ambavyo ni nadra sana kutolewa kwa wapalestina. Hatua hizo zinaonekana kama juhudi za kujaribu kujenga imani.
Hii ni sehemu ya pili ya ziara yake ya kwanza nje ya Marekani tangu alipochukua madaraka mwezi Januari, ambayo imeanzia nchini Saudi Arabia. Katika hotuba yake kwa viongozi wa kiarabu na wa kiislamu mjini Riayadh, Trump aliwataka viongozi hao kuangamiza ''misimamo mikali ya Kiislamu''.
Kabla ya kwenda Israel, Rais Donald Trump alikutana na viongozi wa Kiarabu na wa Kiislamu nchini Saudi Arabia
''Hivi
ni vita kati ya wema na uovu. Tunaposhuhudia uharibifu unaosababishwa
na ugaidi, hatuoni alama kwamba waliouawa ni wayahudi au wakristo,
washia au wasuni. Tunapotazama mtiririko wa damu katika maeneo ya kale,
hatuoni dini, madhehebu au kabila la wahanga.'' Amesema Trump katika
hotuba yake.Afuata nyayo za watangulizi wake
Tofauti na watangulizi wake, Rais Donald Trump hakughusia suala la ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na viongozi wa kiimla katika eneo la Mashariki ya Kati, bali amesema, '' hatuko hapa kutoa mihadhara kuwafundisha wengine namna ya kuishi maisha yao, juu ya cha kufanya na namna ya kuabudu''.
Na kinyume kabisa na matamshi yake wakati wa kampeni, kwamba anaamini Uislamu unaichukia Marekani, mbele ya viongozi wa Kiarabu na Kiislamu, Trump aligeuza kauli na kuusifu Uislamu kama mojawapo ya dini kuu duniani.
Wachambuzi wamesema hotuba ya Trump mbele ya viongozi wa Kiarabu na Kiislamu imechukua mkondo ule ule wa watangulizi wake kuhusu Mashariki ya Kati, akiepuka kabisa kusema chochote kuhusu amri ya kutatanisha aliyoitia saini kupiga marufuku wasafiri kutoka nchi kadhaa zenye waislamu wengi kuingia nchini Marekani, ambayo wakosoaji wake wanasema inalenga waislamu kwa misingi ya imani yao, ambavyo ni kinyume na katiba ya Marekani.
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment