Julian Msacky
JANUARI mwaka juzi Taifa lilishtushwa na tukio la kuuawa kwa
askari watatu wa Kituo cha Polisi Ikwiriri mkoani Pwani.
Hilo lilikuwa tukio la kwanza kutikisa mkoa huo na hadi sasa
hali si shwari kwani mauaji yanazidi kuendelea.
Kama hiyo haitoshi, Februari mwaka huu, Mkuu wa Upelelezi
Wilaya ya Kibiti, Peter Kubezwa aliuawa na watu wengine wawili.
Wakati hali ikiwa hivyo, Aprili 9 mwaka huu askari wengine
watatu waliuawa tena wakati wakiwa eneo la kizuizi.
Haikuishia hapo. Aprili 13 tulipoteza tena askari wengine
wanane kwa mkupuo baada ya kushambuliwa kwa risasi.
IGP Simon Sirro
Askari hao walikumbwa na unyama huo wakati wakirejea kambini
na kujikuta pia wakiibiwa bunduki saba.
Daah. Hii ndiyo Pwani. Eneo hili kwa sasa ni hatari kwani si
kwa askari tu bali na wananchi wengine wanauawa ovyo ovyo.
Ingawa walioathirika ni wengi, itoshe kusema kinachoendelea
Kibiti, Mkuranga na Rufiji ni tishio kwa wengi wetu.
Amani ni kana kwamba imetoweka sehemu hizo. Hofu imetawala wananchi
pamoja na viongozi wao. Huo ndiyo ukweli.
Kwa mfumo huo kuna mambo ambayo Serikali inatakiwa kufanya,
la sivyo Pwani tunayoijua itakuwa si rafiki kwa wengi.
Ni lazima ifanye jambo litakaloonesha ‘wababe’ hao hawana
nafasi tena kuendelea unyama wanaofanya.
Askari wetu wameuawa mno. Raia wetu wameuawa mno. Tumepoteza
vitendea kazi vyetu vingi. Tuseme imetosha.
Je, nini kifanyike kuondoa hali hiyo? Kusema kweli serikali
inatakiwa ibadilishe mbinu ya kukabiliana na maadui hao.
Ninasema hivi kwa sababu siku chache tu baada ya Rais
kuzungumzia mauaji hayo akiwa Pwani, askari wa usalama waliuawa.
Hii ina maana kuwa kuna kikundi kidogo cha wahalifu
kimejichimbia maeneo hayo kufanya unyama unaofanyika sasa.
Lakini pia ni lazima tukubali kuwa mauaji hayo yanaonekana
kulenga kikundi fulani cha watu kwa sababu maalumu.
Kwa hiyo ni jambo muhimu kwa serikali kufanya uchunguzi wa
kina kubaini kiini cha mauaji yanayofanyika.
Ieleweke hapa kuwa mitutu na askari pekee hayatasaidia kuleta
amani eneo hilo. Kuna umuhimu wa kusikiliza wananchi.
Viongozi wa serikali wakae nao. Wasikilize wanasema nini kwa
sababu kwa nini mauaji hayo yanazidi kushika kasi?
Je, kuna uonevu waliofanyiwa au ulifanyika? Je, kuna dalili
za chuki za kisiasa au watu kuchukuliwa ardhi yao?
Ni lazima tuende mbali zaidi kupata kiini cha tatizo. Kwa
hali ilivyo sasa hakuna taarifa ambayo tunaweza kusema haifai.
Kila kinachozungumzwa ni lazima kifuatiliwe kwa umakini
mkubwa kwa lengo la kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Jambo la kutia matumaini ni kuwa maeneo hayo kuna viongozi wa
dini, viongozi wa kisiasa, asasi za kijamii na wananchi.
Makundi yote haya bila shaka yana fununu ya kiini cha tatizo.
Kiongozi wa dini asipojuia wa kisiasa atakuwa na jibu.
Kiongozi wa kisiasa akikosa cha kujibu viongozi wa asasi za
kiraia watasaidia au wananchi wenyewe wa maeneo husika.
Ni muhimu kuchukua hatua za haraka kwa sababu huenda wahalifu
wanaofanya unyama huo wanazidi kujipanua.
Wanazidi kujipanga namna ya kukabiliana na vyombo vya dola
hivyo ni vizuri uchunguzi wa kina ukafanyika.
Tunaamini njia hizo zikitumika kwa kushirikisha wananchi
wenyewe ni lazima tutapata mwanga wa suala hilo.
Kama hiyo haitoshi ninaamini meza ya mazungumzo ni nzuri
zaidi kupata ufumbuzi wa kinachoendelea huko.
Historia inaonesha kuwa mazungumzo yana tija kuliko kutumia
nguvu. Hivyo yatumike kuleta suluhu mkoani Pwani.
Ifike mahali tuseme mauaji ya Kibiti yanafikia mwisho. Lengo
ni kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na upendo.
Hii ni kwa sababu hali ilivyo sasa wananchi wengi wanaishi kwa
hofu achilia mbali wataalamu mbalimbali.
Ni rai yangu kuwa viongozi wa serikali watakaa chini na
kupata ufumbuzi wa hali tete inayoendelea mkoani Pwani.
Kama nilivyosema mwanzo mauaji yanayoendelea Kibiti, Mkuranga
na Rufiji kwa hatua iliyofikiwa si ya kupuuza tena.
Ni lazima hatua za haraka zichukuliwe na kuhakikisha mtandao
unaofanya unyama eneo hilo unazikwa kabisa.
SHARE
No comments:
Post a Comment