TRA

TRA

Tuesday, June 20, 2017

MAADHIMISHO YA SIKU YA WAKIMBIZI DUNIANI

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !



unnamed
Kila mwaka, tarehe 20 Juni, Mataifa yote ulimwenguni huadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani (World Refugee Day). Awali siku hiyo ilikuwa inaadhimishwa Barani Afrika peke yake ikiitwa Siku ya Wakimbizi Barani Afrika na kuanzia mwaka 2001 Maadhimisho hayo yalianza kufanyika Duniani kote baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuelekeza hivyo katika kuadhimisha miaka 50 ya Sheria ya Kimataifa ya Wakimbizi.
Lengo la maadhimisho haya ya kila mwaka ni kuhamasisha Ulimwengu kutambua uwepo wa mamilioni ya wakimbizi na watu wengine wanaohama kutoka kwenye maeneo yao kwenda maeneo mengine ndani ya nchi zao (internally displaced persons) kuogopa vita, migogoro na mateso.
Maadhimisho haya huwahusisha viongozi wa serikali, watumishi wa mashirika ya misaada, watu mashuhuri na wakimbizi wenyewe. Maadhimisho haya huambatana na kauli mbiu ambayo kutoa msisitizo wa jambo ambalo hupewa msukumo katika matamko ya mwaka husika ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tuko Pamoja na Wakimbizi’  ikiwa na lengo la kukumbusha jukumu la kila mmoja la kuwasaidia wakimbizi na kutafuta ufumbuzi wa matatizo ambayo yamesababisha wao kujikuta katika hali hiyo.
Kama inavyofahamika Tanzania imekuwa na historia ndefu ya kuhifadhi wakimbizi toka nchi mbalimbali za Afrika na kwingineko.  Kwa vipindi mbalimbali wamekuwepo wakimbizi tofauti tofauti kama vile  wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi za Kusini ya Afrika ambapo kulikuwa na wakimbizi toka Afrika Kusini, Namibia, Msumbiji, Angola na Zimbabwe ambao walirudi katika nchi zao za asili baada ya ukombozi kupatikana katika nchi hizo.
Aidha, nchi yetu inaendelea kuhifadhi wakimbizi toka nchi za jirani zinazokumbwa na migogoro ya kisiasa na kivita hususani zile za Maziwa Makuu za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Pembe ya Afrika kama Somalia na wachache toka nchi mbalimbali.
Maazimio ya mwaka huu, ya Siku ya Wakimbizi Duniani yanaikuta nchi yetu ikiwa inahifadhi wakimbizi wapatao 345,000, wengi wao wakiwa wanatoka katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na ambao wanahifadhiwa katika kambi zilizoko Mkoa wa Kigoma za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli na wengine wachache waliosalia baada ya wenzao wengi kupata uraia ambao wapo Katavi na Tabora.
Kwa kuzingatia uwepo wa wakimbizi hao, maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika Dar es Salaam ambapo yatahusisha Wakimbizi wenyewe, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Viongozi wa Serikali, Asasi zisizo za Kiraia, watumishi wa Mashirika ya Misaada, na Wasanii maarufu, vyombo vya habari, wananchi na kwenye maeneo yanayohifadhi wakimbizi katika Mikoa iliyotajwa.
Serikali yetu itapenda kutumia maadhimisho ya mwaka huu kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa, wakimbizi wenyewe pamoja na wadau mbalimbali kuwa  itaendelea kuchukua hatua muhimu za kuboresha huduma kwao katika sekta za elimu, afya, makazi na kuihuisha Sera ya Wakimbizi ili ieandane na changamoto za wakati huu.
Kwa upande wa elimu, Serikali inatambua tatizo la upungufu wa madarasa katika kambi za wakimbizi linalotokana na upungufu wa fedha zinazotolewa na Wahisani kufadhili mradi mzima wa kuhifadhi maelfu ya wakimbizi toka nchi za jirani na kwingineko. Pamoja na hayo, nchi yetu kwa kushirikiana na UNHCR na wadau wengine itafanya jitihada za kujenga madarasa na miundo mingine muhimu kuhakikisha kuwa watoto wote wa wakimbizi wanapata elimu bora kuwawezesha  kupata taaluma na ujuzi utakaowanufaisha wao wenyewe na jamii zao wakiwa kwenye kambi na wakati watakaporejea kwenye nchi zao za asili .
Vile vile Serikali, kupitia  taasisi yake   ya RITA, inakusudia kutoa vyeti vya kuzaliwa, kwa watoto wa wakimbizi ambao wanazaliwa hapa nchini, katika kambi za wakimbizi, ili kuwafanya  watoto hao kuwa na hati zinazotambulika kisheria na zenye kubainisha waziwazi uraia wao wa asili. Ni vema ikafahamika kuwa hati hizo ni muhimu hata baada ya maisha ya ukimbizi. Uamuzi wa kuwapatia hati  unafuatia makubaliano baina ya serikali  na UNHCR yanayowezesha Shirika hilo kusaidia
 nyenzo muhimu zinazohitajika  katika zoezi  hilo.
Ni nia ya Serikali kuhakikisha kuwa wakimbizi wanapata hati zote muhimu zinazohitajika kama cheti cha kuzaliwa, kitambulisho n.k kwa mujibu ya Mikataba ya Kimataifa mbayo nchi  imeiridhia. Ni matarajio ya Serikali kuwa vyeti vya kuzaliwa vitaanza kutolewa kabla ya mwisho wa mwaka huu na utakuwa ni utaratibu wa kudumu.
Eneo jingine ambalo litapewa kipaumbele kwa lengo la kuboresha huduma kwa wakimbizi ni mradi wa kuhuishwa Sera ya Wakimbizi na Sheria pamoja na mambo mengine, Sera  mpya na Sheria zitakazotungwa inakusudia kupanua wigo wa wakimbizi wenye ujuzi na sifa za kupata ajira kama wataalamu katika sekta mbalimbali na pia kupata fursa za kujiari wenyewe nje ya kambi.
Wakati dunia inaadhimisha siku ya Wakimbizi Duniani, ni vema pia tukaikumbusha Jumuia ya Kimataifa kuhusu wajibu wao kuongeza ufadhili kuzisaidia nchi changa, kama Tanzania, kutekeleza jukumu la kuhifadhi wakimbizi.  Misaada wanayotoa inasaidia katika  kupatikana kwa bidhaa mbalimbali ambazo zitatumiwa na wakimbizi na huduma nyingine wanazohitaji.  Ni vema ikaeleweka pia kuwa Jumuia ya Kimataifa ina wajibu wa kuzisaidia jamii ambazo zinaathirika na uwepo wa wakimbizi wengi kama  Kagera, Kigoma, Katavi na Kigoma.
Imetolewa na
Balozi Hassan Simba Yahya
Kaimu Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
20  Juni, 2017

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger