
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu,
Kanda ya Iringa, Mhe. Mary Shangali akisisitiza jambo alipokuwa akiongea
na baadhi ya Mahakimu wa Mahakama mkoani Njombe baada ya kukamilisha
ukaguzi katika Mahakama za Mwanzo na Wilaya zilizopo mkoani humo.

Mhe.
Jaji Mfawidhi akiongea jambo huku akiwaonyesha baadhi ya Mahakimu
(hawapo pichani) nakala ya kitabu cha Muongozo wa kufanya ukaguzi wa
Mahakama alipokuwa akiongea nao mara baada ya kukamilisha ziara yake ya
kukagua, Mahakama za Mwanzo na Wilaya- Njombe.

Baadhi ya Waheshimiwa Mahakimu. Waliohudhuria katika kikao kati ya Mhe. Jaji Mfawidhi na Mahakimu Mkoani Njombe.

Mahakimu wakiandika baadhi ya
masuala muhimu aliongelea Mhe. Jaji Mfawidhi katika kikao hicho
kilichofanyika katika Ukumbi wa Mahakama ya Wilaya-Njombe mapema Juni 8.


Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo,
ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto akiendelea na
kazi, Mhe. Jaji Dkt. Kihwelo yupo Njombe akiendelea na vikao maalum vya
kuondosha mlundika wa mashauri linaloendelea kwa sasa.

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo-Lupembe iliyopo mkoani Njombe, Mhe. Godfrey Msemwa akiuliza swali ili kupata ufafanuzi

Naibu Msajili, Mahakama
Kuu-Kanda ya Iringa, Mhe. Agatha Chugulu akitoa ufafanuzi juu ya maswali
kadhaa yaliyoulizwa katika kikao hicho.

Naibu Msajili, Mhe. Chugulu akiendelea kutoa ufafanuzi

Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu,
Kanda ya Iringa, Mhe. Mary Shangali (wa nne kushoto) akiwa katika picha
ya pamoja na baadhi ya Mahakimu wa Mahakama mkoani Njombe mara baada ya
kika, wa tatu kushoto ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Kanda ya Iringa,
Mhe. Agatha Chugulu

Muonekano wa jengo la
Mahakama ya Hakimu Mkazi-Njombe, jengo hili limegawanyika sehemu mbili
(2), ambapo upande mwingine ipo Mahakama ya Wilaya- Njombe.

Muonekano wa sehemu ya jengo la Mahakama ya Wilaya-Njombe (Picha na Mary Gwera, Mahakama)
……………………………………………………………………………………..
Na Mary Gwera, Mahakama, Njombe
JAJI Mfawidhi, Mahakama Kuu,
Kanda ya Iringa, Mhe. Mary Shangali ametoa wito kwa Mahakimu na wadau wa
Mahakama nchini kushirikiana kwa pamoja katika kutoa huduma ya haki kwa
wananchi.
Aliyasema hayo mapema Juni 07,
alipokuwa akiongea na Mahakimu wa Mahakama mkoani Njombe baada ya
kuhitimisha ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama katika Mahakama
za Mwanzo na Wilaya za Njombe, Ludewa na Makete pamoja na Gereza la
Ludewa na Makete.
“Ushirikiano wa karibu na Wadau
wa Mahakama kama Polisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mawakili
na Watumishi wa Mahakama n.k ni muhimu katika kutekeleza shughuli yetu
ya utoaji haki kwa wananchi, jambo hili lina faida nyingi mojawapo
ikiwa ni kusaidia kupunguza mlundikano wa kesi katika Mahakama zetu,”
alifafanua Mhe. Shangali ambaye pia ni Jaji namba moja (1) wa Mahakama
Kuu ya Tanzania.
Kwa upange mwingine, Mhe. Jaji
Shangali alibainisha changamoto alizokumbana nazo katika ziara yake ya
kukagua shughuli za Mahakama mkoani Njombe kuwa ni tatizo kubwa la
usafiri wa kuwachukua Mahabusu kutoka Magerezani na kuwarudisha.
“Hii ni moja ya changamoto kubwa
niliyokumbana nayo katika Mahakama zote nilizozitembelea mkoani Njombe,
changamoto hii haiihusu Mahakama moja kwa moja ipo chini ya Jeshi la
Polisi, lakini kwa kuwa tunafanya kazi kwa kutegemeana changamoto hii
inatuathiri na inaweza kusababisha mlundikano wa mashauri na Mahabusu
magerezani kutokana na Wahusika wa kesi kutofikishwa Mahakamani kwa
ajili ya kusikiliza kesi zao kwa wakati stahiki,” alisema Jaji Shangali.
Aliongeza kuwa, katika ziara hiyo
malalamiko mengine yaliyotolewa yaliwahusisha baadhi ya Mahakimu kuwa
na tabia ya kutowasikiliza Washitakiwa kwa makini na hatimaye kutoa
maamuzi tofauti na uhalisia wa shauri husika.
“Naomba niwaombe ninyi Mahakimu
mliopo hapa na baadhi ya Mahakimu nchini kutekeleza jukumu la utoaji
haki kwa Weledi, kwani Mahakama ndio kimbilio la wananchi hivyo ni vyema
kutoa nafasi kusikiliza kwa makini na usahihi pande zote ili kufanya
maamuzi yanayostahili,” alieleza Jaji Mfawidhi huyo.
Aidha; Mhe. Jaji Shangali
amesisitiza juu ya utoaji wa Adhabu Mbadala kwa watuhumiwa wenye makosa
madogo madogo ili kuepuka mlundikano usio wa lazima magerezani.
Akiongelea juu ya Programu maalum
ya kuondosha mlundikano wa Mashauri linaloendelea nchini, Jaji Mfawidhi
alisema kwa sasa Mahakama kanda ya Iringa inaendelea na kikao maalum
cha Mahakama (special session) cha awamu ya tatu (3) kilichoanza rasmi
Mei 29 kinachofanyika Njombe chini ya Mhe. Paul Kihwelo ambapo katika
kikao hicho jumla ya mashauri 32 yatasikilizwa na kutolewa maamuzi.
“Kikao cha awamu ya kwanza
kilianza rasmi Aprili, 24 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa na Makao
makuu na kumalizika Mei, 26 mwaka huu, katika kikao hicho jumla ya
mashauri 41 yalipangwa kusikilizwa na kutolewa maamuzi, hata hivyo hadi
kufikia Mei 26, jumla ya mashauri 37 yalimalizika huku mengine yakiwa
yanaendelea na usikilizwaji wa awali na mengine yakiwa katika hatua ya
mwisho ya kutolewa maamuzi,” alisema Jaji Shangali.
Aliongeza kuwa kikao kingine cha
pili kilifanyika Mafinga huku jumla ya mashauri 28 kati ya mashari 42
yaliyopangwa kusikilizwa kumalizwa, hata hivyo alisema kuwa mashauri
mengine yaliyobaki yapo katika hatua za mwisho kwa ajili ya kuyatolea
maamuzi.
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama
Kuu, Kanda ya Iringa wamejiwekea utaratibu wa kukagua Mahakama na
utendaji kazi wake pindi wanapomaliza kufanya kikao maalum katika sehemu
husika, hali ambayo huwawezesha kujua changamoto na mafanikio
mbalimbali yaliyopo katika maeneo hayo, lengo kuu likiwa ni kuboresha
huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
Hata hivyo Mahakama ya Tanzania
kupitia Maafisa wake imekuwa na utaratibu wa kufanya kaguzi za mara kwa
mara kwa nyakati tofauti kwa lengo la kufuatilia kwa karibu kuona hali
ya utendaji wa Mahakama mbalimbali kama zinaendana na matakwa ya Mhimili
huu muhimu wenye dhamana ya kutoa haki kwa wananchi.
SHARE
No comments:
Post a Comment