Mbunge wa Dodoma mjini Anthony Mavunde akisalimiana na wauguzi
katika hospitali ya Rufaa ya Dodoma wakati wa uzinduzi wa matumizi
ya mfumo wa Biometrics na kamera za CCTV katika Hospitali hiyo.
NA K-VIS BLOG, DODOMA
MBUNGE
wa Dodoma mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, ((sera,
bunge, kazi, vijana, na watu
wenye ulemavu), Mhe.Anthony Mavunde ameendelea kutatua kero katika sekta
ya Afya jimboni humo ambapo leo Julai 20, 2017 amezindua matumizi ya mfumo wa
Biometrics na kamera za CCTV katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Dodoma,kufuatia hali hiyo wagonjwa wengi waliokuwepo hospital hapo walionekana
wenye furaha na kuunga mkono jitihada za mbunge wao katika kusaidia kuboresha
huduma za Afya katika hospital hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi wa matumizi ya vifaa hivyo, Mavunde
amesema ufungaji wa mifumo hiyo ni miongoni mwa jitihada zake za kuhakikisha
huduma za afya katika jimbo hilo zinatolewa ipasavyo.
Mavunde ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira
na Vijana amesema mfumo huo umefungwa na Ofisi ya Mbunge wa Dodoma na
amelazimika kufunga vifaa hivyo kutokana na malalamiko ya muda mrefu ya
wagonjwa kuwa wamekuwa wakitolewa lugha chafu na wauguzi.
Amesema pamoja na kamera hizo, pia umefungwa mfumo wa
Biometrics(uchukuaji alama za dole gumba) ili kudhibiti watumishi ambao
wamekuwa wakiondoka kabla ya muda na kuchelewa kuingia kazini.
“Kamera hizi zinarekodi sauti na kuchukua video ili kuondokana
na malalamiko yaliyotolewa na wananchi na itakuwa ni rahisi kumbaini mtu
atakayelalamikiwa na mgonjwa,”amesema Mavunde
Mavunde amesema fedha alizotumia kununulia Kamera hizo na mfumo
wa Biometrics amezipata kwa kujibana katika mshahara wake lengo likiwa ni
kutekeleza ahadi yake aliyowaahidi wananchi wakati wa Kampeni kutatua kero za
afya.
Aidha amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya utoaji
huduma kwa wananchi hasa ukizingatia kwasasa Dodoma kuna ongezeko la watu
kutokana na serikali kuhamia mkoani humo.
“Baadaye pia tutaweka mfumo wa kuhifadhi mafaili, hii yote ni
kurahisisha utendaji kazi katika hospitali hii ili wananchi wetu waweze kupata
huduma za afya ipasavyo.pia nimeomba vifaa mbalimbali vya kisasa Ujerumani kwa
ajili ya hospitali hii tukipatiwa itasaidia sana utoaji huduma za
afya,”amesisitiza Mavunde
Amesema ameahidi kutatua changamoto katika sekta ya afya ambapo
mbali na ufungaji vifaa hivyo alishakabidhi vitanda katika Zahanati na Vituo
vya afya 35.
“Nimetoa madawa kwenye kituo cha afya cha Makole yenye thamani
ya Sh. Milioni 15,nimefunga umeme wa jua katika vituo vya Afya 17 pamoja na
huduma za macho kwa watu 7000 na watu 3000 walipata huduma za upasuaji
bure,”amesema
Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo,Dk.Caroline Damiani amemshukuru
Mbunge huyo huku akidai kuwa matunda ya ufungaji wa kamera yameanza kuonekana
kwa watumishi kufanya kazi zao kwa ufanisi wa hali ya juu tofauti na awali.
“Kumekuwa na kero nyingi kutoka kwa wagonjwa sasa Kamera za CCTV
zitatusaidia kutatua kero hizi na kudhibiti wale wanaotoka kabla ya muda wa
kazi kuisha au kuchelewa kazini,”amesema Mganga huyo
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni ya Entersoft
Limited,Keneth Yindi amesema wamefunga Kamera 4 pamoja na mfumo wa Biometrics
katika hospitali hiyo na ina uwezo wa kurekodi matukio kwa miezi tisa
mfululizo.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni ya Entersoft Limited,Keneth
Yindi akitoa maelezo kuhusu matumizi ya kamera za CCTV na mfumo wa Biometrics
katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma
Mbunge wa Dodoma mjini Anthony Mavunde akizungumza katika
uzinduzi wa matumizi ya kamera za CCTV na Mfumo wa Biometrics katika Hospitali
ya Rufaa ya Dodoma.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni ya Entersoft Limited,Keneth
Yindi akitoa maelezo kuhusu matumizi ya kamera za CCTV na mfumo wa Biometrics
katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa Mbunge wa Dodoma mjini Anthony Mavunde.
Mbunge wa Dodoma mjini Anthony Mavunde akiangalia komputa
inayohifadhi video vinazorekediwa kwenye kamera za CCTV katika Hospitali ya
Rufaa ya Dodoma.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni ya Entersoft Limited,Keneth
Yindi akitoa maelezo kuhusu matumizi ya kamera za CCTV na mfumo wa Biometrics
katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma
Mbunge wa Dodoma mjini Anthony Mavunde akizindua matumizi ya
mfumo wa Biometrics katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.
SHARE
No comments:
Post a Comment