MWANAMUME mmoja amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma mkoani
Mara, kwa makosa ya mauaji ya watu 17, wote wa familia moja, wakazi wa
eneo la Mugaranjabo wilayani humo, kwa kuwakata mapanga wakati wakiwa
nyumbani kwao.
Ikumbukwe kuwa tukio la mauaji ya watu hao 17, na wote wakiwa ni
wanafamilia moja lilitokea mwaka 2010. Aliyefikishwa katika mahakama
hiyo mbele ya hakimu Richard Maganga, ametambuliwa kwa majina ya Sura
Bukaba Sura maarufu kwa majina ya Phinias Yona au Epoda (35), mkazi wa
wilayani Butiama mkoani Mara.
Akisomewa mashitaka yake ya mauaji ya watu 17 hao, Mwendesha Mashitaka
wa Polisi Jonas Kaijage, aliiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa huyo
akiwa na wenzake wapatao 15, ambao wote wakazi wa wilayani humo,
walitenda makosa hayo Februari 16 mwaka 2010 majira ya usiku katika eneo
la Mugaranjabo, nje kidogo ya mji wa Musoma.
Kaijage alisema mtuhumiwa huyo, alitenda kosa hilo akiwa na wenzake hao,
ambao tayari walishakamatwa na kufikishwa mahakamani, ambapo kati yao
wanane walikwishafariki dunia wakiwa mahabusu. Inadaiwa watu hao
walimuua Kawawa Kinguye na wenzake wapatao 16, ambao wote ni wa familia
moja kwa kuwakata mapanga wakati wakiwa nyumbani kwao.
Alisema kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kutekeleza mauaji hayo alitoroka,
ambapo wenzake 15 walikamatwa na kufikishwa mahakamani hapo. Alifafanua
kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 18 mwaka huu, kwa kesi nyingine ya
unyang’anyi wa kutumia silaha katika eneo la Rwamulimi mjini Musoma.
Alisema katika tukio hilo la unyang’anyi wa kutumia silaha, mtuhumiwa
huyo alivamia nyumbani kwa mwananchi mmoja na kuvunja nyumba kwa kutumia
nondo na kufanikiwa kuiba Sh 500,000 taslimu. Alisema kuwa polisi
walifanikiwa kumkamata na kumtambua kuwa alishiriki katika tukio la
mauaji ya watu hao 17 lililotokea mwaka 2010.
Mtuhumiwa huyo baada ya kusomewa mashitaka yake, hakutakiwa kujibu
chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusilikiza
kesi za mauaji. Hakimu Karimu Moshi aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 7
mwaka huu, itakapotajwa tena mahakamani hapo na kuunganishwa na
washitakiwa wengine waliosalia.
Wakati huo huo, mahakama hiyo mbele ya hakimu Richard Maganga,
imemhukumu Robert Kabondo (67) mkazi wa wilayani Butiama, kutumikia
kifungo cha miaka saba jela, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na
dawa ya kulevya aina ya bangi kinyume cha sheria.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa polisi, Kaijage
kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 7 mwaka huu, kwa
kupatikana na dawa hizo zenye uzito wa gramu 97.5 kinyume cha Sheria ya
Kuzuia Dawa ya Kulevya Sura ya Tano ya mwaka 2015.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Kaijage aliiomba mahakama hiyo kutoa
adhabu kali kwa mshitakiwa huyo, kwani dawa za kulevya zinaharibu vijana
wetu na kupunguza nguvu kazi ya taifa. Mshitakiwa huyo aliiomba
mahakama hiyo kumpunguzia adhabu.
Utetezi huo wa mshitakiwa huyo ulitupiliwa mbali na hakimu Maganga,
ambaye alimhukumu kifungo cha miaka saba jela ili kuwa fundisho kwake na
kwa watu wengine wenye tabia au nia ya kufanya hivyo.
IMEANDIKWA NA AHMED MAKONGO-HABARILEO MUSOMA
SHARE
No comments:
Post a Comment