Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefafanua juu ya uteuzi wa wabunge wapya wa Viti Maalumu wa Chama cha Wananchi (CUF).
Imesema
kuwa imesikitishwa na kushangazwa na taarifa za Baraza Kuu la Taifa la
chama hicho kwamba tume hiyo imekiuka kanuni zake katika uteuzi wa
wabunge wanane wa chama hicho ili kujaza nafasi za wazi zilizotokea hivi
karibuni.
Aidha,
imesema chama husika kilipewa fursa ya kupendekeza na kilifanya hivyo,
kabla ya NEC kuanika majina ya wabunge wapya wa CUF katika Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo
yamo katika taarifa ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani
aliyoitoa jana jioni, akizungumzia tuhuma dhidi ya tume hiyo,
inayodaiwa kukiuka kanuni katika uteuzi wa wabunge wanane wa viti
maalumu wa CUF.
Sehemu ya Taarifa ya CUF katika mitandao ya kijamii inayoituhumu NEC inasema; “Kanuni
walizojiwekea wenyewe Tume katika uteuzi wa watu wa kujaza nafasi hizo
zinasema uteuzi huo unafuata mpangilio wa majina, kama ulivyokuwa
umewasilishwa na chama husika wakati wa uteuzi wa wagombea wa ubunge wa
viti maalumu wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
“CUF
ilipeleka orodha yake ambayo haihusishi majina yaliyotangazwa, hivyo
ndiyo kusema hata kama hicho kinachoitwa kufukuzwa uanachama wabunge hao
kingekuwa halali (jambo ambalo si halali kama ilivyokwishaelezwa hapo
juu), basi kwa Kanuni za Tume yenyewe, watu wa kujaza nafasi hizo
wasingekuwa hao waliotangazwa.”
Kailima,
katika taarifa yake, alisema taarifa zinazotolewa katika mitandao
zikihusisha NEC kukihujumu chama hicho ni za kushangaza na kwamba Baraza
Kuu la Uongozi la CUF, linataka kuupotosha umma kuhusu utekelezaji wa
kazi za Tume.
“Chama husika ndicho kinaweza kujua ni nani siyo mwanachama wa chama hicho kwa kipindi cha kujaza nafasi wazi inapotokea,”
alieleza Kailima na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa majina manane
yaliyopendekezwa na CUF kujaza nafasi wazi za wabunge wa viti maalumu ni
miongoni mwa majina 55 yaliyowasilishwa na chama hicho kwa barua yenye
kumbukumbu Namba CUF/AK/DSM/ KM/003/1A/2015/14 ya Septemba 28, 2015
iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad.
SHARE
No comments:
Post a Comment