WAKATI
majaji wawili wa Mahakama Kuu waliopata mgawo wa fedha zilizochotwa
kwenye akaunti ya Tegeta Escrow wakijiuzulu nyadhifa zao, hatua hiyo
sasa huenda ikawa imehamishia joto kwa wanasiasa, viongozi wa dini na
watumishi wa umma ambao nao walinufaika.
Majaji
waliojiuzulu ni Profesa John Ruhangisa, Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, ambaye juzi Ikulu ilitoa taarifa kwa umma ikisema Rais Dk.
John Magufuli ameridhia kujiuzulu kwake na Jaji Aloysis Mujulizi pia wa
mahakama hiyo, ambaye alijiuzulu Mei 16, mwaka huu.
Baada ya
kutajwa kwenye kashfa hiyo, waliokuwa kwenye nyadhifa za kisiasa,
wakiwamo mawaziri na wabunge, waliitwa Baraza la Maadili ya Utumishi wa
Umma, ambako baadhi walihojiwa, ingawa hatua zilizochukuliwa hazijawekwa
wazi.Kwa viongozi wa umma, baadhi walifikishwa mahakamani, ingawa
wengine kesi zilifutwa zikiwa kwenye hatua mbalimbali za usikilizaji.
Homa ya
walionufaika na mgawo huo wa fedha za Escrow, ilianza kupanda baada ya
Serikali kuamua kufufua sakata hilo, lililodhaniwa kuwa limekwisha kwa
kuwafikisha mahakamani hivi karibuni vinara wawili.
Vinara
hao ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, aliyekuwa pia mwanahisa
wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), iliyoletwa
nchini miaka 23 iliyopita, James Rugemalira na Mwenyekiti Mtendaji wa
Kampuni ya Pan African Power (PAP), Habinder Sethi Sigh, waliofikishwa
kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 19 na
kusomewa mashtaka sita, yakiwamo ya uhujumu uchumi.
Julai 3, vigogo hao walifikishwa tena kwenye mahakama hiyo na kuongezewa mashtaka sita, yakiwamo ya utakatishaji fedha.
Kwa jumla
wake mashtaka 12 waliyosomewa Rugemalira na Sethi Julai 3, ni pamoja na
kutakatisha fedha na kuisababisha hasara Serikali ya USD 22, 198,544.60
(Sh 309,461,300,158.27).
Kutokana
na hali hiyo, na hatua ya majaji wawili kuamua kuachia nyadhifa zao, ni
wazi walionufaika na fedha hizo presha zao zitakuwa zinapanda na
kushuka, kutokana na kutojua hatima yao ya ama kuunganishwa au
kutounganishwa kwenye kesi inayoendelea mahakamani.
Miongoni
mwa viongozi wa kisiasa na umma ambao wakati fedha hizo zinatolewa
walikuwa madarakani, ama kwa namna moja ama nyingine walihusika
kuiingiza IPTL nchini, huenda sasa wakawa kwenye wakati mgumu zaidi.
Hii ni
kwa sababu baada ya kutajwa kwenye kashfa hiyo, waliishia kwenye Baraza
la Maadili na wengine kesi zao zikifutwa baada ya kufika mahakamani.
Novemba
2014, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliwataja vigogo wa
Serikali, wanasiasa na viongozi wa dini watatu walionufaika na Akaunti
Tegeta Escrow, huku ikishindwa kuweka wazi walionufaika na sehemu ya
fedha zilizodaiwa kuchotwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ilipokuwa
akaunti hiyo na kupelekwa Benki ya Stanbic.
PAC
wakati ikisema Rugemalira aliwagawia baadhi ya watu fedha kupitia
akaunti zao walizofungua kwenye Benki ya Mkombozi, ilisema sehemu ya
fedha nyingine iliwekwa Stanbic, ambako watu walizichota kwa mifuko ya
plastiki, maarufu kama sandarusi.
SHARE
No comments:
Post a Comment