Kaimu Afisa wa mafunzo Kikosi cha Zimamoto Zanzibar Inspekta Ibrahim
Ali Hassan akionyesha utaratibu bora wa kubeba chupa ya gesi kwa ajili
ya kuzima moto katika mafunzo ya wafanyakazi wa Bohari Kuu ya dawa
Maruhubi.
Mmoja
wa wafanyakazi wa bohari kuu ya dawa Zanzibar Ali Othman Omar (kushoto)
akiuliza suala kuhusu matumizi sahihi ya mtungi wa kuzimia moto katika
mafunzo hayo.
Mkurugenzi
Idara ya Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar Zahrani Ali Hamad akifungua
mafunzo ya siku moja ya kukabiliana na janga la moto kwa wafanyakazi wa
Idara hiyo Ofisini kwao Maruhubi Mjini Zanzibar.
Fatma
Omar Said akiwa katika mafunzo ya vitendo ya kukabiliana na janga la
moto katika mafunzo ya wafanyakazi wa Bohari kuu ya dawa Zanzibar
yaliyofanyika Maruhubi Mjini Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga.
Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar
Sehemu
zenye mikusanyiko ya watu zikiwemo Taasisi za Serikali na watu binafsi
zinatakiwa kuwa na vifaa vya huduma ya kwanza vya kupambana na janga la
moto na watu wenye taaluma ya kutumia vifaa hivyo.
Kaimu
Afisa wa mafunzo Inspekta Ibrahim Ali Hassan wa Kikosi cha Zimamoto na
Uokozi Zanzibar amesema sheria No. 7 ya mwaka 1999 ya Idara hiyo imewapa
uwezo wa kuzifungia sehemu hizo iwapo zitashindwa kuweka vifaa na watu
wenye uwezo wa kuzima moto.
Inspecta
Ibrahim ametoa maelezo hayo alipokuwa akitoa mafunzo ya kukabiliana na
moto kwa wafanyakazi wa Idara ya Bohari Kuu ya dawa Maruhubi.
Amesema
lengo la kuwepo sheria hiyo ni kujaribu kuokoa maisha ya wananachi na
mali zao wakati wa janga la moto ambalo linasababisha athari kubwa
katika jamii.
Hata
hivyo amesema bado taasisi nyingi za Serikali na binafsi hazijaona
umuhimu wa kuweka vifaa vya huduma ya kwanza vya kuzimia moto na kuwapa
mafunzo wafanyakazi wao .
Ameipongeza
Wizara ya Afya kwa kujali kuwapatia mafunzo ya kukabiliana na moto
wafanyakazi wa vitengo vyake mbali mbali na kuimarisha huduma hiyo
katika taasisi zake kila mwaka.
Katika
kukabiliana na janga la moto, Inspekta Ibrahim Ali Hassan aliwataka
wafanyakazi wa bohari kuu kuacha fadhaa na kutumia njia za kitaalamu kwa
kuondosha vitu ambavyo havijaanza kuungua, kuunyima moto hewa na kutia
maji kwa moto wa kuni.
Aidha
amewashauri wananchi kuanzisha utaratibu wa kuweka chupa ya kuzimia
moto katika majumba yao na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar
kinatoa mafunzo ya matumizi sahihi ya kifaa hicho bila malipo.
Amesema
binadamu hawezi kuishi bila kutegemea moto na moto ni adui mpenzi wa
binadamu hivyo tahadhari inahitajika wakati wote katika kujilinda.
Akizindua
mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Bohari Kuu ya dawa Zanzibar Zahran
Ali Hamad ametaka kila mfanyakazi wa taasisi hiyo kuwa na uwezo wa
kujilinda na moto yeye mwenyewe na mali iliyopo ndani.
Amesema
bohari kuu ni taasisi muhimu katika ustawi wa maisha ya wananchi wa
Zanzibar na imeweka mkazo kuhusu mafunzo hayo kwa wafanyakazi wote hivyo
amewashauri kuyapokea kwa umuhimu wake.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
SHARE
No comments:
Post a Comment