Maoni ya wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani leo hii
wanazungumzia juu ya athari za ghasia zilizotokea wakati wa mkutano wa
nchi zinazoongoza kiviwanda, G20 mjini Hamburg.
Mhariri anasema waliofanya ghasia walivuruga maandamano yalilyokuwa
halali. Waandalizi wa maandamano hayo walikuwa na lengo la kusisitiza
umuhimu wa kulinda mazingira na vile vile umuhimu wa kuyazingatia
madhila ya wakimbizi. Mhariri huyo wa gazeti la Kölner Stadtanzeiger
pia anatilia maanani kwamba waandamanaji hao walikuwa na nia ya kupinga
sera za marais wa Urusi Vladimir Puttin,rais wa Uturuki Recep Tayyip
Erdogan na rais wa Marekani Donald Trump. Vilevile mhariri wa gazeti
hilo anawataka waandamanaji wanaolemea mrengo wa shoto wajiweke kando na
vitendo vya ghasia katika siku za usoni.Naye mhariri wa gazeti la Mittledeutsche anasema kiwango cha ghasia zilizotokea katika mji wa Hamburg hakijawahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia. Mhariri huyo anaendelea kueleza kwamba baraza la seneti la mji wa Hamburg halikujiandaa vyema kukabiliana na ghasia zilizotokea. Mhariri wa gazeti la Süddeutsche anaiunga mkono hoja hiyo kwa kumtaka meya wa mji wa Hamburg Olaf Scholz ajiuzulu badala ya kuwalaumu wengine.
Wahariri leo pia wanazungumzia juu ya kuimarika kwa upinzani dhidi ya sera za rais wa Uturuki RecepTayyip Erdogan zinazohatarisha demokrasia nchini humo. Maalfu ya wapinzani walishiriki kwenye maandamano yaliyofanyika katika mji wa Istanbul. Mhariri wa gazeti la Die Welt anasema lingekuwa jambo la manufaaa kama maandamano hayo yangelikuwa ndio mwanzo wa vuguvugu la kiraia nchini Uturuki.
Na mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker anatilia maanani upinzani dhidi ya rais Erdogan unaoendelea kupamba moto na huku sauti zinazidi kupazwa dhidi yake. Mhariri wa gazeti hilo ameandika maoni yake kwa kusema hata hivyo Erdogan ni kiongozi anayefahamika kwa kutouvumilia upinzani na ni wazi kwamba katika muda usio mrefu atachukua hatua dhidi ya wapinzani nchini mwake.
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment