Na: Thobias Robert – MAELEZO
Wanawake wa Jumuiya ya Tanzania
Fellowship of churches kutoka makanisa mbalimbali wanatarajia kufanya
kongamano la maombi na dua maalumu kwaajili ya kumuombea ulinzi Rais
Dkt. John Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya katika kutetea wanyonge na
kulinda rasilimali za nchi.
Hayo yamesemwa leo, Jijini Dar
es Salaam na Mratibu wa kongamano hilo Mchungaji Deborah Malassy, wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo la siku tatu
linalotarajia kuanza Julai 20 hadi Julai 23 mwaka huu katika ukumbi wa
Millenium Tower ulioko Jijini humo.
Mchungaji Malassy amesema kuwa,
kongamano hilo linalenga kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kuipatia
Nchi ya Tanzania Kiongozi ambaye Watanzania walikuwa wanamhitaji kwa
muda mrefu ili kulinda amani ya Nchi, kutetea wanyonge pamoja na
kusimamia rasilimali za nchi pamoja na uadilifu kazini.
“Mwaka huu, ni mwaka wa Baraka na
Neema kwa Taifa la Tanzania kufuatia matendo makuu ya Mungu
aliyotutendea Watanzania, hasa kuwa na kiongozi mwenye uwezo, mcha
Mungu, mtiifu mkweli na asiyependa mapato ya Serikali kupotea,” amesema
Mchungaji Malassy.
Aidha amesema, kwa muda mfupi
aliokaa madarakani, Rais Magufuli amefanya mambo mengi na kila Mtanzania
ameyashuhudia kama vile kurejesha maadili kwa watumishi wa Umma,
kuwaondoa viongozi wala rushwa pamoja na kutetea rasilimali za Tanzania
zilizokuwa zikisafirishwa nje ya nchi, mfano mchanga wa dhahabu.
Vile vile kongamano hilo litatoa
elimu kwa wanawake juu ya kujilinda dhidi ya unyasasaji wa kijinsia, na
kuwajengea Wanawake uwezo wa namna ya kujikwamua kiuchumi pamoja na
kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia unaotokana na rushwa ya ngono.
Akinukuu Maneno ya kitabu
kitakatifu kutoka kitabu cha Nyakati wa Pili 7:18, Mchungaji Malassy
amesema, “Ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu wataziacha njia zao
mbaya wakajinyenyekesha na kuomba nami nitasikia kutoka mbinguni na
nitaiponya nchi yao,” kwahiyo wao kama wakina mama walioitwa kulia na
kuomboleza kwa ajili ya Taifa lao wanayo haki ya kufunga na kuomboleza
kwaajili ya kuliombea Taifa.
Mgeni Rasmi wa Kongamano hilo
anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samia Suluhu Hassan. Vile vile, viongozi wanawake kutoka nchi za Afrika
ya Kusini, Marekani, Uingereza, Zambia, Kenya, Kongo na Botswana pia
watakuwepo katika kongamano hilo.
Kongamano hilo limekuwa
likifanyika kila mwaka mwezi Disemba na Julai ambapo hufanyika pamoja na
mkesha mkubwa wa maombi katika uwanja wa Taifa, lengo likiwa ni
kuombea amani, utulivu, upendo pamoja na kuwaombea viongozi wa Serikali
ili waongoze Nchi kwa hekima na busara kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
SHARE
No comments:
Post a Comment