TRA

TRA

Monday, July 10, 2017

WAVAMIZI WA RELI WAPEWA MIEZI SITA KUONDOKA HIFDHI YA RELI

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !
 

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngoyani(pichani juu anayezungumza), ametoa Miezi sita kwa wakazi wa Mpanda Mkoani Katavi kuondoka katika maeneo ya hifadhi za Reli ili kupisha maboresho yanayoendelea kufanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRL) kwenye miundombinu yake.
Ametoa agizo hilo wakati akiongea na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo Mkoani Mpanda na kusema ni wakati sasa kwa wananchi kufuata sheria kwa kutovamia miundombinu hiyo.
“Ninatoa miezi sita kuanzia sasa, itakapofika Mwezi Januari mwakani wananchi wote watakaokuwa ndani ya hifadhi ya reli watabomolewa nyumba zao kwa kuzingatia sheria zinazolinda miundombinu,” alisisitiza Eng. Ngonyani.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mpanda kusimamia zoezi la wananchi kuhama na kuhakikisha kila aliyevamia miundombinu hiyo anabomoa nyumba yake kabla ya sheria kufata mkondo wake.
Aidha, Eng. Ngonyani amewatahadharisha wafanyakazi wa Wakala wa barabara nchini (TANROADS) kuzingatia maslahi mapana ya Taifa wakati wa kutafuta zabuni kwa kufanya hivyo watakuwa wanamuunga Mkono Mhe. Rais Dkt. John Magufuli.
Katika hatua nyingine Eng. Ngonyani amekagua barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (76.6KM), Sumbawanga-Kanazi (75KM) ambapo ameiagiza TANROADS Mkoa wa Rukwa kuweka mizani katika barabara zinazojengwa ili kudhibiti magari makubwa yanayozidisha uzito na kusababisha uharibifu kwa barabara katika Mkoa huo.
“Ni wakati sasa wanaotoa huduma za usafirishaji wa mizigo kufuata  sheria na kubeba mzigo wa uzito unaostahili sababu madereva hao hao wakienda nchi za jirani wanafuata sheria kwa umakini, SUMATRA simamieni utoaji wa leseni kwa magari ya abiria na mizigo kwa kuzingatia uzito wa magari ili kuziweshesha barabara zetu zidumu,” alisisitiza Eng. Ngonyani.
Kwa upande wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa, Eng. Msuka Mkina amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa Wakala utahakikisha Mizani inawekwa sehemu za barabara  ili kubaini Magari yanayozidisha uzito na kuyachukulia hatua za kisheria.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani yupo katika Ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Viwanja vya Ndege, Ujenzi wa Nyumba za viongozi, huduma za mawasiliano ya simu   na Madaraja katika Mkoa wa Katavi na Rukwa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.





Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger