Said Mwishehe
KWA Ujinga Wangu nimeipokea kwa mikono miwili kauli ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete ambayo anaelezea umuhimu wa utawala bora na kuheshimu sheria.
Hivyo akazitaka serikali barani Afrika zisichukulie vyama vya upinzani kuwa maadui. Akaongeza kuwa wanasiasa wa upinzani wasichukuliwe na Serikali kuwa ni maadui.
JAKAYA KIKWETE
Rais huyo mstaafu bila kusita akawashauri wabunge wa vyama tawala barani Afrika kujenga utamaduni wa kuzikoa Serikali zao wanapoona ilani za uchaguzi hazitekelezwi.
Kwa Ujinga Wangu nikaanza kuwaza Kikwete amefikiria nini lakini nikapata jibu amekuwa na uzoefu wa kutosha mbali tu ya kuwa amewahi kuwa Rais lakini anatambua changamoto zilizopo kwenye nchi za Afrika na hasa uhusiano kati ya vyama vya upinzani na Serikali zao.
Kikwete ambaye ni maarufu kwa jina la JK alitoa kauli hiyo alipokuwa akijadili mada iliyowasilishwa juzi (majuzi) na Barney Pityana ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kuhusu utawala bora na sheria.
Hivyo akaeleza wazi vyama tawala na Serikali zao havina sababu ya kuvichukia vyama vya upinzani au viongozi wake huku akihimiza kuishi kwa amani na mshikamano.
Kwa Ujinga Wangu ni sawa Kikwete ametoa kauli hiyo kwa ajili ya viongozi wa Serikali katika Bara la Afrika lakini kimsingi kila nchi inayo jukumu la kuichambua kauli yake.
Hivyo kwa Tanzania nako iko haja ya kuijadili kwa kina ili pale ambapo kuna mambo yanaenda tofauti na utawala bora basi walioko kwenye mamlaka warekebishe.
Naangalia hali ya vyama vya siasa vya upinzani nchi kwetu. Naangalia maisha ya wanasiasa wa upinzani kwa sasa. Naangalia namna ambavyo wabunge wanaotokana na chama tawala na kisha nautafakari utawala bora. Naangalia mwenendo wa demokrasi nchini kwetu. Nikiri kuna mahali tunapaswa kujitazama upya.
Lazima nikubali na ndio ukweli Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopo kwenye Bara Afrika ambayo inaheshimu utawala bora. Viongozi wa Tanzania wanatambua uwepo demokrasia na misingi yake na hivyo imekuwa huru kuiacha ifanye kazi yake.
Hata hivyo lazima tukubali kuna baadhi ya maeneo demokrasia inaonekana kutopata nafasi yake. Viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakitoa kauli za kulalamika kuwa wamebanwa na hawana nafasi ya kufanya siasa tena.
Kila wakitaka kuzungumza na wananchi wanajikuwa wakiwa kwenye vikwazo. Ni malalamiko ambayo yameendelea kushika kasi siku hadi siku. Sawa uchaguzi mkuu ulishakwisha mwaka 2015 na sasa Serikali inaendelea kutimiza majukumu yake. Hata hivyo kwenye demokrasia haiwezi kuwa kikwazo kwa wapinzani nao kufanya siasa.
Kwa Ujinga Wangu kama kuna eneo ambalo wanasiasa wa upinzani walikuwa wanafurahia kuifanya siasa basi na hapa nchini kwetu na utamaduni huo lazima uendeleee.
Kwa kuwa tulikubali wenyewe kuwa tuwe na utawala bora unaoheshimu sheria pamoja na demokrasia pana ni vema ikaachwa ikaendelea.
Pale ambapo kuna mambo yanaonekana kutokwenda sawa wapinzani waseme na Serikali ikijiridhisha itekeleze. Si dhambi kusikiliza wapinzani wanazungumzia nini kwa maslahi ya nchi yao.Wapewe nafasi ya kuelezea changamoto zilizopo na Serikali ichukue hatua.
Kwa Ujinga Wangu natambua vyama vya siasa vinapatika lakini Watanzania watabaki pale pale. Najua viongozi wa kisiasa nao wataongoza na baadae watapumzika kwenye siasa lakini Tanzania itabaki kuwa ile ile.
Tusiruhusu vyama vya siasa kutugawa na kujenga uadui kati ya watu na watu. Ni vema mwanasiasa anayeamini kwenye vyama vya upinzani akaishi maisha yenye furaha kama ambavyo anaishi mwanasiasa aliyeoko chama tawala.
Natambua wapo viongozi wa kisiasa wa vyama vya upinzani ambao wanatumia uwepo wa demokrasia kujenga chuki kwa Serikali. Wapo wenye kuzusha mambo ambayo wakati mwingine si mazuri katika maisha yetu na ustawi wa maendeleo ya nchi yetu.
Wanasiasa wa aina hiyo hata kama ndio kuna demokrasia lazima waangaliwe kwa jicho la aina yake na ikiwezekana wachukuliwe hatua kabla ya kuleta madhara.
Kwa Ujinga Wangu ni vema Serikali ikatambua kuwa upinzani si maana yake haustahili kuzungumza lolote kwa nchi yako. Itoe nafasi wapinzani waseme, waeleze wanachoona kinafaa kwa ajili ya nchi yao.
Kwa bahati mbaya kuna kundi kubwa la wanasiasa iwe wa upinzani au wa chama tawaka wanaogopa kusema hadharani na matokeo yake wanajaza mambo mengi kwenye moyo. Ni vema watu wakaachwa huru waseme.
Kikwete akiwa madarakani alikubali kukosolewa na wakati mwingine wapo waliotumia vibaya demokrasia kwa kumshambulia na kumdhiki lakini aliziba masiko na kufumba macho na mambo yakaenda.
Yale ambayo aliona yanafaa aliyafanyia kazi hata kama yamesemwa na mpinzani. Hivyo viongozi wa Bara la Afrika ipo haja ya kujifunza kutoka kwake na ndio maana aliamua kutoa kauli hiyo kwa ajili ya Bara la Afrika. Ahsante Kikwete Afrika imekuelewa na mimi nimekuelewa vema.
Tuwasiliane
0713833822
SHARE









No comments:
Post a Comment