Julian Msacky
“Kama ni kweli tunapenda amani kama viongozi wanavyosema kwa
nini bara letu limezungukwa na vita?”.
Alihoji hivyo Rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo
wakati akizungumza katika mkutano wa Jukwaa la Viongozi Afrika maarufu kama The
Africa Leadership Forum (ALF).
Obasanjo hakuishia hapo bali alionesha masikitiko yake namna
Libya ilivyotumbukia kwenye vita na amani haijapatikana hadi leo.
Ni kwa nini Rais huyo anahoji hivyo? Hili ni swali muhimu kwa
sababu viongozi wa Afrika wamekuwa mabingwa wa kuhubiri amani na upendo kwa
shingo upande.
Matokeo yake wanaingiza mataifa yao kwenye vita
visivyokwisha. Chanzo kikubwa cha machafuko ni wanasiasa wenyewe, lakini
waathirika ni raia.
Kwa sababu hiyo wanahubiri amani na mikononi wamebeba
majambia ya kubaki madarakani hata kwa kumwaga damu.
Hawapo tayari kushindwa hata kwa sanduku la kura. Ndiyo maana
leo hii wananchi wakisikia kitu kinachoitwa uchaguzi mioyo yao inashtuka.
Ndiko viongozi wa Afrika walikofikisha raia wao. Hii ikiwa na
maana kuwa kipindi cha uchaguzi ni kipindi cha hofu.
Hii ni kwa sababu wananchi huweka mguu sawa ili wajue pa
kukimbilia kwani ghasia zinaweza kuibuka wakati wowote.
Hii ndiyo Afrika ambayo viongozi wake hujigamba ni walezi wazuri
wa demokrasia, utawala bora na sheria.
Lakini matokeo yake wanatumia nyundo kufifisha mifumo hiyo
kwa kisingizio cha kulinda amani wakati si kweli.
Ni kwa sababu hiyo Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alitumia
mkutano huo uliofanyika Johannesburg, Afrika Kusini kuwakumbusha viongozi
umuhimu wa kutojenga chuki na vyama vya upinzani.
Kikwete ambaye anasifiwa kwa kutoa fursa kubwa kwa wapinzani
kusema, aliwaambia viongozi wa vyama tawala barani Afrika kwamba upinzani ni
ufunguo wa demokrasia.
Hakuishia hapo bali aliendelea kusisitiza kuwa viongozi
waliopo madarakani watakuwa wanafanya makosa kwa kuwachukulia wapinzani kama
maadui.
Kusema kweli hizi ni nasaha muhimu kwa viongozi wa bara letu
kwa sababu bila kulea vyama hivyo badala ya amani ni vurugu.
Badala ya demokrasia ni utawala wa mabavu. Badala ya utawala
bora na sheria ni maangamizi.
Kwa kutozingatia ukweli huo mchungu Afrika imejikuta ikingia
kwenye machafuko ya mara kwa mara kwa sababu baadhi ya viongozi wana shingo
ngumu.
Swali sasa ni je, ni viongozi wangapi Afrika wanahimili
anachosema Kikwete kwa ustawi wa Afrika na watu wake?.
Rais mstaafu Jakaya Kikwete
Viongozi waliopo madarakani ni muhimu kuzingatia ushauri wa
Kikwete kwani una maslahi mapana zaidi kwa Afrika.
Tabia ya viongozi waliopo madarakani kujiona wao ndiyo alfa
na omega, ni kujidanganya na kushindwa kusoma alama za nyakati.
Hivi haikuandikwa kwamba ajikwezaye atashushwa na ajishushae
atakwezwa?
Au haikusema kwamba mkiwapenda wale mnaowapenda tu mwapata
thawabu gani?
Kwa msingi huo viongozi wa Afrika ni lazima wajenge mfumo wa
kuendesha siasa kwa njia ya kuvumiliana.
Wajifunze kuendesha siasa kwa kutoa pia fursa kwa wengine ili
sauti zao zisikike kwani ndivyo tangazo la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa
linavyotaka.
Historia inaonesha kwamba kutoa fursa kwa raia au asasi
nyingine za kijamii kutoa hisia zao inajenga zaidi kuliko kubomoa.
Ndiyo maana Waziri Mkuu akiwa Tabora aliwataka viongozi
wasizue wananchi kutumia mabango kwani wanatoa hisia zao/kuwasilisha matatizo
yao.
Huo ndiyo ukomavu wa kisiasa na siasa maana yake ni pamoja na
kuhimili changamoto/upinzani kutoka kwa wadau wengine.
Ni imani ya Waafrika na Watanzania kwa ujumla kwamba ujumbe
wa Kikwete utakuwa chachu ya kupanua wigo wa demokrasia katika bara letu la
Afrika.
“Utawala bora bila serikali imara ni jambo lisilowezekana,”
alisema Kikwete na kuhimiza uwepo uwiano sawa kwa wabunge kutoa hoja zao.
Afrika ambayo inapitia changamoto nyingi za ujio wa mfumo wa
vyama vingi vya siasa ni lazima ijifunze namna ya kuendesha mfumo huo bila kuumiza
wengine.
Ili Afrika ibaki salama chini ya mfumo huo sharti mfumo wa
utawala bora na sheria uheshimiwi ili kurutubisha demokrasia.
Ni lazima pia uwepo uvumilivu wa kweli kisiasa badala ya
kujengeana chuki na uhasama bila sababu za msingi.
SHARE









No comments:
Post a Comment