MGOMO
wa kutohudhuria mahakamani uliotangazwa na Rais wa Chama cha Mawakili
Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, umepingwa na kukosa kuungwa mkono baada
ya mawakili kujitokeza kwa wingi mahakamani jana huku wakieleza kuwa ni
wazo la mtu mmoja na kwamba huenda wanaogoma hawana kesi katika siku
hizo mbili.
Katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Arusha, Kagera, Geita na
Mara, gazeti hili limeshuhudia mawakili wakiendelea kuwawakilisha wateja
wao licha ya agizo la TLS chini ya Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa
Singida Mashariki (Chadema), kuwaagiza kugoma kwa siku mbili; jana na
leo.
Lissu aliwaeleza waandishi wa habari Jumapili kuwa Baraza la Uongozi la
TLS limetangaza mgomo wa siku mbili, kupinga uharibifu uliotokana na
mlipuko kwenye Ofisi za Kampuni ya Mawakili ya Immma iliyoko Upanga
katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Lakini jana, mawakili walikuwapo mahakamani kama walivyoshuhudiwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam uwepo wa mawakili
wachache ambao ni wakongwe huku idadi kubwa ikiwa ni ya mawakili wapya
ambao huenda waliingia kwenye tasnia hiyo hivi karibuni.
Mmoja wa mawakili hao alisema baada ya tukio hilo, kama chama walipaswa
kuitwa na kukaa kujadiliana ni jambo gani wafanye na sio wazo la mtu
mmoja kwamba wagome. “Haya ni makosa makubwa na ndio maana unaona kuna
mgawanyiko kila mtu anaangalia maslahi yake.
Baada ya tukio tungeitwa ili tujadiliane, lakini hali hii inaonesha kuwa
hili ni wazo la mtu mmoja na halitekelezeki,” alisema wakili huyo
aliyeomba asitajwe jina. Alifafanua kuwa mawakili wengi wamepima uzito
wa agizo hilo na kuona kwamba tukio lililotokea si la kuhusishwa moja
kwa moja na Polisi kwa kuwa inawezekana kuna tatizo baina ya kampuni na
wateja au majambazi wameamua kufanya hivyo.
Wakili mwingine alidai kuwa hawezi kufanya mgomo kwa sababu hauna
uhusiano na uanasheria. Alisema wao wanawawakilisha wateja wao hivyo
kitendo cha kutofika mahakamani kwa sababu ya mgomo ni kugomea wateja
ambao ndio wamewaajiri.
Miongoni mwa mahakimu, aliliambia gazeti hili kuwa shughuli za mahakama
zinaendelea kama kawaida na ameona uwepo wa mawakili katika vyumba vya
mahakama. Alisema katika kesi zote zilizopo mahakamani hapo ambazo
washitakiwa wanawakilishwa na mawakili, walihudhuria, hali ambayo haina
utofauti na wakati mwingine.
Baadhi ya mawakili ikiwemo Jeremiah Ntobesya, Nehemiah Nkoko, Alex
Mgongolwa ambao licha ya kukataa kuzungumzia mgomo huo, walikuwepo
mahakamani kuwawakilisha wateja wao. Kwa upande wa Mahakama Kuu,
mawakili walijitokeza kwa wingi kuwawakilisha wateja wao.
Katika Kanda ya Ziwa, mawakili wa kujitegemea wanaofanya kazi katika
Mahakama Kuu ya Kanda ya Mwanza na mahakama za wilaya na mkoa kwa mikoa
ya Mwanza, Mara na Geita, wameendelea na shughuli zao za kimahakama kama
kawaida na hakuna mgomo wowote ulioripotiwa kutokea.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Jaji Robert Makaramba alisema shughuli za
mahakama zimeendelea vizuri na hakuna mawakili waliojitokeza kugoma.
Alisema Jaji Mkuu ndiye mtu pekee anayeweza kutoa maamuzi ya mawakili
kuja mahakamani au kutohudhuria mahakamani kutokana na kuwa na dhamana
ya kisheria ya kuwasimamia mawakili hao.
Alisema kimsingi mgomo huo, hauwezi kuathiri mahakama, isipokuwa kwa
sehemu kubwa utawaathiri mawakili wenyewe na wateja wao, ambao aliwatoa
hofu wananchi wenye mashauri mahakamani waendelee kupeleka mashauri yao
na yatasikilizwa kwa mujibu wa taratibu za mahakamani.
“Maelekezo tunayofuata sisi kama Mahakama juu ya utendaji kazi wetu ni
ya Kaimu Jaji Mkuu na siyo ya mawakili,” alisisitiza Jaji Makaramba, na
kuonya kuwa hatua iliyochukuliwa na mawakili hao ya kuitisha mgomo,
inalenga kuiacha njiapanda mahakama ambayo imepewa jukumu la kuwatumikia
wananchi.
Aliitaka TLS kama zilivyo taaluma, zao wana miiko na maadili ya utendaji
kazi wao ikiwa ni pamoja na kutoshiriki kwenye mambo ambayo hayatoi
huduma kwa wananchi. “Sitaki kuwasemea TLS wana mamlaka na taratibu zao
za kufanya kazi, lakini kwa watakaoacha kufika kazini, taratibu
zinajulikana mahakamani, tutakuuliza kwa nini hujaja mahakamani,”
alifafanua Jaji Makaramba.
Naye Mratibu wa TLS Kanda ya Ziwa, Amri Linusi alisema kutokana na
shughuli za kimahakama wapo baadhi ya mawakili waliohudhuria mahakamani
na ambao hawakwenda. “Katika hili la mgomo wa mawakili kwenda kutokwenda
mahakamani, limekuwa na interpretation (tafsiri) tofauti kwa tukio la
kuvamiwa kwa Ofisi ya Kampuni ya Mawakili ya Immma, wengine wanasema ni
siasa na wengine wanadai ni maslahi ya watu”, alifafanua.
Kwa upande wake, Wakili Mande Remigius alisema mawakili wameshindwa
kugoma kwa sababu maamuzi ya kugoma yamechukuliwa kwa haraka bila
kushirikisha Mahakama na Wizara ya Sheria na Katiba nchini.
“Katika mgomo huo watakaoathirika sio mahakama bali ni wananchi ambao
hawana hatia yoyote, tuwa kama mawakili tuna wajibu kwa wateja wetu
kuwasimamia haki zao, kwa mantinki hiyo ni vigumu kufanya mgomo
unamuathiri mteja,” alieleza Remigius.
Gazeti hili lilitembelea Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na Mahakama ya
Biashara na Wilaya ya Nyamagana na kuwakuta baadhi ya mawakili wakiwa
kazini huku shughuli za kimahakama zikiendelea kama kawaida.
Mkoani Arusha, mawakili wanachama wa TLS walisema hawawezi kuunga mkono
mgomo huo kwa kuwa ni batili na unakiuka maadili ya taaluma hiyo. Wakili
Pares Parpay alisema haungi mkono mgomo huo kwa sababu ameingia
mikataba na wateja wake ambao ni wananchi na tayari ameshalipwa
mamilioni ya fedha kwa kazi hiyo hivyo kugoma ni kumsaliti mteja wake.
Alisema ni aibu kwa mtu kama yeye kuamua kutoka usingizini na kuunga
mkono mgomo wa kutokwenda mahakamani kwani mteja wake atashindwa
kumwelewa na kauli za namna hiyo zinapaswa kuangaliwa upya kwani
zinaweza kutuingiza mahali pabaya bila ya sababu za msingi.
“Sisi kazi yetu ni kuwatetea wateja wetu na kuunga mkono mgomo ni
kumwonea mteja wangu aliyenipa pesa nyingi kufanyia kazi mahakamani kwa
niaba yake,” alisema na kuitaka TLS kuviacha vyombo vya usalama kufanya
kazi yake kikamilifu ili wahusika wachukuliwa hatua kali.
Naye Edmund Ngemela alipinga kuunga mkono mgomo na kueleza kuwa kufanya
hivyo ni kuidhalilisha taaluma ya kuwadhalilisha wateja walioingia nao
mkataba wa kufanya kazi mahakamani. Alisema mgomo ulipaswa kushirikisha
pande zote ikiwemo Mahakama na kama hilo halikufanyika basi mgomo huo ni
batili.
Naye Albert Msando alisema ni vigumu kwake kugoma kwani alikuwa na kesi
zenye hati ya dharura ya usikilizwaji na kama angegoma zingefutwa na
ingekuwa hatari kwake. Msando alisema nchi ni ya amani na kila mmoja
anahitaji amani na tukio la mlipuko Immma linalaaniwa na kila wakili,
lakini suala la kugoma ni suala binafsi linalopaswa kuangaliwa kwa
mapana zaidi na siyo kukurupuka.
Wakili Moses Mahuna alisema haoni sababu ya kugoma kwani kugoma ni
kujidanganya kwa kuchukua fedha bila kufanyika kazi, kitu ambacho
kinaweza kutafsiriwa kuwa ni utapeli.
Kaimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Deusdedit Kamugisha
alisema jana alikuwa na kesi tano katika mahakama hiyo na kesi zote
zilikuwa na mawakili wa kujitegemea na wale wa serikali, hivyo hakuona
athari yoyote ya mgomo.
Mkoani Mbeya, mawakili mkoani humo wameiuta msimamo wa Lissu kuwa wenye
kulenga maslahi yake binafsi na si wanataaluma hiyo. Sambwee Shitambala
na Kambu Habibu ni miongoni mwa mawakili ambao wamesema maamuzi ya
Lissu, hayana tija kwa mawakili wengine ambapo waliyasema hayo walipotoa
maoni yao, walipozungumza na gazeti hili jana katika viunga vya
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.
Wakili Shitambala alisema alichofanya Lissu ni ubinafsi, kwani
amelazimika kutoa tamko kutokana na ofisi ya mawakili wanaomtetea yeye
kwenye kesi zake imeungua, lakini vitendo vinavyowakuta mawakili kila
siku katika utendaji wa kazi zao hajawahi kusema chochote.
Alisema TLS ni chama cha wasomi, hivyo ilipaswa kufuata utaratibu kwa
baadhi ya wawakilishi kwenye mikoa kuitwa au kutuma barua ya tamko hilo
kiofisi, lakini hakuna kilichofanyika zaidi ya kiongozi huyo kutoa tamko
lake binafsi.
Naye Wakili Habibu alisema tayari walikuwa na mashauri mbalimbali
mahakamani hivyo kukubali kugoma, kutasababisha mashauri hayo kufutwa na
kuongeza kuwa tamko la Tundu Lissu, wamelipata kupitia mitandao ya
kijamii hivyo limedhihirisha kuwa na maslahi binafsi na siyo tamko la
Chama.
Kwa upande wake, Msajili Msaidizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, George
Helbert alisema mgomo wa mawakili haujaathiri utendaji wa kazi za
mahakama kwani kutokuwepo kwa wakili mahakamani kunaweza kuwa na sababu
nyingi ikiwemo kuwa na ratiba zingine.
Nacho Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimedai mgomo wa siku
mbili uliotangazwa nchini, hauwezi kuwathiri wateja wao kwa hali yoyote
ile kwani unalenga kuonesha nafasi ya wanataaluma hao kwa jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo- Bisimba alisema hayo jana
jijini Dar es Salaam wakati chama chake kilipoungana na wanaharakati wa
haki za binadamu kwa madai ya kuungana na mawakili wengine, wakipinga
kitendo cha kulipuliwa kwa ofisi za Immma usiku wa manane, Jumamosi
iliyopita.
LHRC pamoja na Lissu jana walikusanyika katika ofisi za kituo hicho
wakiwa wamevalia nguo nyeusi na kufunga vitambaa vyeusi, na kudai kuwa
wanaungana na mawakili wengine katika mgomo huo ambao haukufanikiwa.
Bisimba alililaumu Jeshi la Polisi akidai hawana imani nalo katika
kuchunguza shauri hilo, madai ambayo yanakinzana na Mkurugenzi Mshirika
wa Immma, Sadoki Magai aliyesema wanasheria hao wanaliamini Jeshi la
Polisi kwa uchunguzi wake na hawapendi kuweka hisia za tukio lililotokea
na chochote.
Imeandikwa na Francisca Emmanuel, Lucy Lyatuu (Dar), Nashon Kennedy
(Mwanza), John Mhala (Arusha), Joachim Nyambo (Mbeya). - HABARILEO
SHARE
No comments:
Post a Comment